Rufaa
ya kupinga hukumu ya kifungo cha miezi mitano jela iliyotolewa kwa
mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga imewasilishwa Mahakama Kuu
Kanda ya Mbeya.
Akizungumza
leo Machi 1, 2018 mmoja wa mawakili wa Sugu, Faraji Mangula amesema
tayari maombi ya rufaa yao yamepokewa leo mchana na kupewa kumbukumbu
namba 29/2018.
“Tayari
rufaa yetu imeshapokewa Mahakama Kuu (Mbeya) na tunachosubiri ni
kupangiwa tarehe ya kuanza kusikiliza tu, ila tunachoshukuru watu wa
Mahakama hii wapo vizuri kushughulikia suala hili,” amesema Mangula.
Mbali
na kukata rufaa hiyo, lakini pia mawakili hao wanakusudia kuomba
dhamana kwa wateja wao ili waweze kuwa nje katika kipindi ambacho
wanakuwa wanasikiliza rufaa yao.
Sugu na Masonga walihukumiwa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Wawili
hao walitoa kauli hiyo Desemba 30 mwaka jana katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.