Gari la polisi likimwaga maji ya kuwasha
Askari wakiwa nyumbani kwa marehemu wakipiga mabomu na kusambaratisha waombolezaji
***
Jeshi la polisi mkoani Shinyanga, limelazimika kuwa piga mabomu ya machozi waendesha bodaboda, kwa kitendo cha kuundamana kupinga kifo cha mwenzao ,kilichodaiwa kusababishwa na askari polisi PC Edmund,Mwandishi wetu Kadama Malunde anaripoti.
Tukio hilo la kupiga mabomu limetokea leo Jumatano Juni 7,2017 majira ya saa moja asubuhi hadi saa sita mchana ambapo askari polisi walikuwa wakipimana nguvu na boda boda ,hao kwa kutupiana mawe na mabomu hali ambayo imesababisha shughuli za kijamii mjini Shinyanga kusimama.
Tukio la polisi kupiga mabomu linakuja siku moja baada waendesha bodaboda hao kulazimika kuwapiga mawe askari polisi kwa madai ya kusababisha kifo cha mwezao Joel Gabriel Mamla (26) mkazi wa Ibinzamata mjini hapa baada ya kupasuka kichwa kwa kuanguka kwenye pikipiki aliyokuwa amembeba na askari polisi aliyemkamata kwa makosa ya usalama barabarani .
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga ACP Muliro Jumanne Murilo, alisema maandamano hayo siyo halali na wameamua kuzui maandamano hayo kwa sababu yanahatarisha hali ya usalama,walitakiwa kutii sheria bila shuruti na kufuata taratibu za kudai kuonewa, na siyo kutishia kuharibu amani.
Hata hivyo jeshi hilo halikuishia kupiga mabomu bali lilikwenda hadi nyumbani kwenye msiba Ibinzamata alipokuwa akiishi marehemu na kuwatawanya kwa mabomu waombolezaji kwa kuwakamata waendesha bodaboda na pikipiki zao hali iliyozua taharuki zaidi.
Mmoja wa bodaboda Simoni Bundala alisema wameamua kuandamana kwa madai ya kufikisha ujumbe serikalini kuwa jeshi la polisi mkoani Shinyanga linafanya kazi kwa kuwaonea.
Alisema haiwezekani askari aliyevaa kirai akamate pikipiki yenye makosa bila hata ya kuonyesha kitambulisho jambo ambalo ni hatari kwa kuhofia unyang'anyi wa pikipiki.
Tukio la kupoteza maisha kwa bodaboda huyo limetokea Juni 6,2017 majira ya saa 6.45 mchana katika eneo la Kona ya Buhangija barabara kuu ya kutoka Mwanza kwenda Tabora.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema walimuona mwendesha bodaboda akiwa mwendo kasi huku pikipiki yake ikiyumba,huku akivutana mikono na kupigana viwiko na abiria aliyekuwa amempakiza na walipokaribia eneo hilo la ajali ndipo akakabwa shingo na abiria wake anayedaiwa kuwa ni polisi na hatimaye kuiachia pikipiki na kuanguka chini.
"Wamekuja wanavutana kwenye pikipiki,walikuwa wanakabana juu ya pikipiki,walipofika eneo ambako yanatokea mabasi,askari akawa anaburuza miguu chini,mara akamkaba mwendesha bodaboda ili pikipiki isimame,askari akamkaba roba dereva,ikabidi aachie usukani,alivyotaka kurudi akakuta pikipiki imeshahama barabarani ndiyo akakutana na alama ya barabarani akaibamiza,akaangukia jiwe”,waliongeza.
Mmoja wa mashuhuda hao ,Yahaya Kisewene alisema walipoanguka chini ndipo bodaboda huyo akapiga kichwa kwenye jiwe na kuanza kuvuja damu puani na maskioni hali iliyosababisha kifo chake papo hapo, na baada ya hapo ndipo wananchi wakaanza kumshushia kichapo mtu ambaye alikuwa amempakiza.
“Wakati kichapo kikiendelea ndipo mtu huyo alipojitambulisha kuwa ni polisi, na wananchi hawakuweza kumfahamu kwa sababu alikuwa amevaa kiraia na kuhisi labda ni jambazi alikuwa akitaka kupora pikipiki, lakini hawakujali na kuendelea kumpiga hadi alipowaponyoka na kukimbilia kwenye mji jirani ndipo akanusurika naye kifo”,alieleza Shabani
Akielezea tukio hilo kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Muliro Jumanne Murilo alisema askari mwenye cheo cha CPL wa kikosi cha usalama barabarani akiwa na askari wenzake wawili wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kisheria ya ukamataji wa kawaida wa waendesha pikipiki zisizotii sheria za barabarani,waliikamata pikipiki na MC 700 AWH SANLG iliyokuwa ikiendeshwa na Joel Gabriel Mamla kwa kosa la kutovaa helmet.
Mtuhumiwa huyo alipoambiwa kosa lake na kuamriwa kwenda kituo cha polisi kwa hatua zaidi za kisheria na
alidai yeye ndiye atakayeendesha pikipiki yake kuelekea kituo cha polisi na hivyo akampakia kwa nyuma askari polisi aliyekuwa amevaa kiraia.
Alisema badala ya kwenda kituoni dereva huyo wa bodaboda alibadilisha uelekeo wa barabara na kuanza kuendesha kwa kasi kubwa kuelekea barabara ya Tabora- Tinde huku akimweleza askari yule kuwa watakufa wote.
Aliongeza kuwa alipofika eneo la Buhangija aliielekeza pikipiki kwenye nguzo ya alama ya usalama wa barabarani na akafanikiwa kuitumbukiza kwenye shimo kwa maksudi ambapo wote walianguka na hivyo kupata majeraha na wakakimbizwa hospitali ya mkoa kwa matibabu.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Shinyanga Dkt Herbert Masigati alikiri kupokea mwili wa marehemu hospitalini hapo majira ya saa 7 mchana na kuuhifadhi kwenye chumba cha kutunzia maiti, huku askari ambaye alikuwa na marehemu naye wakimpatia matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Social Plugin