Wakati Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu akiwa nje kwa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani kwa makosa matatu yakiwamo ya uchochezi, Jeshi la polisi mkoani Geita limevamia Hoteli ya KG iliyopo mjini Geita aliyokuwa amefikia Katibu wa Chadema Kanda ya Ziwa, Meshack Miku na Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Geita, Neema Chazaile na kuwashikilia kwa tuhuma za uchochezi wa kutumia mitandao ya kijamii.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa uongozi wa Chadema Mkoa wa Geita na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa, Mponjoli Mwabulambo zimedai kuwa katibu huyo alikamatwa jana saa 12 asubuhi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Geita, Sudy Mtanyagala alidai kwamba askari wa polisi zaidi ya 10 wakiongozwa na Kamanda wa Upelelezi Mkoa (RCO) waliizunguka hoteli aliyokuwa amelala katibu huyo wakidai wanatafuta majambazi yenye silaha.
Mtanyagala alidai kuwa polisi hao waliingia chumba baada ya chumba na walipofika katika chumba cha mwisho ambacho ndicho alichokuwa amelala katibu huyo walimkamata na kuchukua simu yake.
Alisema baada ya kumkamata walisoma nyaraka za chama alizokuwa nazo kisha kumtaka yeye na mwenyekiti wa Bavicha kuongozana na polisi hadi kituoni kwa uchunguzi zaidi.
Alisema katibu huyo wa kanda pamoja na mwenyekiti wa Bavicha mkoa walikuwa wakijiandaa kwa kwenda katika ziara Wilaya ya Nyang’wale ambako wangefanya mikutano ya ndani na viongozi wa chama hicho.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Geita, Hellena Thobias alisema walipata taarifa za kukamatwa kwa viongozi hao asubuhi na kufika polisi.
Alisema baada ya kufika polisi, maelezo yalibadilika na kuelezwa katibu wao anatuhumiwa kwa uchochezi kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Alisema wamejitahidi kuomba dhamana lakini imeshindikana baada ya kuelezwa kuwa watuhumiwa hao watakuwa chini ya uangalizi wa polisi kwa uchunguzi zaidi.
“Polisi wametunyima dhamana hadi saa 10 jioni tuko polisi tumeomba dhamana wamekataa sijui ni sheria gani inayomzuia mtu kupata dhamana lakini pia sijui ni sheria gani ya polisi kumnyang’anya mtu simu yake bila ridhaa na kuichunguza. Hatutanyamaza juu ya uonevu huu,” alisema.
Alisema Serikali imekataza mikutano ya hadhara na kueleza kusikitishwa kwake na hatua ya jeshi la polisi kufuatilia hadi mikutano ya ndani ya chama hicho ambayo ni haki yao kikatiba.
Akizungumza kwa simu na mwandishi, Kamanda Mwabulambo alikiri jeshi lake kuwashikilia katibu huyo wa Chadema wa kanda na mwenyekiti wa Bavicha mkoa lakini akasema yupo nje ya ofisi hivyo hawezi kulizungumzia jambo hilo kwa undani.
Social Plugin