Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack ametoa onyo kali na kuwataka wananchi kuachana na maandamano yanayodaiwa kuwa yatafanyika tarehe 26 Aprili mwaka huu siku ya sikukuu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuwataka wanaotaka kuandamana waage familia zao na ikiwezekana wampigie simu mkuu wa magereza awaandalie nafasi gerezani.
Telack ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 23,2018 wakati wa uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika kimkoa katika viwanja vya Zimamoto mjini Shinyanga.
Alisema wapo watu wanapanga kuandamana hivyo yeye kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kazi yake kubwa na muhimu ni kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na kazi hiyo anaifanya kwa weledi mkubwa akishirikiana na kamati ya ulinzi na usalama.
"Tunapigania amani ya nchi kadri inavyowezekana..Nataka niwathibitishie Wana Shinyanga kwamba mko salama,nitumie nafasi hii kuwaambia wale wote ambao wanataka kuandamana kesho kutwa kwamba wakiamua kuandamana wafanye mambo mawili, moja waage familia zao kwa sababu watachelewa kurudi nyumbani kwa kuwa lazima tuwakamate na lazima tuwaweke mahali tuwahoji na muda wa kuhoji hatujui ni muda kiasi gani ndiyo maana nasema waage nyumbani kwao,...kama ni vijana waage familia zao kama ni baba aage mke wake na familia yake kama ni mama aage watoto na mme wake",alisema Telack
"La pili ikiwezekana wampigie simu kamanda wa magereza awaandalie mahali pa kukaa kwa sababu nikiwakamata lazima niwapeleke magereza ili tuwachukue mmoja mmoja kuwahoji ili tujue walikuwa na nia gani inawezekana walivuta bangi tu asubuhi,bangi ikamtuma aingia barabarani,lazima tujue hilo".
"Kama kuna mtu popote anajiandaa kuandamana sisi tunamsubiri,nendeni shambani mkavune mpunga, twende tukafanye kazi zetu,twende minadani tukafanye biashara ,tuachane na maandamano acheni kuandamana na kuhamasishwa na watu waliopo ulaya".
"Wale ambao hawatasikia wakaingia barabarani kuandamana,mimi kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa nawaambia nawasubiri,lakini nawatahadhalisha tu ili tusije kulaumiana",aliongeza Telack.
Mkuu huyo wa mkoa alisema wananchi mkoani Shinyanga wataitumia siku ya Aprili 26,2018 kufanya usafi wa mazingira.
Mkuu huyo wa mkoa alisema wananchi mkoani Shinyanga wataitumia siku ya Aprili 26,2018 kufanya usafi wa mazingira.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin