Mzee anayefahamika kwa jina la Joseph Sahani (60) mkazi wa kijiji cha Nzonza Kata ya Salawe wilaya ya Shinyanga amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu ya kuongezewa nguvu za kiume kwa mganga wa kienyeji kwa kujazwa dawa kwenye tundu la uume kwa kutumia pampu ya baiskeli.
Tukio hilo limetokea Oktoba Mosi mwaka huu majira ya saa 10 jioni katika kijiji cha Nzonza kata ya Salawe ambapo mzee huyo alipokuwa akipatiwa matibabu ya kuongeza nguvu za kiume kwa mganga wa kienyeji aitwae Robert Nkoma(58).
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Simon Haule alisema chanzo cha tukio ni marehemu kuwa na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume na kwenda kwa mganga huyo ili atibiwe ndipo mganga akatumia njia ya kumuingiza unga unaosadikiwa kuwa ni dawa ya kienyeji kwenye tundu la uume kwa kutumia pampu ya baiskeli.
“Mganga alianza kuingiza dawa hiyo kwenye tundu la uume akitumia pampu ya baiskeli akawa anapampu kama anajaza upepo na kusababisha marehemu kuishiwa nguvu na kutoka damu nyingi kwenye uume na kusababisha kifo chake”,alieleza Kamanda Haule.
Alisema tayari jeshi la polisi linamshikilia mtuhumiwa kwa hatua zaidi za kisheria.
“Natoa wito kwa wananchi wenye matatizo ya kiafya kuacha tabia ya kuendekeza kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kutafuta tiba, bali waende kwenye vituo vya afya au hospitali kufanyiwa uangalizi na kupewa matibabu sahihi”,alisema Kamanda Haule.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin