Send to a friend |
MAHAKAMA ya hakimu mkazi wa Wilaya ya Geita, imemtia hatiani Pendo Fikiri (20) mkazi wa Mtaa wa Mwembeni Kijiji cha Nyankumbu wilayani Geita baada ya kupatikana na hatia ya kuiba mtoto mwenye umri wa miaka sita kishirikina. Katika hukumu hiyo, Pendo amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na Hakimu wa mahakama hiyo, Zablon Kesase, baada ya kupatikana na hatia ya kumuiba mtoto huyo (jina linahifadhiwa) na kuishi naye nyumbani kwake katika kipindi cha wiki tatu huku akijua kuwa siyo wake. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Kesase alisema kuwa adhabu aliyoitoa kwa mshitakiwa imekusudiwa kuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo hapa nchini na kuonywa watu wenye tabia kama hizo kuacha. ''Mahakama inamtia hatiani kwa kosa hili ambalo umekiri hapa wewe mwenyewe, hivyo hakuna shaka kwamba ulilitenda. Kosa ulilokiri ni kinyume cha kifungu cha sheria namba 169 (1) (a) kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, hivyo pasipo kutilia shaka yoyote ninakuhukumu kwenda jela miaka mitatu ili liwe fundisho kwako,'' alieleza katika hukumu hiyo. Awali akisomewa mashitaka na Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Abner Wegoro, alidaiwa kwamba alitenda kosa hilo Septemba 30 mwaka huu, majira na saa 6 mchana eneo la Mtaa wa Mwembeni wilayani humo. Alisema, baada ya mshitakiwa kumuiba mtoto huyo kwa njia za ushirikina, aliishi naye kwa muda wa wiki tatu hadi wazazi wa mtoto huyo walipopata taarifa toka kwa majirani ambao walimsikia mtoto akilia toka nyumbani kwa huki wakitambua yeye hana mtoto. Alisema kutokana na kupotea kwa mtoto huyo katika mazingira ya kutatanisha wazazi wake walilazimika kutoa taarifa kwa uongozi wa jeshi la sungu sungu kijijini hapo, ambapo Oktoba 17 mwaka huu, majira ya 5.00 asubuhi mshitakiwa huyo alikamatwa na kisha kufikishwa kituo cha polisi. Akijitetea mahakamani hapo, mshitakiwa huyo aliwaacha hoi wasikilizaji baada ya kueleza kwamba alimuiba mtoto huyo kwa ajili ya kumtumia kishirikina lakini bahati mbaya alikamatwa na hivyo kuomba mahakama hiyo kumsamehe kwani alitenda hayo kutokana na mumewe kuwa mbali naye. Licha ya utetezi wake huo, mahakama hiyo ilimtia hatiani na hivyo kutwaliwa na askari kupelekwa gerezani kwa ajili ya kuanza kutumikia kifungo chake. |
Social Plugin