MWELEKEO wa upelelezi wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow umebadilika na sasa tukio hilo linahusishwa na kisasi cha mapenzi na tayari mtu mmoja anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi Mwalimu Dorothy Moses kutiwa mbaroni na polisi.Awali, ilidaiwa kwamba Kamanda Barlow ambaye aliuawa kwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi muda mfupi baada ya kumfikisha mwalimu huyo nyumbani kwake, alivamiwa na majambazi.
Mkurugenzi
wa Makosa ya Jinai, DCI, Robert Manumba alithibitisha jana kukamatwa
kwa mtu huyo (jina tulihifadhi) akisema: “Ni kweli mtu mmoja
amekamatwa, lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia kwa kina kuhusu suala
hilo kwa sababu bado tunamhoji na tunaendelea na uchunguzi.
Tutakapokamilisha, tutatoa taarifa.”
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola pia alithibitisha
kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo. Hata hivyo, alisema amesikia habari hizo
kwa kuwa yuko safarini kwenda mkoani Kilimanjaro kwenye mazishi ya
kamanda huyo... “Hayo nimesikia, lakini kwa sasa sipo Mwanza hivyo
siwezi kuzungumzia lolote.”
Habari
za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinaeleza kwamba upelelezi
wa mauaji hayo umefanikiwa kwa hatua kubwa na kwamba mtu huyo
alikamatwa Dar es Salaam baada ya kuwekewa mtego na makachero waliopo
katika timu ya uchunguzi na alisafirishwa hadi Mwanza ambako
anashikiliwa na jeshi hilo.
Ilielezwa kuwa mtu huyo alikamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa za siri za kiitelejensia kutoka kwa watu mbalimbali.
“Kuna
hali imefunguka na imesaidia sana. Inaonyesha kwamba Dorothy alikuwa
na uhusiano na mtu huyu ambaye alikuwa akifika nyumbani kwake, kama
mumewe na watu wanajua jambo hili,” alieleza mmoja wa askari polisi
ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Alisema
kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba uamuzi wa mwalimu huyo
kusitisha uhusiano wa mapenzi na mtu huyo huenda ndicho chanzo cha
mauaji hayo lengo likiwa ni kumshawishi Dorothy kurejesha uhusiano.
“Mimi
natambua kwamba huyu jamaa na Dorothy walikuwa na uhusiano na
inajulikana mjini kuwa hata mke wa mtuhumiwa anatambua jambo hilo
kwani walishagombana siku moja mjini na hata katika msiba nyumbani kwao
na mtuhumiwa,” alisema mama mmoja (jina tunalo), aliyejitambulisha
kama mmoja wa marafiki wa karibu wa Dorothy.
Mwanafunzi
wa Shule ya Sekondari Kitangiri (jina tunalo), anasema amekuwa
akimfahamu mtuhumiwa aliyekamatwa kama baba mwenye nyumba hiyo na kila
mara amekuwa akimkuta hapo nyumbani wakati wa kujisomea na wanafunzi
wenzake.
“Mimi ninamfahamu kama baba wa rafiki yangu na nimewahi kumkuta wakati wa kujisomea hapo nyumbani na watoto wa nyumba hiyo.”
Dorothy
ambaye ametajwa kuwa mjane, ni Mwalimu katika Shule ya Msingi
Nyamagana na tangu kufariki kwa mumewe Ofisa wa zamani wa TRA, Modest
Lyimo mwaka 1997.
“Watu
wote wanajua kwamba mtuhumiwa alikuwa akitembea na huyo mwalimu,
wameonekana mara nyingi wakiwa muziki,” alieleza mmoja wa ndugu wa
karibu wa mke wa mtuhumiwa.
Hili
ni tukio la tatu mkoani Mwanza kutokea kwa ofisa wa polisi kuuawa.
Katika tukio la awali lililotokea mwaka 1987, askari aliyetambulika kwa
jina la Inspekta Gamba aliuawa kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa
ni majambazi eneo la Nyakato na katika tukio la pili mwaka 1997,
aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Kati ASP Mahende aliuawa kwa kupigwa risasi
eneo la Bugando saa nne usiku alipokuwa akifuatilia majambazi
waliokuwa wakijitayarisha kuvamia.
Dar wamuaga Kamanda Barlow
Makamu
wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliongoza waombolezaji waliofika
kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Barlow nyumbani kwake,
Ukonga Dar es Salaam jana.
Mwili
wa Kamanda Barlow ambao unasafirishwa leo kwenda mkoani Kilimanjaro
kwa mazishi, uliwasili nyumbani kwake saa 6.45 kabla ya kupelekwa
katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Ukonga kwa ajili ya ibada na
kutoa heshima za mwisho.
Akitoa
salamu za Serikali, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira
Silima alisema kifo cha Kamanda Barlow ni pengo kwa taifa...
“Tutahakikisha watuhumiwa wanapatikana kwa mikono yote miwili na hatua
za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.”
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema alisema juhudi za kuwasaka watuhumiwa zinaendelea kwa ushirikianao wa wananchi.
“Kifo
cha Kamanda Barlow kimeacha pengo kwani hivi sasa askari mmoja
analinda watu 1,300 hivyo kwa kifo chake unaweza kuona ni pengo la
aina gani na ukilinganisha yeye alikuwa kamanda wa mkoa mzima,” alisema
IGP Mwema.
Alisema jeshi lake litaendelea kulinda amani ya wananchi na kifo cha Kamanda Barlow kinalifanya liongeze nguvu.
Akitoa
mahubiri, Padri Veri Urio alisema kila jambo hutokea kwa wakati na
kifo cha Kamanda Barlow kimesababishwa na watu. Alisema mwenye mamlaka
ya kuondoa uhai wa mtu ni Mungu pekee hivyo waliosababisha kifo chake
siku ikifika, watajibu kwa nini walifanya hivyo.
IGP
Mstaafu, Omary Mahita alisema atamkumbuka Kamanda Barlow kwa uchapaji
wake kazi tangu akiwa polisi Interpol (polisi kimataifa)alifanya kazi
kwa weledi uliotukuka.
“Daima
nitamkumbuka kwani nimefanya naye kazi sehemu tofauti na askari
waliobaki waige mfano wake wa uwajibikaji” alisema Mahita.
Mbali
ya Dk Bilal, viongozi wengine walioshiriki katika ibada hiyo jana ni
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, makamanda wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), makamanda wa polisi, viongozi wa Serikali
na vyama vya siasa na wananchi.
Imeandikwa na Frederick Katulanda, Mwanza na Ibrahim Yamola, Dar.
CHANZO CHA HABARI HII NI "GAZETI LA MWANANCHI".
Social Plugin