JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia mkazi wa Olasiti, jijini Arusha, Hamisi Amani (17), kwa tuhuma za kumuua mwenzake wakati wakigombea soda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu, saa mbili usiku katika eneo la Kwa Morombo.
Kamanda Mkumbo alimtaja marehemu kuwa ni Novatus Tadei (26), mkazi wa Kwa Morombo na kwamba aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani upande wa kushoto.
“Marehemu na mtuhumiwa walikuwa wapishi kwenye kampuni inayojulikana kwa jina la ZZ Catering inayomilikiwa na Bashiri Ally.
“Siku ya tukio, marehemu pamoja na wafanyakazi wengine, akiwamo mtuhumiwa, baada ya kumaliza kazi waliyokuwa wanafanya, walipanda gari lenye namba za usajili T 375 CHH, aina ya Toyota Hiace wakirejea nyumbani.
“Wakiwa ndani ya gari hilo, mtuhumiwa Hamis aligundua kuwa soda aliyokuwa ameiweka ndani ya begi lake, haipo na kuanza kuhisi marehemu ndiye aliyeichukua.
“Kwa hiyo, ulizuka ugomvi baina yao na kuanza kutukanana matusi. Wakati ugomvi huo ukiendelea, mtuhumiwa alimkaba marehemu na kuchukua kisu wanachotumia kwenye shughuli zao za mapishi kilichokuwa ndani ya vyombo na kumchoma kifuani.
“Baada ya kuchomwa kisu, Tadei alianguka chini na jitihada za wafanyakazi wenzake waliokuwamo ndani ya gari hilo kuokoa maisha yake zilishindikana, kwani alifariki wakati anapelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu,” alisema Kamanda Mkumbo.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.