SOMA: TAARIFA YA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MWANDISHI WA HABARI WA CHANNEL TEN BW. DAUD MWANGOSI
Wednesday, October 10, 2012
1.0 UTANGULIZI
Mnamo tarehe 03 Septemba mwaka 2012, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi (MB) aliteua Kamati ya watu watano kufanya
uchunguzi kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha
televisheni cha Channel Ten, marehemu Daud Mwangosi, kilichotokea tarehe
02 Septemba 2012, katika Kijiji cha Nyololo,Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa
Iringa. Kituo cha kazi cha marehemu Daud Mwangosi kilikuwa mkoa wa
Iringa ambapo pia alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa
Mkoa wa Iringa (IPC).
Wajumbe wa Kamati hiyo ni:
Jaji (Mst.) Steven Ihema – Mwenyekiti
Bibi Pili Mtambalike – Mjumbe
Kanali (Dkt. Eng) Wema Wilson Wekwe – Mjumbe
Bwana Theophil Makunga – Mjumbe
Naibu Kamishna wa Polisi Issaya Juma. Mngulu – Katibu
Sekretarieti ya Kamati ni:
Bi. Edith T. Assenga – Wizara ya Mambo ya Ndani
Bwana Nasoro H. Msumi – Wizara ya Mambo ya Ndani
2.0 HADIDU ZA REJEA
Kamati ilipewa Hadidu za rejea zifuatazo:
- Uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo,Wilaya
ya Mufindi, Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba, 2012 na kuwepo kwa
uvunjifu wa amani.
- Kama yalikuwepo makubaliano au maelekezo kuhusu mikutano ya hadhara au maandamano nchini katika kipindi cha Sensa.
-Mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu iliyosababisha
kifo cha Marehemu Daud Mwangosi na wengine kuumizwa, na uwiano wa nguvu
hiyo na tukio.
-Madai ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la
Polisi na Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa na chanzo cha uhasama huo.
Aidha kuna madai ya kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao
Jeshi la Polisi limepanga kuwashughulikia.
-Uwepo wa Sheria,
Kanuni au Taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la Polisi kuzuia
mikusanyiko inayoitishwa na Vyama vya Siasa na Mamlaka ya Rufaa endapo
vyama hivyo havitaridhika na amri hizo.
-Hali ya Mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa nchini katika Utendaji kazi wao na Utii wa Sheria.
3.0 MUDA WA UCHUNGUZI
Kamati ilipewa muda wa siku 19 kuanzia tarehe 11 Septemba 2012 iwe
imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha Ripoti yake ifikapo tarehe 02
Oktoba 2012.
4.0 NJIA ZILIZOTUMIKA KUFANYA UCHUNGUZI:
4.1 Mahojiano na watu mbalimbali waliokuwepo kwenye tukio.
4.2 Kupitia nyaraka na vielelezo mbalimbali.
4.3 Kutembelea eneo la tukio.
4.4 Majadiliano na vikundi mbalimbali (viongozi wa dini ngazi ya kijiji
na wilaya hadi ya mkoa; viongozi wa vyama vya siasa kwenye ngazi ya
kijiji, wilaya, mkoa na Taifa, viongozi wa serikali ngazi ya kijiji,
wilaya, mkoa, Taifa) na wanakijiji wa Nyololo.
5.0 UCHUNGUZI
Kamati ya Uchunguzi ilifanya mahojiano na watu mbalimbali ikiwa pamoja
na watendaji wa serikali hususan Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya
wilaya Mufindi na mkoa wa Iringa viongozi wa Jeshi la Polisi viongozi wa
vyama vya Siasa, Viongozi wa Madhehebu ya Dini, Waandishi wa Habari na
wananchi wa kawaida (ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa).
6.0. YALIYOJITOKEZA
Baada ya Kamati kukutana na makundi ya watu mbalimbali katika Mkoa wa
Iringa na Viongozi wa Vyama vya Siasa wa kitaifa jijini Dar es Salaam,
mambo kadhaa yalijitokeza na baadhi yao ni:
-Hofu ya kutoweka
kwa amani miongoni mwa viongozi na wananchi hasa katika mikutano na
maandamano ya siasa ambayo yameanza kuota mizizi ya uvunjifu wa amani na
mengine kusababisha mauaji. Viongozi na wananchi wengi waliotoa maoni
yao mbele ya Kamati wameonyesha hofu kuwa hali hiyo isipodhibitiwa
mapema inaweza kulipeleka pabaya Taifa letu.
-Kuna walakini wa mahusiano kati ya waandishi wa habari na Jeshi la Polisi mkoani Iringa.
-Uwepo wa utashi wa makusudi/dhati kwa viongozi wa vyama vyote vya
siasa kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya vyama.
-Umuhimu wa Ushirikiano na mahusiano baina ya vyombo vya serikali,
vyama vya siasa, wanahabari na wananchi kwa ujumla badala kuonyeshana
ubabe ambao umetufikisha hapo.
- Haja ya kufanya mabadiliko ya kisheria katika mfumo wa usimamizi na utendaji wa masuala ya siasa nchini
- Haja ya kuwa na mabadiliko ya kimfumo katika Jeshi la Polisi badala
ya ulioko sasa ambao kwa maoni ya baadhi ya watu waliozungumza na Kamati
ni wa kitaifa zaidi na kuacha serikali za mitaa bila ya wajibu wa
kulinda usalama wa raia na mali zao.
-Kwamba nguvu kubwa inatumika na vyombo vya dola/usalama dhidi ya raia na hivyo kupunguza imani ya jamii kwa vyombo hivyo.
-Kupungua kwa maadili/uzalendo miongoni mwa Watanzania kuanzia viongozi hadi wananchi hususan kwenye shughuli za kisiasa.
-Haja ya kusisitiza elimu ya uraia kwa jamii kuanzia kwa watoto hadi
kwa watu wazima hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi ili kujenga
umoja wa kitaifa.
-Kuwepo kwa mikutano na maandamano ya vyama vya siasa yasiyokuwa na kikomo.
-Muonekano wa Jeshi la Polisi mbele ya jamii.
7.0. MATOKEO YA UCHUNGUZI KUTOKANA NA HADIDU ZA REJEA
7.1 Kuhusu “Uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la
Nyololo, Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba 2012 na
kuwepo uvunjifu wa amani”, uchunguzi wa Kamati umebaini yafuatayo:
Tarehe 30 Agosti 2012 CHADEMA iliandika barua, Ofisi ya Mkuu wa Polisi
Wilaya ya Mufindi kutoa taarifa kuhusu ratiba ya mikutano ishirini na
sita (26) kwenye majimbo ya Mufindi Kusini na Kaskazini tarehe 02-03
Septemba 2012. Awali ratiba ya mikutano hiyo ilikubaliwa, lakini baadaye
siku hiyo ya tarehe 01 Septemba 2012 mikutano hiyo ilisitishwa kwa
barua Kumb. Na MFG/A.24/9/54 kutokana na kuongezwa siku za zoezi la
Sensa ya watu na Makazi hadi tarehe 08 Septemba 2012.
CHADEMA
walikataa kusitisha ratiba ya mikutano hiyo kama inavyothibitishwa na
Justin Leornard Mpotwa Katibu wa Wilaya ya Mufindi kwa barua yake Kumb.
Na CDM/M4/002/Vol.01/2012 ya tarehe 01 Septemba 2012 kuwa “pia tunaomba
ieleweke bayana kwamba kisheria shughuli zetu hazina mwingiliano na wala
kuhusiana na program iliyoongezwa ya Sensa. Kwa barua hii tunakuarifu
kuwa mikutano tuliyokutaarifu kuifanya kuanzia kesho tarehe 02 septemba
2012 itaendelea kama ilivyopangwa – CHADEMA VEMA”.
Aidha kuwepo
kwa zuio la mikutano ya Siasa ya CHADEMA Mkoani Iringa wakati wa zoezi
la Sensa ya Watu na Makazi linathibitishwa na Amri ya Utendaji
(Operation Order) ya Kamanda wa Polisi Mkoa (SACP Michael Kamuhanda) ya
tarehe 01 Septemba 2012. Amri ya Utendaji ambayo ni amri halali
ilitolewa ili “kuzuia shughuli za Siasa (mikutano na maandamano) kipindi
cha zoezi la kitaifa la Sensa kuanzia tarehe 25 Agosti 2012 hadi 08
Septemba 2012”. Uhalali wa Amri/Zuio hili ulithibitishwa pia na Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini katika barua yake Kumb Na. DA. 112/ 123/ 01/
34 ya tarehe 28/08/2010 na wakati wa mahojiano na Kamati ya uchunguzi
tarehe 22 Septemba 2012.
Licha ya zuio/amri hii Viongozi wa
CHADEMA walikataa kutii amri hiyo. Kutokana na taarifa hizi, Kamati ya
Uchunguzi inathibitisha kwamba hapakuwepo na uhalali wa
mkusanyiko/mkutano ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo, Wilaya ya
Mufindi, Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba 2012. Kuhusu kuwepo kwa
uvunjifu wa amani Kijijini Nyololo tarehe 02 Septemba 2012 Kamati ya
Uchunguzi ilibaini mambo yafuatayo:
-Tukio la kuuawa kwa Daud
Mwangosi jioni ya tarehe 02 Septemba 2012 lilitokea baada ya Operesheni
ya Jeshi la Polisi kumalizika. Hii ni kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa
Iringa na Joseph Senga Mpiga picha/Mwandishi Tanzania Daima.
-
Kitendo cha kutotii amri halali ya Kamanda wa Polisi kuagiza wafuasi wa
CHADEMA watawanyike kutoka kwenye eneo la ofisi ya Kata ya CHADEMA
ilikuwa chanzo cha vurugu.
Uamuzi wa CHADEMA kung’ang’ana
kukusanyika isivyo halali eneo la Nyololo ikizingatiwa kuwepo kwa ujumbe
wa SMS kutoka kwa Dkt. Slaa, Katibu wa CHADEMA uliosema, “IGP nasubiri
simu yako. Wajulishe Polisi wako waandae risasi za kutosha, mabomu ya
kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha kusherehekea, mjiandae kwa
kwenda mahakama ya Den Hague. Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya”.
Dr. Slaa. : ujumbe huu ukiashiria umwagaji wa damu ni ushaidi tosha
kuwepo kwa uvunjifu wa amani. CHADEMA ndiyo Chanzo cha vurugu na
uvunjifu wa amani Kijijini Nyololo tarehe 02 Septemba 2012.
7.2
Kama yalikuwepo makubaliano kuhusu mikutano ya hadhara au maandamano
nchini katika kipindi cha Sensa. Katika kuzungumzia hoja hii tukianzia
na Uongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi
Taifa, Kamati ya Uchunguzi ilithibitisha kuwepo kwa maagizo ya
kusimamisha mikutano/maandamano ya Vyama vya Siasa wakati wa kipindi cha
Sensa ya Watu na Makazi yaliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini, na kuongezwa muda wa Sensa hadi tarehe 08 Septemba 2012 na
Kamishna wa Sensa hapo tarehe 01 Septemba 2012.
Aidha hoja hii
imethibitika kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa barua yake
yenye Kumb Na DA. 112/ 01/ 34 ya terehe 28 Agosti 2012 kwenda kwa
Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa akiwasihi kusimamisha shughuli zote za
mikutano na maandamano ya Vyama vyao kwa kipindi chote cha Sensa ya
Watu na Makazi. Aidha kwa mujibu wa Gazeti la Serikali Na 29 VOL 93 ya
tarehe 20 Julai 2012, Mhe. Rais, JAKAYA MRISHO KIKWETE kwa mamlaka
aliyopewa chini ya kifungu namba 14 cha Sheria ya Takwimu sura 351
alielekeza kwamba Sensa ya Watu na Makazi itafanyika kuanzia tarehe 26
mwezi wa nane, mpaka tarehe 08 mwezi wa tisa mwaka 2012.
Kamishna wa Sensa aliratibu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kumalizika
ifikapo tarehe 01 Septemba 2012. Hata hivyo kutokana na tathmini
aliyofanya, kazi hiyo ilikuwa imekamilika kwa asilimia 95%. Hivyo tarehe
01 Septemba 2012 alitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kwamba ili kila
mwananchi apate nafasi ya kuhesabiwa watu watakaokuwa wamesalia ambao ni
chini ya 5% wanaombwa kutoa ushirikiano ili zoezi hili likamilike.
Hivyo, wale wote mmoja mmoja waliobakia wataendelea kuandikishwa hadi
tarehe 08 Septemba 2012.
Kwa upande wake Inspekta Jenerali wa
Polisi kwa ujumbe wa simu Kumb Na S8.7/ 2/ A/ VOL XIV/ 59 ya tarehe
28/08/2012, pia simu yake Kumb Na C.28/ B/ 44 ya terehe 01/ 09/ 2012
aliwaelekeza Makamanda wa Polisi wa Mikoa kutoruhusu mikutano na
maandamano wakati huu wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi mpaka
litakapokamilika tarehe 08 Septemba 2012.
Kimsingi Kamati ya
uchunguzi imethibitisha kwamba maelekezo kwa Vyama vya Siasa kutoendesha
shughuli za mikutano ya hadhara au maandamano yalitolewa kwa mujibu wa
Sheria.
7.3 Mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia
nguvu iliyosababisha, kifo cha marehemu Daud Mwangosi na wengine
kuumizwa, na uwiano wa nguvu hiyo na tukio.
Hoja kuwa Polisi
walitumia nguvu kubwa katika kudhibiti mkutano wa CHADEMA iliungwa mkono
na Viongozi wa Serikali ya Kijiji, Viongozi wa dini na Viongozi wa
siasa Kijijini Wilayani na Mkoani pamoja na Waandishi wa Habari. Hata
hivyo Kamati za Ulinzi na Usalama Wilaya na Mkoa na Viongozi wa Jeshi la
Polisi waliona nguvu hizo ni za mazingira ya hali ilivyokuwa.
Uchunguzi wa suala hili umebaini kwamba tarehe 02 Septemba 2012 muda wa
saa 10 za jioni huko eneo la Sokoni, Kijiji cha Nyololo kulikuwepo na
mkutano usio halali ulioandaliwa na viongozi wa CHADEMA. Upo ukweli
kwamba uongozi wa Polisi ulitoa ilani kuamuru wafuasi wa CHADEMA
waliokuwepo mkutanoni hapo waondoke la sivyo nguvu itatumika. Walikaidi
amri hiyo na ilipoagizwa viongozi wakamatwe ndipo walianza kurusha mawe
kwa Askari Polisi. Baadhi ya Askari walijeruhiwa, akiwamo G 9934 PC
Mgaka alivunjwa mkono wa kulia. Pia kofia (helmet) tatu ziliharibiwa.
Kutokana na hali hiyo amri ya kupiga mabomu ya machozi na ya kishindo
ilitolewa, kwa mujibu wa Kifungu 77 hadi 79 cha Kanuni za Adhabu, Sura
ya 16 – R.E 2002. Operesheni hii ilimalizika baada ya kukamatwa viongozi
na wafuasi wa CHADEMA jumla yao saba.
Baada ya zoezi hilo
kukamilika Askari Polisi walioshiriki kwenye Operesheni waliamriwa
kuingia katika magari tayari kwa kuondoka. Wakati Askari wakipanda
kwenye magari kishindo kikubwa kilitokea umbali wa zaidi ya mita 100
kutoka sehemu ambayo operesheni ilikuwa inafanyika na iligundulika
kwamba kishindo kile kimesababisha kifo cha Mwandishi wa Habari Daud
Mwangosi.
Upelelezi wa awali pamoja na picha za mnato
unaonyesha kwamba marehemu alikuwa amemkumbatia Mkuu wa Polisi Kituo cha
Mafinga ASP Assel Mwampamba na huku akiwa amezungukwa na Askari Polisi
wasiopungua sita ambao licha ya kumzunguka marehemu Daud Mwangosi kuna
madai yaliyotolewa na mwandishi wa Habari Joseph Senga kwamba, Askari
Polisi hao walikuwa wanamshambulia marehemu kwa kumpiga, ndipo askari
mmoja aliyetambuliwa kuwa ni G 2573 PC Pasificus Cleophace Simon
alifyatua Bomu la kishindo na kusababisha kifo cha Daud Mwangosi.
Tukio hili linaweza kugawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza
ni wileamapamebas(mni ya kutawanya watu na ya pili ni ile ya mauaji ya
Daud Picha Namba 15: Askari Polisi wakimpiga Marehemu Daud Mwangosi,
huku OCS M wenye kifimbo) akijaribu kuwazuia. Mwangosi. Katika tukio la
kwanza idadi ya Askari walioshiriki ni Sekisheni Tukio hili linaweza
kugawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza ni lile ya Operesheni
ya kutawanya watu na ya pili ni ile ya mauaji ya Daud Mwangosi.
Katika tukio la kwanza idadi ya Askari walioshiriki ni Sekisheni tatu
ambapo ni askari wasiozidi thelathini. Kwa maelezo yaliyotolewa na
Mwandishi wa Habari mbele ya Kamati, Bw Joseph Senga anaeleza kuwa watu
walishatawanyika na hali kutulia mara baada ya Operesheni hii kukamilika
na Polisi kujiandaa kuondoka kwenye eneo la tukio. Tukio la mauaji ya
Daud Mwangosi lilisababishwa na kupigwa bomu la kishindo.
Maswali ya kujiuliza katika tukio la mauaji ni Je, kulikuwepo na uwiano
unaolingana na tukio hili?, Je Palikuwa na uhalali wa kutumia Bomu la
kishindo?, na Je, utumiaji wa Bomu hilo ulikuwa na umuhimu?
Kulingana na tukio lenyewe majibu ya maswali hayo ni kama ifuatavyo:
-Hapakuwa na uwiano wa Bomu na tukio la mauaji, kwa vile utaratibu wa
matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45 na umbali
mita 80 mpaka mita 100.
-Hapakuwa na uhalali wa kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia.
- Hapakuwepo umuhimu wa kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata
ingekuwa ukamataji tayari Askari Polisi wapatao sita walikuwepo eneo la
tukio.
Kwa misingi hiyo Kamati imeona kwamba nguvu iliyotumika
mwanzo hadi kumaliza Operesheni haikuwa kubwa. Kuhusu tukio la kuuawa
Bw. Daud Mwangosi na kuumizwa baadhi ya Askari Polisi halikustahili
kabisa.
7.4 Madai ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na
Waandishi wa Mkoa wa Iringa na chanzo cha uhasama huo. Aidha madai ya
kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao Jeshi la Polisi
limepanga kuwashughulikia.
Katika kupata ukweli wa jambo hili,
Kamati ilikutana na wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa na
pia iliwahoji Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda,
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Nyigesa Ramadhani Wankyo na Mkuu wa Kikosi
cha Kutuliza Ghasia mkoani Iringa Said Abdallah Mnunka.
Pia,
wakati Kamati inakutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ilileta
suala la mahusiano kati ya Polisi na waandishi wa habari na watendaji
wakuu wa serikali wa mkoa wa Iringa.
Katika mkutano na
waandishi wa habari, ilionekana kuwa katika thathmini yao uhusiano kati
yao na Polisi hapo mkoani ni mbaya sana. Walieleza matukio kadhaa ya
kunyanyaswa waandishi wa habari wakati wapo kazini, ikiwamo kupigwa,
kutishiwa kuharibiwa na kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na hata kutishiwa
maisha ili wasiripoti mambo ambayo Polisi wana maslahi nayo.
Kwa mfano, mwandishi wa habari wa Star TV, Oliver Moto alieleza Kamati
kuwa: “Waandishi wa habari hawana mahusiano mazuri na Jeshi la Polisi,
na hata wanapofika ofisi za Polisi huwa hawapewi ushirikiano. Kutokana
na uhusiano mbaya wanahabari walifanya maandamano tarehe 06 Machi 2012
kupinga unyanyasaji wanaofanyiwa na Jeshi la Polisi hapa Iringa”.
Mwandishi mwingine wa habari Zulfa Shomari ambaye anaandikia gazeti la
Mwananchi alieleza kuwa kuna matukio kadhaa ambayo Polisi wamewazuia
waandishi kufanya kazi zao mojawapo ni lile ambalo Polisi walikataza
kupigwa picha tukio la kukamatwa kwa pembe za ndovu.
Kamati pia
iielezwa na mwandishi wa habari wa ITV, Bw. Laurian Mkumbata mkasa wa
kuvunjwa kamera yake na OCD Iringa kwenye tukio moja. Ilibidi OCD alipe
kamera hiyo kwa maagizo ya RPC.
Pia walisema kuwa Kamanda wa
Polisi wa Mkoa hivi sasa ana mawasiliano duni sana na waandishi wa
habari na juhudi za wengi wao kumfuata ili athibitishe tukio zimekuwa
zikishindwa kwani ameweka maagizo getini kuwa mtu yeyote ambae anataka
kumuona ni lazima aeleze anataka kumuona kwa sababu gani ndipo aruhusiwe
kuingia. Kwa sababu hii waandishi wa habari wengi wamekata mguu kwenda
ofisini kwake.
Mwandishi mmoja wa Ebony FM Bw. Raymond Francis,
aliiambia Kamati kuwa yeye binafsi alitishiwa kuuawa na baada ya
kuandaa kipindi kuhusiana na watu wanaoshukiwa kufanya biashara haramu
ya madawa ya kulevya ambao wanahusiana na baadhi ya Polisi wasio
waadilifu.
Mwandishi wa Habari Greyson Mgoi wa gazeti la
Kwanza Jamii aliiambia Kamati kuna tukio la kuanguka kwa lori la mafuta
eneo la Ifunda karibu na Mafinga ambapo waliwakuta wananchi na polisi
wakichota mafuta kutoka kwenye hilo gari.
Alisema kuwa waliamua
kupiga picha tukio hilo lakini Polisi waliwakamata na kuwalazimisha
wafute hizo picha walizopiga. Kwa kuogopa shari walikubali kuzifuta na
wakaruhusiwa kuendelea na safari yao.
Waandishi wa Habari hata
hivyo walibainisha kuwa uhusiano wao na Polisi hapo mkoani ulikuwa mzuri
sana kipindi cha uongozi wa RPC Advocate Nyombi. Walisema kuwa wakati
wa RPC Nyombi, alikuwa na utaratibu wa kukutana na waandishi wa habari
na pia alikuwa anafikiwa na waandishi wa habari kwa urahisi kwa simu au
ofisini kwake. Walisema lakini ulianza kuharibika alipohama na nafasi
yake kuchukuliwa na RPC Mangara na kuwa mbaya zaidi alipokuja Kamuhanda.
Walidai kuwa Polisi wa Iringa si waadilifu na wamekuwa wakijiona kama
miungu watu.
Waandishi walieleza Kamati, kitu kilichowaudhi
sana ni yale majibu yaliyotolewa na RPC baada ya mauaji ya Daud Mwangosi
ambayo yalionekana yalikuwa ni ya kupanga ili ukweli usijulikane.
Walisema kama si picha zilizotolewa na waandishi wa habari waliokuwepo
kwenye tukio, hawadhani kama umma wa Watanzania wangepata ukweli wa
tukio hilo.
Walisema tarehe 06 Machi 2012, walifanya maandamano
ili kupinga manyanyaso ya Polisi wa mkoani Iringa yaliyopokelewa na
Mkuu wa Mkoa. Waandishi wa Habari mkoani Iringa pia walionyesha
masikitiko yao kuwa tangu kutokee kwa mauji ya Daud Mwangosi,
hawajapokea pole kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na watendaji wake wa juu hata
kama ni ya “kinafiki”.
Kwa upande wa pili, yaani Jeshi la
Polisi, Kamati ilipata taswira tofauti. RPC Kamuhanda alisema kuwa yeye
anaona mahusiano ya Polisi na waandishi wa habari kwa ujumla ni mzuri na
yeye binafsi amekuwa akikutana na waandishi wa habari takriban kila
siku asubuhi saa nne kuwapa habari. Pia aliiambia Kamati kuwa waandishi
wa habari walishiriki kikamilifu katika kuripoti michuano ya mpira ya
Kikombe cha Kamuhanda yaliyofanyika mjini Iringa.
Msimamo huo
pia ulichukuliwa na viongozi wa juu wa kiutawala akiwemo Mkuu wa Mkoa
Dkt. Christine Ishengoma, Katibu Tawala wa Mkoa Bibi Getrude Mpaka ambao
walisema kuwa hapakuwa na uhasama wowote kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
na Waandishi wa Habari. Wote wawili walisema kuwa walimfahamu marehemu
Daud Mwangosi na aliteuliwa katika kamati kadhaa za kimkoa ikiwa ni
pamoja na ile ya kuandaa Sensa ya Watu na Makazi Mkoani, Kamati ya
Masuala ya Katiba ya Mkoa na Kamati ya Kukuza Utalii ya Mkoa.
Kuhusiana na hisia kuwa Mkuu wa Mkoa na watendaji wake hawakujumuika na
waandishi katika msiba wa Daud Mwangosi, Dkt. Ishengoma alisema si kweli
hawajatoa rambirambi zao kwa kifo cha Mwangosi lakini alitoa pole kwa
waandishi wakati ameenda na IGP Mwema kijijini Nyololo na pia kupitia
radio katika kipindi kilichotayarishwa na mwandishi wa habari Francis
Godwin.
Baada ya kuongea na pande hizo mbili, Kamati imebaini
kwamba kuna walakini wa mahusiano kati ya waandishi wa habari na baadhi
ya askari polisi mkoani Iringa. Kuhusu madai ya kuwepo kwa orodha ya
waandishi watatu (3) ambao jeshi la polisi limepanga kuwashughulikia.
Kwenye tukio la Nyololo ambapo mwandishi wa habari Daud Mwangosi
aliuawa, mwandishi wa habari mwengine Godfrey Mushi alipigwa na Polisi
na inasemekana kujeruhiwa vibaya na baadaye kukamatwa na Polisi.
Kwa mujibu wa Joseph Senga mpiga picha/mwandishi wa habari wa gazeti la
Tanzania Daima ambaye alikuwepo kwenye tukio na kupiga picha, alimuona
marehemu akipita nyuma ya gari moja la Polisi ambalo lilikuwa na baadhi
ya wanachama wa CHADEMA. Punde tu alimwona mtu amezungurukwa na askari
akipigwa lakini hakujua ni nani na yeye aliendelea kupiga picha tukio
hilo mpaka nae alipokamatwa na Polisi watatu ambao walimwuliza kama nae
anataka aende kuungana na mtu anayepigwa pale.
Senga alisema
wakati kipigo kinaendelea, kuna askari mmoja mwenye nyota tatu (OCS
Mwampamba) aliteremka kutoka kwenye gari na kwenda pale ambapo Yule mtu
aliyekuwa anapigwa huku akiwaambia “mwachieni, mwachieni, namfahamu mimi
huyo ni mwandishi wa habari!”
Senga alisema mara alisikia
kishindo kikubwa na wale askari ambao walikuwa wanamshikilia walikimbia
ndipo yeye akaendelea kupiga picha sasa za marehemu Daud Mwangosi ambaye
alikuwa amekwisha sambaratishwa na bomu. Alieleza kuwa alimsikia yule
askari ambaye alikuja kumsaidia marehemu Mwangosi akisema “afande
wameniuwa”, “afande wameniuwa”, akimwambia RPC ambaye alikuwa karibu nae
kwani nae aliumizwa vibaya katika mlipuko huo. Senga aliiambia Kamati
wale wote ambao walikuwa wame mzunguka marehemu kama wanavyoonekana
kwenye picha alizopiga walikuwepo wakati anapigwa.
Maelezo ya
Bw. Senga yanatofautiana sana na yale yaliyotolewa na RPC na OC FFU kuwa
Marehemu alimvamia OCS Mwampamba na kuwa wale askari huenda walidhania
kuwa mkubwa wao alikuwa amevamiwa ndipo walipoamua kwenda kumsaidia. OCS
Mwampamba mwenyewe wakati akihojiwa na Kamati ilipokuwa Mafinga alisema
hakumbuki kitu.
Hata hivyo, kwa maelezo ya Bw. Senga, ambayo
yanakubaliana na yale ya RPC na OC-FFU, kitendo cha kupigwa na mauaji ya
marehemu Daud Mwangosi kilitokea baada ya kuisha ile operesheni ya
kusambaratisha mkutano wa CHADEMA na hapakuwa na mabishano yeyote au
purukushani iliyotokea kabla ya marehemu kuzungukwa na kuanza kupigwa.
Kwa minajili hii basi Kamati imeshindwa kubaini baada ya kumalizika
operesheni na askari Polisi kuanza kuondoka, kwa nini Mwangosi
alishambuliwa kwa kipigo kabla ya kulipuliwa na bomu la kishindo?
Kwa nini kuna maelezo yanayokinzana kati ya Bw. Senga ambaye alikuwa
karibu sana na tukio na yale ya RPC na OC-FFU ambao katika maelezo yao
kwa Kamati walisema kuwa wao walikuwa mbali kidogo na tukio kwa hiyo
hawakuweza kuona kwa dhahiri kilichotokea. Maelezeo ambayo yalirudiwa na
viongozi wa juu wa Polisi ikiwa ni pamoja na Kamishna wa Upelelezi
(DCI) Robert Manumba na Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema katika
mahojiano na Kamati.
Uchunguzi wa Kamati haukuweza kupata
ushahidi wa kubainisha kama kupigwa kwa waandishi hao kulitokana na
njama yeyote ya Polisi kuwashughulikia au ilitokea kwenye purukushani ya
vurugu zilizotokea baada ya FFU kuamriwa kutawanya wanachama wa
CHADEMA.
Pia Kamati haikupata ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa
mauaji ya Daud Mwangosi yalikuwa ni ya kupangwa. Kutokana na maelezo ya
hapo juu, Kamati inapendekeza yafuatayo:-
-Taasisi za habari
zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari, hususan Baraza la
Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri wafanye utaratibu unaostahiki za
upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi la Polisi na uongozi wa
mkoa wa Iringa. Hii itasaidia kurejesha uhusiano mzuri kati ya vyombo
hivyo muhimu katika mkoa;
-Waandishi wa habari wapewe mafunzo ya jinsi ya kuripoti matukio ya hatari/ghasia;
-Waandishi wa habari wavae vivazi maalum vya kuwatambulisha wakiwa katika matukio hasa kwenye maeneo hatarishi;
- Waandishi wa habari wafanye kazi kwa weledi, uadilifu, uwazi na wasijibainishe na vyama vya siasa;
- Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Daud Mwangosi kabla hajauawa wachukuliwe hatua stahiki za kisheria;
- Kamati ya Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari
iliyoanzishwa mwaka 2008 ifufuliwe. Na kamati hizo ziteremke hadi kwenye
ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.
- Viongozi wa polisi wanapotoa taarifa za tukio, ziwe zimefanyiwa utafiti wa kina ili zisipotoshe jamii.
7.5 Uwepo wa Sheria, Kanuni au Taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la
Polisi kuzuia mikusanyiko inayoitishwa na Vyama vya Siasa na Mamlaka ya
Rufaa ambapo Vyama hivyo havitaridhika na amri hiyo.
Sheria
Namba 5 ya 1992 kama ilivyorekebishwa na Sheria Namba 7 ya 2009
inaratibu mahusiano ya kiutendaji kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya
Siasa. Kwa mujibu wa Sheria hii Jeshi la Polisi limepewa madaraka ya
kutoa zuio kwa maandishi na kuweka bayana sababu za kuzuia mikutano au
maandamano. Zuio aina hii ni halali kwa mujibu wa Sheria na ni sherti
Chama cha Siasa kiheshimu na kutii. Fungu la 11 vifungu vidogo Na 1, 4,
5, 6, 7 na 8 ya Sheria ya Vyama vya Siasa likisomwa pamoja na mafungu
Namba 43, 44, 45 na 46 ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Auxiliary Forces
Act Sura 322 vitatumika kusimamia uendeshaji mikutano ya Vyama vya Siasa
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na kwamba
Vyama vya Siasa vinatakiwa kutoa taarifa na siyo kuomba idhini, Jeshi la
Polisi limepewa uwezo na madaraka juu ya mikutano hiyo kuhusu kuzuia au
kuruhusu na au kutoa maelekezo stahiki, kama vile kupendekeza, na
kushauri eneo mbadala na tarehe tofauti ya kufanya mikutano/maandamano.
Aidha kutotii amri/zuio ya Jeshi la Polisi ni kosa la Jinai kwa mujibu wa Fungu la 74 la Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura 16 RE.
Vilevile kwa mujibu wa Fungu la 43 (6) ya Sheria ya Jeshi la Polisi na
Auxiliary Forces Act, Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye Mamlaka ya Rufaa
dhidi ya amri/zuio linatolewa na Jeshi la Polisi.
Pamoja na
kuwepo kwa Sheria hizi mbili bado kuna mapungufu katika uendeshaji na
usimamizi wa shughuli za Siasa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Kwa mfano
pamoja na madaraka aliyonayo Msajili wa Vyama vya Siasa ya kukifuta
Chama cha Siasa kwenye rejesta ya usajili kwa mujibu wa Fungu la 19 na
20 ya Sheria ya Vyama vya Siasa, kusimamisha utoaji wa ruzuku na
matumizi yake, uratibu wa shughuli za vyama hivyo hauko mikononi mwake.
Wadau wanashauri umuhimu wa kuimarisha uhusiano katika shughuli za
utendaji kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi
ili kudumisha utulivu na amani na utii wa sheria bila shuruti kwa upande
mmoja na kukuza mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa kwa upande
mwingine.
7.6 Hali ya mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa nchini katika utendaji kazi wao na Utii wa Sheria.
Kamati ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten,
Daud Mwangosi katika kupata majibu kwa hadidu hii ya rejea, ilizungumza
na viongozi wa vyama vya siasa kutoka ngazi za Kijiji cha Nyololo,
Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa na Viongozi wa kitaifa jijini Dar es
Salaam na viongozi wa dini kutoka ngazi za Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya
Mufindi na Mkoa wa Iringa.
Kwa ujumla, kila kiongozi wa chama
cha siasa wa ngazi zote ambaye Kamati imezungumza naye kuhusu hadidu hii
ya rejea, ameelezea umuhimu wa Jeshi la Polisi katika kulinda usalama
wa raia na mali zao na wangependa jeshi hilo liachwe huru katika
kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa na wanasiasa ili lifanye
kazi zake kwa weledi na uadilifu.
Hata hivyo taswira
iliyojitokeza ni kwamba kuna mgawanyiko wa mtizamo kuhusu jinsi Jeshi la
Polisi linavyoshughulikia mikutano/maandamano ya Vyama vya Siasa.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wanaamini kuwa Jeshi la Polisi
linakipendelea Chama cha Mapinduzi na kubinya vyama vya upinzani, huku
viongozi wa CCM kutoka ngazi ya kijiji hadi Taifa wakilisifia Jeshi hilo
kuwa linafanya kazi yake vizuri na kwa weledi mkubwa.
Mgawanyiko wa taswira kuhusu madai kuwa Jeshi la Polisi kuipendelea CCM
hauko tu kati ya vyama vya upinzani na CCM bali pia kwa viongozi wa dini
kuanzia ngazi za kijiji, wilaya hadi mkoani Iringa kwa maelezo kuwa
hawajasikia hata siku moja mtu anauawa na Polisi kwenye mkutano wa CCM.
Mwandishi mmoja alitoa udadisi wake kuwa huwa wanapata shida sana
kuandika habari za mikutano ya CHADEMA kutokana na jinsi Polisi
wanavyojipanga kwenye mikutano ya chama hicho.
Kudhihirisha
umuhimu wa Jeshi la Polisi katika jamii, hata wale wanaolituhumu kuwa
linakipendelea CCM, katika kutoa maoni yao kuhusu hatua za kuchukuliwa
askari wanaoharibu sifa ya Jeshi hilo, wanapendekeza kuwa askari
wahusika wachukuliwe hatua na kuomba Jeshi hilo liendeshwe kwa weledi
hasa inapotokea askari akalazimika kutumia silaha kukabiliana na fujo
isifikie kuua.
Kwa mfano, Mchungaji Peter Katanga wa Revival
Baptist Church, alishauri chombo cha Polisi kisitumike kufanya mauaji,
au kisitumike na mtu, watu, au kikundi chochote kufanya matendo yasiyo
mazuri kwa jamii kwa sababu chombo hicho kipo kwa ajili ya kulinda
usalama wa raia wote na mali zao.
Viongozi wa siasa wengine
bila kujali itikadi zao, wameonekana kukerwa sana na tabia ya watu
kuuawa wakati Jeshi la Polisi linatuliza ghasia na hii ikiachiwa
iendelee inaweza kuleta uvunjifu wa amani katika nchi. Kwa mfano,
Mchungaji wa Kanisa la EFATA Nyololo, Mkombozi Kiliwa alishauri Polisi
watumie njia zinazofaa kukabiliana na wanaovunja sheria na si kuua.
Pia Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyololo, Obby Kimbale, alielezea
kutokukubaliana kwake na kitendo cha mauaji ya Daud Mwangosi,
alipendekeza elimu ya uraia itolewe kwa jamii nzima vikiwemo vyombo vya
dola, viongozi wa serikali, wanasiasa na wananchi kwa ujumla wao ili
kila mtu kwa nafasi yake akaelewa namna ya kutimiza wajibu wake ndani ya
mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Kwa upande mwingine, wengi
waliotoa maoni yao juu ya mahusiano ya Polisi na vyama vya siasa,
pamoja na kulaumu Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa katika kukabiliana
na wafuasi wa CHADEMA, pia waliwalaumu viongozi wa chama hicho, kwa
kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi hatimaye kusababisha Polisi
kutumia nguvu kiasi hicho.
Kitendo cha kuuawa kwa Mwandishi wa
Habari, Daud Mwangosi na tabia ya kutokea mauaji katika mikutano ya
CHADEMA kimeonekana kuwakera viongozi wengi wa vyama vya siasa kwani
wanaamini kuwa Polisi huwa wanatumia nguvu kubwa kupita kiasi
‘wanapotuliza ghasia’ katika mikutano ya CHADEMA.
Katibu wa CCM
Wilaya ya Iringa, Zakaria Mwansasu alielezea sababu ya matukio ya namna
hii kuwa ni kutokana na mmomonyoko aliouita mkubwa wa maadili hasa
katika vyama vya siasa na akashauri viongozi wa vyama vya siasa wakapewa
elimu ya uraia.
Maoni mengi ya viongozi wa vyama vya siasa
yamejikita zaidi katika hofu ya nchi kuingia kwenye vurugu na kutoka
kwenye kisiwa cha amani na hivyo kutoa uashauri kwa viongozi wa vyama
vya siasa na Jeshi la Polisi kuweka mbele maslahi ya taifa.
Mchungaji Yokonia Koko wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), alielezea ukosefu wa maadili kwa baadhi ya askari Polisi kuwa
umetokana na jeshi hilo kuajiri vijana ambao hawana maadili na kwamba
watuhumiwa wa mauaji kwenye matukio yanayolihusisha Jeshi la Polisi
wakati wa kuzuia fujo katika mikutano/maandamano ya vyama vya siasa
wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa askari wengine.
Kasi ya CHADEMA kuendesha mikutano katika sehemu mbalimbali nchini kwa
ajili ya kujiimarisha kichama, imepokewa kwa hisia tofauti na vyama
vingine vya siasa. Wakati kuna makundi ya watu katika jamii wakidhani
kuwa hiyo ni haki yao kama chama cha siasa kinachotaka kukua na
kukubalika kisiasa, wengine wanaiona mikutano hiyo ya hadhara ya CHADEMA
kama ni kuwapunguzia muda wa kufanya shughuli zao za maendeleo hasa
baada ya kipindi cha uchaguzi kumalizika.
Katibu Mkuu wa CCM
Wilson Mukama, alishauri kufanyiwa marekebisho kwenye sheria ya Vyama
vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992 itakayoweka wazi shughuli za vyama vya
siasa baada ya Uchaguzi Mkuu. Alisisitiza kuwa shughuli za siasa baada
ya Uchaguzi Mkuu zihamie bungeni kwa wanasiasa kuhoji mipango ya
maendeleo ya serikali na matumizi ya rasilimali za nchi na wananchi
waachwe wachape kazi zao za maendeleo.
Kuhusu Jeshi la Polisi,
Mukama alisema mfumo uliopo wa Jeshi hilo unalifanya lionekane la
kitaifa zaidi na kushauri libadilishwe kimuundo ili liweze kutandaa hadi
serikali za mitaa kuongeza nguvu katika mpango wa ulinzi shirikishi
ulioanzishwa na Jeshi hilo.
Mwanasiasa John Shibuda
alizungumzia mahusiano kati ya vyama vya siasa na Jeshi la Polisi kwa
kutoa lawama kwa vyama vya siasa kuwa havitoi malezi kwa wanachama wake
ambayo yatawafanya wawe waadilifu, wazalendo, waaminifu na watiifu wa
sheria.
Alisema vyama vya siasa havina mfumo wa kujihakiki,
kujikosoa na kujiwajibisha na akapendekeza kuanzishwa kwa mfumo huo
kisheria ambao utawajibisha vyama vya siasa kwa matendo ya viongozi au
wanachama wao.
Shibuda alifafanua kwamba sheria anayopendekeza
iwe na nguvu ya kutoa adhabu kwa chama cha siasa na kwa kiongozi au
mwanachama ambaye atathibitika kuwa ndiyo chanzo cha uvunjifu wa amani.
Kuhusu Jeshi la Polisi mwanasiasa huyo alipendekeza kufanyike kwa
marekebisho ya utendaji ili wakuu wa wilaya na mikoa waondolewe nguvu za
kiutawala ambazo huwafanya wakati mwingine kutoa maagizo ya kisiasa kwa
Jeshi la Polisi na hatimaye kulifanya Jeshi hilo lionekane linatekeleza
maslahi ya wanasiasa badala ya kuwa chombo cha kulinda amani.
Kwa ujumla Kamati kutokana na maelezo mbalimbali ya Viongozi wa Vyama
vya Siasa na Jeshi la Polisi, imeona kuwa kuna mahusiano hafifu kati ya
baadhi ya Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi.
Kwa kuwa taasisi zote hizi ni wadau muhimu wa amani na utulivu nchini, Kamati inapendekeza:
-Kuwe na jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi
na Vyama vya Siasa ili kila upande ujue wajibu wake na wa taasisi
nyingine katika kudumisha amani ya nchi na utamaduni wa kuheshimu sheria
zilizopo na kupunguza migongano.
-Kuhusu madai kwamba mauaji
yanayotokea nchini yaundiwe Tume, Kamati imeona kuwa zipo sheria
zinazotoa mamlaka ya kutafiti au kuchunguza endapo kuna mashaka ya kifo
hicho.
-Muundo uliopo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya
kisheria ili kuziba mianya inayotoa nafasi kwa wanasiasa kulitumia Jeshi
hilo kwa manufaa ya kisiasa.
-Nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kiutendaji ziangaliwe upya ili zisitumike na mhusika kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.
-Kwa kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwa ndiye mlinzi wa usalama wa
raia na mali zao, siasa za ubabe kwa vyama vya siasa ziepukwe kwa kuwa
zinaleta msuguano usio wa lazima na Jeshi la Polisi
8.0. MAONI NA MAPENDEKEZO:
Kutokana na uchunguzi uliofanyika kupitia mahojiano na Viongozi wa kada
mbalimbali, kuanzia ngazi ya Kijiji, Wilaya, Mkoa hadi Taifa, Kamati
ina maoni na mapendekezo yafuatayo:
MAONI:
-Kuhusu
madai kwamba mauaji yanayotokea nchini yaundiwe tume, Kamati imeona kuwa
zipo sheria zinazotoa mamlaka ya kutafiti au kuchunguza endapo kuna
mashaka ya kifo hicho.
-Nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kiutendaji ziangaliwe upya ili zisitumike na mhusika kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.
-Kwa kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwa ndiye mlinzi wa usalama wa
raia na mali zao, siasa za ubabe kwa vyama vya siasa ziepukwe kwa kuwa
zinaleta msuguano usio wa lazima na Jeshi la Polisi
-Kuhusu
operesheni ya uzuiaji wa mkutano wa CHADEMA usio halali Kijijini Nyololo
tarehe 02 Septemba 2012, Jeshi la Polisi lilitekeleza wajibu wake
ipasavyo na kutumia nguvu sahihi. Operesheni iliyoandaliwa na kufanyika
ilikamilika kwa kuwatawanya watu waliofika kwenye mkutano, kukamata
baadhi ya Viongozi na wafuasi wa CHADEMA na hali ya utulivu ilirejea
kwenye eneo husika.
MAPENDEKEZO
-Mauaji ya mwandishi
wa habari Daud Mwangosi yalitokea baada ya operesheni kumalizika, na
amri ya kuondoka kwa askari eneo la tukio kutolewa na Viongozi wa
operesheni hiyo
-Jamii wakiwemo Viongozi waelimishwe umuhimu wa
utii wa sheria, kanuni na taratibu ili kudumisha amani na utulivu hapa
nchini. Viongozi wengi walionyesha hofu ya kuliingiza Taifa kwenye
machafuko makubwa na uvunjifu wa amani iwapo jamii haitazingatia umuhimu
wa kutii sheria, kanuni, taratibu na amri halali za Mamlaka.
-Msajili wa Vyama vya siasa afafanue majukumu ya vikundi vya Ulinzi vya
Vyama vya Siasa kama vile Green Guard, Red Brigade, Blue Guard.
-Iwepo programu mahususi ya Elimu ya Uraia nchini ili kujenga uzalendo
na kukuza maadili ndani ya jamii wakiwemo viongozi wa kada mbalimbali.
Hivi sasa jamii inashuhudia kutoweka kwa uzalendo na kuwepo kwa
mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii.
Njia zifuatazo zitumike:
- Elimu ya uraia iimarishwe katika mitaala ya elimu kuanzia Shule za msingi hadi Vyuo Vikuu.
- Uamuzi wa kurudisha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana utekelezwe mapema.
- Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Tasnia ya Habari na Taasisi
zisizokuwa za Serikali zishiriki kikamilifu katika uenezi wa Elimu ya
Uraia nchini.
- Kuhimiza uzingatiaji wa weledi katika utendaji
kazi kwa mujibu wa taaluma na miongozo inayotolewa kuleta ufanisi. Aidha
elimu endelevu sehemu za kazi itiliwe mkazo.
-Kufanya
marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya 1992 ili kuweka wazi
shughuli za Vyama vya Siasa baada ya Uchaguzi Mkuu. Lengo ni kuwa
Shughuli za Siasa zihamie Bungeni kujadili na kuhoji mipango ya Serikali
na matumizi ya rasilimali za nchi. Kwa kufanya hivyo wananchi watapata
nafasi kufanya kazi za maendeleo.
-Kuboresha Ofisi ya Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini, hususan uanzishwaji wa ofisi ngazi ya Mkoa na
Wilaya ili kuratibu ushirikiano/mahusiano baina ya serikali (Jeshi la
Polisi) na Vyama vya Siasa. Lengo ni kukuza mahusiano na kuondoa
mgongano.
-Utaratibu wa kufanya mikutano mara kwa mara kati ya
Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa, Jeshi la Polisi na Waandishi wa
Habari uimarishwe ili kujenga mahusiano mazuri na kupata ufumbuzi wa
haraka kwa matatizo yaliyojitokeza.
- Jeshi la Polisi nchini ni
chombo muhimu katika ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Muundo
uliopo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya Kisheria ili kuziba mianya
inayotoa nafasi kwa wanasiasa kulitumia Jeshi hilo kwa manufaa ya
Kisiasa. Aidha mipango ya kuboresha utendaji kazi kitaaluma iliyopo hivi
sasa upewe msukumo stahiki hususan rasilimali watu na fedha.
-
Wananchi wahamasishwe kushirikiana na Polisi Jamii na Ulinzi
shirikishi. Polis ishirikiane na Serikali za mitaa kufanikisha malengo
hayo.
- Jeshi la Polisi liimarishwe ili litekeleze majukumu
yake kikamilifu na kujenga mahusiano sahihi kati yake na Jamii, Vyama
vya Siasa, Tasnia ya Habari na Asasi zisizo za Kiserikali.
-Taasisi za habari zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari,
hususan Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri wafanye
utaratibu unaostahiki wa upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi
la Polisi na uongozi wa mkoa wa Iringa. Hii itasaidia kurejesha uhusiano
mzuri kati ya vyombo hivyo muhimu katika mkoa.
-Waandishi wa habari wapewe mafunzo ya jinsi ya kuripoti matukio ya hatari/ghasia.
-Waandishi wa habari wavae vivazi maalum vya kuwatambulisha wakiwa katika matukio hasa kwenye maeneo hatarishi.
-Waandishi wa habari wafanye kazi kwa weledi, uadilifu, uwazi na wasijibainishe na vyama vya siasa.
-Kamati ya Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari
iliyoanzishwa mwaka 2008 ifufuliwe. Na kamati hizo ziteremke hadi kwenye
ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.
-Viongozi wa Polisi wanapotoa taarifa za tukio, ziwe zimefanyiwa utafiti wa kina ili zisipotoshe jamii.
-Kuwe na jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi
na Vyama vya Siasa ili kila upande ujue wajibu wake na wa taasisi
nyingine katika kudumisha amani ya nchi na utamaduni wa kuheshimu sheria
zilizopo na kupunguza migongano.
9.0. CHANGAMOTO
Changamoto zilizojitokeza katika Uchunguzi zimegawanyika katika mtiririko ufuatao:-
9.1 Jeshi la Polisi:
- Ukosefu wa Mafunzo endelevu.
- Ukosefu wa Uvumilivu katika utekelezaji wa Majukumu.
-Uelewa mdogo wa Elimu ya Uraia.
- Mmomonyoko wa Maadili.
- Kukosekana kwa uzalendo.
- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu
9.2 Vyama vya Siasa:
- Kukosekana kwa uvumilivu katika kuendesha shughuli za Siasa.
-Kukosekana kwa Elimu ya Uraia
- Uelewa mdogo wa baadhi ya Viongozi wa Vyama kuhusu uendeshaji wa Vyama vya Siasa.
- Ukosefu wa Sera/Mwongozo kwa Vyama vya Siasa kuendesha shughuli za Kisiasa baada ya uchaguzi mkuu.
- Kukosekana kwa Jukwaa linalokutanisha mara kwa mara Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi
- Mmomonyoko wa Maadili.
- Suala la Uzalendo.
- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu
9.3 Jamii:
- Elimu ya Uraia.
- Mmomonyoko wa Maadili.
- Kukosekana kwa uzalendo.
- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu.
26
10 HITIMISHO
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake aliwahi
kusema kuwa, “ili nchi iendelee inahitaji vitu vinne ambavyo ni watu,
ardhi, siasa safi na uongozi bora. Watanzania kila mtu mahali pake,
tunahitaji kuwa na siasa safi yenye kujenga ustawi, tija, mshikamano,
amani, maendeleo na afya kwa taifa letu”.
Utulivu na amani kwa
ajili ya mustakabali wa taifa, imekuwa ni kauli mbiu ya viongozi
mbalimbali ambao Kamati hii imepata fursa ya kuzungumzia juu ya hali ya
siasa na mahusiano yaliyopo baina ya Serikali, (Jeshi la Polisi, Kamati
za Ulinzi na Usalama wilaya na mkoa), vyama vya siasa, viongozi wa dini
na wananchi.
Wananchi na Viongozi wanataka kuona shughuli za
siasa ya vyama vingi inaendeshwa kwa hoja zenye tija badala ya vurugu na
utengano. Njia mojawapo ya kukabiliana na hali hii inayojitokeza ni
kujenga uzalendo, maadili mema, na mshikamano ili Tanzania iendelee kuwa
kisiwa cha amani na utulivu.
Kamati hii inashauri na kupendekeza kuwa maoni haya yazingatiwe na kutekelezwa.
Aidha Kamati imefaidika sana kupata fursa ya kukutana na viongozi
mbalimbali kuanzia kijiji hadi taifa na walitoa ushirikiano wa dhati
katika kutoa mchango wao wa mawazo. Kamati inapenda kutoa shukrani za
dhati kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dkt Emmanuel Nchimbi
(Mb) kwa imani yake kwa wajumbe wa Kamati ya Uchuguzi.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin