'NABII TITO' ANAYEFANYIA IBADA ZAKE BAA AKOMAA KUMUOA WEMA SEPETU


Mkazi mmoja wa Dodoma anayejitangaza kama nabii, Tito Machija amesema watu wasimuone kuwa hana akili kutokana na mahubiri yake ambayo yanatofautiana kwa kiasi kikubwa na imani za waumini wa dini nyingine, hasa Wakristo.


Machija, ambaye anajulikana kama ‘Nabii Tito’ anahamasisha kuoa mke zaidi ya mmoja, ikiwa ni pamoja na kutembea na wafanyakazi wa ndani; anatumia pombe kunasa waumini na anadai hataki nyimbo za injili kwenye ‘ibada’ zake, ambazo nyingi hufanyikia baa.


‘Nabii’ huyo anaonekana kwenye mitandao ya kijamii akiwa amevalia kanzu nyeupe yenye misalaba miwili, chupa ya bia na kitabu kitakatifu aina ya Biblia.


“Nawashangaa wanaoniona mimi sina akili, niko timamu kabisa na ninaelewa ninachokifanya,” alisema.


“Narudia tena kusisitiza kuwa walevi ndio watakaoingia ‘mbinguni’ na mafundisho ninayoyatoa ni sahihi,”


Tito amekuwa akionekana kwenye mitandao ya kijamii, hususani kwenye video fupifupi za Instagram, akiwa amevalia mavazi kama ya kichungaji na kucheza muziki huku akinywa bia na akiwa ameshika biblia.


‘Nabii’ huyo, mwenye wake watano na watoto 12, amedai kuwa kwa sasa hitaji lake kubwa ni kumuoa mwigizaji Wema Sepetu ili aungane naye katika huduma zake.


“Wema ni msichana mzuri wa sura na umbo nataka nimuoe awe sehemu ya kanisa langu na nina imani watu wengi wataongezeka kwenye ibada ili kuja kumuona yeye na wake zangu hawana tatizo na hilo hata mmoja wao ananisaidia kumshawishi ili tuungane naye,” alisema Tito.


Tito anakiri kuwa ‘kanisa’ lake halijasajiliwa ila anadai kwamba anapata ufadhili kutoka kwa walevi mbalimbali.


Tito amedai kuwa ‘kanisa’ lake lipo karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma na mara nyingi ibada zake huwa anazifanya kwenye baa na ana wafuasi wengi kiasi cha kutojua idadi yao.


Amesema kabla ya ibada kufanyika kwenye baa husika, huanza kwa kupeleka vipeperushi kwa mmiliki ili kuwapa taarifa waumini wake siku hasa ya ibada kufanyika katika baa hiyo.


“Siku ya ibada ikifika naenda pale nikiwa na bia zangu za (anaitaja aina ya bia) ambazo nimeshaziombea. Zina ‘upako’. Kila anayetaka kuingia kwenye ibada analipa kiingilio cha Sh12,500. Ukilipa pesa hiyo unapata bia zako tano ndiyo huduma inaendelea usipotoa unafukuzwa,” alisema.


Tito anajinasibu kuwa ana waumini wengi ambao hujitokeza kusikiliza mafundisho yake ambayo kwa kiasi kikubwa yanahamasisha ulevi na mapenzi kwa wasichana wa kazi wa majumbani.


Amesema kwenye huduma zake nyimbo za injili hazina nafasi kwa kuwa huwaburudisha waumini wake kwa nyimbo za kisasa.


“Mtu akishaweza safari zake kichwani ukimuwekea bongofleva anacheza na kufurahi huku ibada inaendelea,” alisema.


Nabii huyo amedai kuwa hakuna anachokizungumza kutoka kichwani mwake bali anasimamia mistari ya vitabu vitakatifu.


“Wapo wengi wanaopinga huduma zangu ila nawaambia sijakurupuka nafanya kitu ambacho kipo na wala sioni kama ninakosea,” alisema.


Kwanini ‘ibada’ kwenye baa
Tito amedai kuwa anaingia makubaliano na wenye baa kwa kuwa ndiyo sehemu ambayo walevi hukutana na kwake ni mahali sahihi pa kutoa huduma.


“Pale nakwenda na bia zangu kadhaa kwa ajili ya waumini watakaoingia kwenye ‘ibada’. Zikiisha naondoka zangu, nawaacha wanaendelea kununua za baa hapo ndipo mwenye baa anaponufaika,” alisema.


Watu wengi wamekuwa wakilaumu mafundisho ya Tito kuwa yanapotosha na wameiomba Serikali kuchukua hatua.


Credit: Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post