TAARIFA KWA UMMA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MFUMO WA JAZIA DAWA,VIFAA TIBA NA VITENDANISHI MKOA WA SHINYANGA


Katibu tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Mzabuni Teule “Prime Vendor System” yaani Mfumo Jazia Dawa,Vifaa Tiba na Vitendanishi mkoa wa Shinyanga Desemba 13,2016 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog

TAARIFA KWA UMMA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI, SHINYANGA, 13 DISEMBA 2016
Uzinduzi Wa Mfumo wa Jazia Dawa,Vifaa Tiba Na Vitendanishi Katika Mkoa Wa Shinyanga

Mfumo Jazia Dawa,Vifaa Tiba Na Vitendanishi kwa kutumia Mzabuni mmoja (Prime Vendor) ni moja ya mafanikio ya ushirikiano wa sekta binafsi na serikali ukiwa na lengo la kujazia upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya uma vya kutolea huduma za afya pale ambapo bohari kuu ya dawa inashindwa kukidhi mahitaji ya vituo vya kutolea huduma. Manunuzi yanafanywa kutoka kwa mzabuni mmoja tuu katika mkoa.

Upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ni moja ya misingi ya uendeshaji mfumo wa huduma za afya. 

Hivyo basi dawa na vifaa tiba vikipatikana katika vituo vya kutolea huduma unawapa motisha watoa huduma katika maeneo yao ya kazi na husababisha jamii kuuamini mfumo wa afya wa umma, na kutoa fursa kwa wagonjwa kupata huduma bora. 

Upatikanaji wa dawa unachukuliwa ni kama huduma nzuri za afya, licha ya kwamba kuna huduma zingine muhimu kama lugha nzuri upatikanaji wa huduma kwa gharama nafuu na kwa wakati.

 Ila kwa dhana ya kuwa na huduma bora za afya nchini, upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu utachangia wingi wa watu kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).


Vituo vya serikali vya mkoa wa Shinyanga vinapokea dawa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka Bohari Kuu ya dawa. Taasisi hii ya serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha inakuwa na dawa zinazokidhi mahitaji ya vituo licha ya mfumo wake wa uagizaji na usambazaji  kuwa na changamoto za hapa na pale hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya dawa ambayo yanahitajika. 

Hivyo Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na mradi wa Tuimarishe Afya (HPSS Project) unaofadhiliwa na Serikali ya Uswizi kupitia Shirika lake la Maendeleo na Ushirikiano (SDC) umeamua kutafuta njia ya kuziba pengo linalosababishwa na ukosefu wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi toka Bohari Kuu ya Dawa kwa kutumia mfumo wa manunuzi nje ya Bohari Kuu ya Dawa unaohusisha mzabuni mmoja tuu kwa Mkoa mzima.

Halmashauri zina fedha za kununua dawa ila hukabiliwa na  mlolongo mrefu wa manunuzi unaohusisha wazabuni tofauti tofauti wasiokua na uwezo wa kukidhi mahitaji ya vituo ambao pia unaongeza gharama ya dawa.

Hivyo kwa mfumo huu unaozinduliwa leo, mahitaji ya kununua dawa kutoka vituoni kwa kila halmashauri yatatumwa kwa Mzabuni mmoja aliyeteuliwa kwa kushirikisha halmashauri zote ndani ya mkoa. Dawa hizi zitanunuliwa kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya mapato kama CHF, NHIF, Papo kwa Papo na Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health basket funds).

Mchakato wa kumpata Mzabuni umefuata taratibu zote za manunuzi ya uma. Mkoa una furaha kushuhudia uzinduzi wa mfumo huu mkoani Shinyanga.

 Mzabuni aliyeshinda katika machakato huu ni Bahari Pharmacy Ltd na anaingia mkataba na Mkoa wa Shinyanga ili kuhudumia halamshauri zote leo.

Huu utakuwa mwanzo mzuri wa utekelezaji wa mfumo huu na tukiamini dawa zitapatikana na kujazia ule upungufu wa dawa, kwa kushirikiana na wadau wetu Bohari Kuu ya dawa kama msambazaji mkuu wa dawa katika vituo vyetu vya serikali. 

Mkoa pia utashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya chakula na dawa, baraza la wafamasia, na kitengo cha wafamasia kilichopo Wizara ya Afya katika kusimamia utekelezaji wa mfumo huu.

Kusaini tu mkataba kati ya Mkoa na Mzabuni sio mwisho, bali kuna  miongozo ambayo ni rafiki kwa vituo vya kutolea huduma na halmashauri imeandaliwa ili kuwezesha utekelezaji fanisi wa mfumo huu ili kuleta matokeo yalikusudiwa.

Kila mhusika atapaswa kufuata miongozo iliyopo katika kuagiza dawa na vifaa tiba kwa mfumo huu.

Katika hatua za kupunguza ukosefu wa dawa, matibabu yanayozingatia miongozo ya kitabibu ni muhimu kufuatwa hasa ugawaji wa dozi stahiki kwa mgonjwa lazima uzingatiwe. 

Pia usimamizi wa dawa utaimarishwa ili kuhakikisha dawa zinakuwepo vituoni muda wote.

Uzinduzi wa mfumo huu katika mkoa wa Shinyanga umefungua mwanga mpya katika serikali na jamii kwa ujumla. Ushiriki madhubuti wa viongozi  wa mkoa na wilaya ndio nguzo  katika kuboresha mfumo huu  wa manunuzi wa dawa. 

Ni matumaini yangu mfumo huu utasaidia kupunguza ukosefu na kuongeza upatikanaji wa dawa halmashauri na vituo vyote vya mkoa wa Shinyanga. Mfumo huu unatoa nafasi kwa mijadala mbalimbali ya kisera na hata kuja kutumika nchi nzima.

Albert G Msovela
Katibu Tawala Mkoa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post