Vurugu za aina yake Shinyanga: Katika hali isiyokuwa ya kawaida wakazi kadhaa wa kijiji cha Welezo kata ya Tinde wilayani Shinyanga wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao huku wanne wakidaiwa kupoteza fahamu baada kushambuliwa kwa silaha za jadi ikiwemo fimbo na kundi la walinzi wa jadi sungusungu wapatao 800 waliofika kijijini hapo kwa madai ya kuchemsha jeshi la jadi ‘kusebya’ na kuondoa adhabu katika kijiji hicho kilichokuwa kimepigwa faini 'mchenya' shilingi 1,300,000/-.
Tukio hilo la aina yake limetokea Desemba 10, mwaka huu saa kati ya saa 3.30 na 4.00 asubuhi katika uwanja wa shule ya msingi Welezo iliyopo katika kijiji cha Welezo kata ya Tinde wilayani Shinyanga ambapo wakazi wa eneo hilo zaidi ya 400 walikuwa eneo hilo wakisubiri sherehe ya kuchemsha jeshi la jadi 'kusebya' huku wengine wakiendelea na hekaheka za kupika nyama baada ya ng'ombe watatu kuchinjwa.
Inaelezwa kuwa chanzo cha vurugu ni mwenyekiti wa kijiji Salum Shaban kudaiwa kula njama za kuwaalika walinzi wa jadi kutoka vijiji jirani kuja kuwadhalilisha na kuwacharaza viboko huku wakipewa adhabu za kupiga pushapu,kuinamisha vichwa chini ya ardhi bila kujali wanawake wenye ujauzito.
Wakizungumza jana Desemba 15 ,2016 katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro wanakijiji hao walisema vurugu hizo zilitokea baada ya kundi la sungusungu wanaodaiwa kuwa zaidi ya 800 kutoka vijiji jirani kufika kijijini hapo kwa lengo la kutatua mgogoro baina ya wanakijiji na viongozi wa jeshi la sungusungu na kuwatawaza upya sungusungu wa kijiji hicho 'kusebya'.
Wakifafanua kwa kina kuhusu kiini cha tukio hilo,wanakijiji hao walidai chanzo cha wao kuadhibiwa na kusababisha baadhi yao kupoteza fahamu na kujeruhiwa kwa vipigo vya fimbo na silaha zingine za jadi ni wanakijiji kuwashinikiza viongozi wao kuwasomea taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji cha Welezo.
Walibainisha kuwa viongozi wa sungusungu na kijiji walishindwa kutekeleza agizo la mkutano mkuu wa kijiji ulioagiza kugawanywa kwa mpunga gunia 160 ambao hukusanywa kutoka kwa watu wanaolipishwa adhabu “mchenya” baada ya kufanya makosa madogo madogo kijijini.
Walisema hivi karibuni waliwaagiza viongozi wao kuandaa mkutano wa kuwasomea taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji ikiwemo kupanga utaratibu wa jinsi watakavyogawa mpunga wa kijiji kwa wanakijiji ambapo viongozi wao walikiri kutekeleza agizo hilo.
Hata hivyo siku iliyopangwa viongozi hao akiwemo mwenyekiti na katibu wa sungusungu,mwenyekiti wa kijiji,afisa mtendaji wa kijiji hawakujitokeza katika mkutano na badala yake waliendesha vikao vya ndani wakishirikiana na viongozi wa sungusungu kitu ambacho wanakijiji hawakukiafiki na hivyo kuchukua hatua ya kuukataa uongozi wa sungusungu.
“Baada ya kubaini viongozi wetu wanatuzungusha na hawataki kutekeleza maazimio ya mkutano mkuu, wanakijiji tuliamua kuwavua madaraka viongozi wa sungusungu, hali ambayo wenzetu hawaikuafiki, na hivyo walikula njama na viongozi wa sungusungu wa kata na tarafa ili kutukomoa”,alisema Shija Pius.
“Tulipowavua madaraka, viongozi wa sungusungu wa kata na tarafa walishinikiza kijiji chetu kitengwe, na kweli tulitengwa na kijiji kizima kilipe shilingi 1,300,000/= ili kujikomboa na kuchemsha upya jeshi la sungusungu ‘Kutemya’",alisema Janeth Kulubone.
“Baada ya muda tukaombwa tuchangie shilingi 5,000/- kila kaya ili tuweze kuondolewa adhabu tukanunua ng’ombe sita na mbuzi kadhaa kwa ajili ya kazi hiyo,lakini pia vijana walichanga shilingi 1,000/- ili kutawazwa kuwa walinzi wa sungusungu kwa kile walichokiita kuchemsha upya jeshi la jadi 'kusebya'”, alieleza John Kitumbo.
Waliendelea kueleza kuwa baada ya kukamilisha mahitaji yote kwa ajili ya shughuli za kujikomboa na kuchemsha jeshi, mkutano uliitishwa na viongozi wa jadi kutoka ngazi ya kata, tarafa na wilaya na ndiyo waliohusika kusimamia shughuli yote.
Walisema siku ya kufanyika kwa shughuli iliyokuwa imekusudiwa,walishangaa kuona viongozi wao wakiibuka na agenda tofauti na iliyokuwa imepangwa kufanyika ambapo kikao hicho kilichoongozwa na mwenyekiti wa sungusungu wilaya ya Shinyanga Kulwa Masanja kiligeuka cha kuwataja watu wanaojihusisha na uhalifu kama vile wezi na wakata mapanga vikongwe.
“Tulishangaa kuona mambo yamebadilika, tukiwa tunajiandaa kutawazwa upya,tukiwa tumezungukwa na sungusungu wa vijiji jirani, ghafla kamanda wa sungusungu wa wilaya, Kulwa Masanja alitoa agizo la wanaume tuvue mashati,wanawake wavue viremba hata kama ni muislm na kukaa chini,kushika vichwa kisogoni na kisha kuinamisha uso ardhini”,alieleza Nkanda Hussein.
“Tulitii agizo ambapo hata akina mama wajawazito waliinamishwa chini pamoja na kwamba walilalamika kuhusu hali zao,Kamanda alianza kuita majina ya watu na kuwataka wajitokeze mbele ya mkutano ambapo waliambiwa wao ni wahalifu na wanatakiwa kuchapwa viboko na kujikomboa kwa shilingi 200,000/- kila mmoja”,alieleza Hussein.
“Hii haikuwa agenda yetu, baadhi ya watu waliokuwa wakitajwa na kuelezwa kuwa ni wahalifu walishambuliwa kwa viboko na kutakiwa walipe shilingi 200,000 ili wajikomboke, mmoja alilipa lakini mtu wa nne aligoma, akapigwa fimbo,hapo ndipo vurugu zilipoanzia kwani wananchi hawakukubali kuchapwa mpaka askari polisi walipofika kutuliza vurugu,” alieleza Anna Kulwa.
Wanakijiji hao walisema baada ya mtuhumiwa wanne kati ya 36, kugoma kupigwa ndipo vurugu zilipoanza na kamanda wa sungusungu wilaya alitoa amri ya wanakijiji wote kucharazwa viboko na wengi walichapwa huku baadhi wakipoteza fahamu na kukimbizwa kituo cha afya cha Tinde kupatiwa matibabu.
Kufuatia tukio hilo wanakijiji hao wamekataa mwenyekiti wao wa serikali ya kijiji mbele ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro aliyefika kijijini hapo kutafuta suluhu ya mgogoro uliojitokeza.
Kutokana na hali hiyo mkuu wa wilaya ya Shinyanga amelazimika kumsimamisha uongozi mwenyekiti wa kijiji cha Welezo, Salumu Shabani na Janeth Kulubone kukaimu nafasi hiyo huku akiagiza kufanyika kwa uchunguzi dhidi ya tuhuma zote anazotuhumiwa.
“Nimesikiliza maelezo yenu kwa kina,nimebaini chanzo cha vurugu hizi ni viongozi wenu kukiuka maadili ya uongozi,naunga mkono azimio lenu la kumkataa mwenyekiti wa serikali ya kijiji, asimame na uchunguzi wa tuhuma zake ufanyike mara moja, na hapa hapa chagueni mwenyekiti wa muda, na kamati mpya ya sungusungu” ,alielieza Matiro.
“Wananchi wamenyanyaswa,wameumizwa bila sababu,chanzo viongozi wasiotaka kusikiliza wananchi wao,sasa tunawaondoa wote,hakuna mwenye mamlaka ya kuonea mtu,haiwezekani watu wachache waharibu amani yetu,sungusungu kazi yenu siyo kunyanyasa wananchi hii iwe mara ya mwisho sitasita kumchukulia hatua kali yeyote atakayeendeleza vurugu kijijini hapa",aliongeza.
Naye Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Shinyanga Azza Hilal (CCM) aliyehudhuria mkutano huo alieleza kusikitishwa na tukio hilo huku akiwataka viongozi kuwa na utamaduni wa kufanya mikutano ya hadhara ikiwemo kusoma taarifa za mapato na matumizi.
Kwa upande wake kamanda wa Jeshi la Sungusungu wilaya ya Shinyanga Kulwa Masanja alikiri kutoa agizo hilo la wanakijiji kuadhibiwa akidai kutekeleza kanuni na taratibu za sungusungu huku akidai kuwa kitendo hicho kilitokana na kulaghaiwa na baadhi ya watu wenye nia mbaya.
“Naombeni radhi wanakijiji,nimejifunza mambo mengi kwenye tukio hili,nimebaini wengine tulichomekwa tu,natambua viongozi wapya waliopatikana leo nitawapa ushirikiano naamini watanisaidi kiutendaji japo kuna mapungufu”,alisema Masanja.
Mwenyekiti wa kijiji cha Welezo aliyeondolewa katika nafasi hiyo Salum Shaban alisema chanzo cha mgogoro katika kijiji hicho ni uozo wa viongozi wa sungusungu ambao hawakutaka kusikiliza wananchi wanataka nini na kutosikiliza ushauri wake.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kudai kuwa tayari kuna kesi ya shambulio la kudhuru mwili imefunguliwa na waathirika wanne wa tukio hilo.
Muliro alisema jeshi la polisi linaendelea kuwahoji watu mbalimbali kutoka katika kijiji hicho wakiwemo viongozi na upelelezi utakapokamilika kesi itapelekwa mahakamani huku akisisitiza kuwa hakuna mwananchi yeyote atakayeonewa.
Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde ametusogezea picha...tazama hapa chini
Hapa ni katika kijiji cha Welezo kata ya Nsalala wilaya ya Shinyanga ambapo Desemba 10,2016 kulitokea vurugu
Bwana John Kitumbo akionesha majeraha aliyoyapata baada ya kuchapwa viboko na walinzi wa jeshi la jadi sungusungu katika kijiji cha Welezo kata ya Nsalala wilaya ya Shinyanga
Mkazi wa kijiji cha Welezo akionesha majeraha
Mkazi wa kijiji cha Welezo akiwa ameumia kichwani na kwenye sikio
Kulia ni bwana Nkanda Hussein akionesha majeraha mgongoni
Mkazi wa Kijiji cha Welezo John Kitumbo akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake
Mkazi wa kijiji cha Welezo akiwa na majeraha kwenye paji la uso
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika shule ya msingi Welezo iliyopo katika kijiji cha Welezo kata ya Nsalala wilaya ya Shinyanga
Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga waliokuwa wameambatana na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na viongozi wa kijiji cha Welezo wakiwa katika mkutano wa hadhara
Wanakijiji cha Welezo wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wakazi wa kijiji cha Welezo
Wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara
Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga wakiwa katika mkutano.Wa pili kutoka kushoto ni mbunge wa viti maalum mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Azza Hilal (CCM) akifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika mkutano huo uliotishwa na mkuu wa wilaya
Aliyesimama ni mwenyekiti wa kijiji cha Welezo bwana Salum Shaban akijibu hoja za wananchi kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo
Mkazi wa kijiji cha Welezo akieleza kero yake kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga
Wananchi wakiwa katika mkutano huku askari wa jeshi la polisi waliokuwa na silaha za moto wakiwa wamezingira mkutano huo ambao mwanzo ulitawaliwa na kelele za hapa na pale mpaka kufikia hatua ya wananchi kutaka kuwapiga viongozi wote waliosababisha wanakijiji wachapwe viboko
Katikati ni mwenyekiti wa kijiji cha Welezo bwana Salum Shaban akijieleza kwenye mkutano
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiongea baada ya mwenyekiti mpya wa kijiji cha Welezo Janeth Kulubone (kulia) kuteuliwa kukaimu nafasi ya mwenyekiti wa awali Salum Shaban anayedaiwa kuwa chanzo cha vurugu
Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Welezo Janeth Kulubone aliyeteuliwa kushika nafasi ya mwenyekiti wa awali Salum Shaban anayedaiwa kuwa chanzo cha vurugu
Kamanda wa Jeshi la Sungusungu wilaya ya Shinyanga Kulwa Masanja aliyeongoza zoezi la wanakijiji kucharazwa viboko akiomba radhi wakazi wa kijiji cha Welezo kwa yale yaliyotokea
Kamanda wa Jeshi la Sungusungu wilaya ya Shinyanga Kulwa Masanja alisema amechomekwa tu kwenye sakata hilo na anachofanya yeye ni kufuata kanuni na taratibu za jeshi hilo
Mbunge wa viti Maalum mheshimiwa Azza Hilal akizungumza na waandishi wa habari eneo la mkutano ambapo alilaani kitendo cha wananchi kuumizwa huku akiwataka viongozi kujenga utamaduni wa kusikiliza wananchi na kuwasomea mapato na matumizi badala ya kuwapuuza kama ilivyofanyika kwa viongozi wa kijiji cha Welezo
Mwandishi wa gazeti la Majira Suleiman Abeid akifanya mahojiano na kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Welezo Janeth Kulubone baada ya mkuu wa wilaya Josephine Matiro kufunga mkutano wa hadhara
Mmoja kati ya akina mama wajawazito waliolazimishwa kuinamisha vichwa chini wakiwa wamekaa baada ya kupewa agizo la kuvua viremba licha ya kujitetea
Mwandishi wa habari gazeti la Nipashe na radio Faraja Marco Maduhu akifanya mahojiano na Anna Kulwa mmoja wa akina mama waliochapwa viboko siku ya tukio mpaka pale polisi walipofika kutuliza vurugu
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Welezo waliochapwa viboko siku ya tukio
Waandishi wa habari wakifanya mahojiano na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Welezo waliochapwa viboko
Wakazi wa kijiji cha Welezo wakieleza namna walivyozingirwa na kuchapwa viboko na walinzi wa jeshi la jadi Sungusungu kutoka kijiji jirani.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog