MTOTO ANAYETUHUMIWA KUKOJOLEA QURAN NA WAKAZI 35 WA MBAGALA WAFIKISHWA MAHAKAMANI



Watuhumiwa
wa vurugu za Mbagala wiki iliyopita, wakiwa chini ya ulinzi wa polisi,
walipofikishwa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa
mara ya kwanza jana. Watuhumiwa 29, wawili kati yao wanawake, walisomewa
mashtaka mbalimbali kuhusiana na vurugu zilizopelekea makanisa kadhaa
kuchomwa moto wiki iliyopita, chanzo ikiwa ni baadhi ya watu wanaodaiwa
kuwa waislamu, kuandamana wakipinga mtoto mmoja kukojolea Quraan tukufu.
Dhamana ya watu hao itaamuliwa Oktoba 30.
.........................................



Mtoto
anayetuhumiwa kukojolea Quran Tukufu pamoja na wakaazi 35 wa Mbagala,
Dar es Salaam, wanaodaiwa kuchoma makanisa na kuharibu magari za
Serikali wamefikishwa kizimbani  leo  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu chini ya ulinzi mkali wa Polisi.

Mtoto
huyo mwenye umri wa miaka 14 (jina limehifadhiwa), na ni mwanafunzi,
alifikishwa mahakamani hapo kwa shtaka la kudhalilisha dini ya Kiislamu
kwa kukojolea Quran Tukufu Oktoba 10 mwaka huu, akiwa eneo la Mbagala
Chamazi. Kesi hiyo inasikilizwa katika mahakama ya watoto kwa sababu
mtoto huyo ana umri chini ya miaka 18.


Washtakiwa
wengine  waliosomewa mashtaka yao ni Maenga Yusuph (28), Hamad Euli
(26),Shego Musa (26), Abdallah Said (22),Ramadhan Salum (28), Mashaka
Iman (21), Kassimu Juma (33), Ibrahim Jumanne (20), Sospeter  John (33),
Hamza Mohamed (22), Mwanahamisi Mohamed (30) , Dodo Mohamed (20) na
wengine 23.


Wakazi
hao wa Mbagala wanashtakiwa na makosa manne ya kula njama, kuharibu
mali, wizi, kuvunja majengo na kuchoma moto makanisa  kati ya Oktoba 10
na 12 mwaka huu kwa nia ovu ya kutenda kosa.


Wakili
wa Serikali, Tumaini Kweka, alimwambia  Hakimu Sundi Fimbo wa mahakama
hiyo kuwa washtakiwa walivunja na kuingia ndani ya Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbagala, na kutenda makosa hayo.


Washtakiwa hao pia wanatuhumiwa kuharibu mali mbali mbali zenye thamani ya sh. milioni 500 za  kanisa la KKKT.


Pia
wanatuhumiwa kuiba vitu mbalimbali  vyenye thamani ya sh. milioni 20,
lakini kabla ya kuiba mali hizo walimtishia Michael Samwel kwa kutumia
nondo na matofali kwa nia yakufanikiwa kuiba mali hizo.


Washtakiwa
hao wanatuhumiwa kuchoma moto kanisa la ELCT, kanisa la Agape Usharika
wa Mbagala na kusababisha uharibifu wa mali zenye thamani ya sh. milioni
80.


Vile
vile washtakiwa wanatuhumiwa kuharibu magari tisa, ambapo thamani ya
uharibifu huo ni sh. milioni 20. Katika ya gari ambazo zimeharibiwa
 lipo gari la  Serikali PT 2068 mali ya Jeshi la Polisi,  gari lingine
ni la  Mchungaji Kinyota.


Pia
wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, alidai kuwa washtakiwa
wanatuhumiwa kuvunja kanisa la  Tanzania Assemblies of God (TAG), KKKT
na kuiba vitu mbali mbali vyenye thamani ya sh. milioni 8 mali ya Kanisa
la Waadventisti Wasabato (SDA).


Mawakili
hao wa Serikali walidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika,
na waliomba mahakama itoe masharti ya dhamana kwa kuzingatia kifungu
namba 148 kifungu kidogo cha 5 (e).


Kesi
hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 30 mwaka huu kwa kuangalia dhamana za
washtakiwa, ambapo kuna washtakiwa wengine hawatapata dhamana kwa sababu
wamepatikana na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha. Kisheria
shtaka hilo halina dhamana kwa hiyo washtakiwa hao wataendelea kusota
rumande.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post