MBUNGE wa Kilombero, Peter Lijualikali kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amemueleza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba , kuwa hayupo tayari kutoa fedha za Mfuko wa Jimbo kuchangia kazi za maendeleo ya Polisi jimboni humo.
Amesema hawezi kufanya hivyo, kwa sababu Polisi wa jimbo lake hawamtii na wanashindwa kumpigia saluti.
Lijualikali aliweka bayana msimamo huo wakati akizungumzia changamoto mbalimbali kwa waziri huyo, kabla ya kupanda jukwaani kuwahutubia mamia ya wananchi waliojitokeza mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Ifakara.
Mbunge huyo alisema. “ Huu ni ugeni wa kwanza wa hadhi ya kitaifa kuja kwenye jimbo hili kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara… sasa tufanye kazi ya kujenga taifa letu badala ya kuendeleza siasa”.
Mbunge huyo alimuomba waziri huyo wa mambo ya ndani, atoe majawabu mbele ya mkutano huo ikiwa ni pamoja na suala la bodaboda kufukuzana na polisi na dawa za kulevya. Pia, Lijualikali alihoji kwa nini polisi wa Ifakara katika Jimbo la Kilombero, hawampigii saluti wakati yenye ni mbunge .
“Hii ni hoja ya bungeni… mbunge kupigiwa saluti, lakini Polisi wa Ifakara hawanipigii saluti,” alisema Lijualikali, akimuarifu waziri huyo mwenye dhamana na jeshi la polisi.
Hivyo, alisema hawezi kuhamasisha uchagiaji wa ujenzi wa vituo vya polisi au kutoa fedha za Mfuko wa Jimbo kwenda kusaidia juhudi za ujenzi wa vituo hivyo.
Mbunge huyo alimuomba waziri kuwa kituo cha sasa cha polisi, kihamishwe kutokana kilipo ni eneo linalokumbwa na mafuriko nyakati za masika hivyo kutofikika kirahisi. Kwa upande wake, Mwigulu alisema hoja hiyo ni ya kiutawala na kiutendaji zaidi na pia ni ya kuangalia historia ya wabunge waliomtangulia.
Chanzo-Habarileo