Habari Mpya

    Loading......

ASKARI POLISI AUA RAIA BUKOMBE

Na Danson Kaijage wa Habarika Blog

JESHI la polisi nchini limeendelea kuandamwa na mzimu wa mauaji ya raia wasiokuwa na hatiai baada askari polisi aliyefahamika kwa jina moja la (Manase) kutuhumiwa kumpiga mwananchi na kusababisha kifo.
Maiti ya Rashid Juma aliyepigwa risasi na askari polisi ikiwa imelazwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Wilaya Bukombe.(Picha na Danson Kaijage)

 Hali hiyo imejitokeza leo Novemba 24 katika kituo cha polisi cha Ushirimbo Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita, ambapo askari polisi amempiga risasi na kumuua kijana ambaye amefahamika kwa jina la Rashid Juma (23).

Tukio la polisi kumuua kijana huyo  limesababisha tafrani kubwa baina ya polisi na wananchi wenye hasira kali ambao wamevamia kituo hicho kwa lengo la kulipiza kisasi kwa kuchoma moto kituo hicho na kutaka askari aliyehusika na mauaji ya kijana huyo naye auwawe.

Hata hivyo askari walilazimika kutumia nguvu nyingi kwa kurusha mabomu ya machozi, risasi za moto na risasi baridi kwa ajili ya kuwatawanya wananchi hao ambao walikuwa wakirusha mawe kwa lengo la kuwajeruhi askari hao na  kuharibu mali za kituo hicho.

Tukio hilo limetokana na askari ambao walikwenda kumkamata mtu ambaye anadaiwa kuwa ni jambazi na aliyesadikiwa kuwa alikuwa amejificha katika nyumba ambayo ipo katika mtaa wa Kilimahewa mjini Ushirombo,
ambapo askari hao walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na kumweka ndani ya gari. 

Baadhi ya wananchi wameonekana kulizingira gari hilo huku wakitaka mtuhumiwa huyo atolewe kwenye gari ili auwawe.

Katika kukabiliana na hali hiyo askari wamelazimika kufyatua risasi juu kwa lengo la kuwatawanya wananchi na ndipo askari mmoja alipomlenga kijana huyo risasi ya kiunoni na kijana huyo kupoteza maisha hapo hapo.

Baada ya kuzuka kwa ghasia hizo za wananchi kutaka kuchoma kituo, mbunge wa Bukombe, Peofesa Kulikoyela Kahigi(Chadema) akiwa ameambatana na Diwani wa kata ya Igulwa, Soud Ntanyagalla (Chadema)walituliza ghasia hizo kwa kuwasii ndugu wa marehemu paomaja na mama yake mzazi Justina Fransis kwa madai kuwa watashughulikia suala hilo.


 Mbunge wa Bukombe Profesa, Kulikoyela Kahigi Chadema akipokea maelezo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe Dk. Archard Rwezahura, aliyevaa shati la kitenge jinsi alivyopokea maiti ya kijana huyo ambaye alipigwa risasi na Polisi na kufikishwa hospitali hapo akiwa amefariki.(Picha na Danson Kaijage )

Mbunge pamoja na Diwani walimtaka mkuu wa Polisi Wilaya kuambatana naye hadi kwenye hospitali ya Wilaya ili kujilidhisha kama kijana huyo ambaye alipigwa risasi kama amefariki ama yuko mahututi.

Viongozi hao walitaka kufika hospitalini hapo kutokana na Mkuu wa Polisi kudai kuwa kijana huyo yupo hai na anaendelea na matibabu.

Hata hivyo baada mbunge na diwani kufika katika hospitali ya Wilaya ya Bukombe, Mganga Mkuu wa Wilaya Dk.Archard Rwezahura alithibitisha kuwa kijana huyo ambaye alipigwa risasi na polisi alifia mikononi mwa polisi na wala siyo hospitalini kama ilivyokuwa ikidaiwa na jeshi la polisi.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC) Lenard Paul alipoulizwa juu ya tukio hilo alikiri kupata taarifa ya kijana huyo kupigwa risasi na kufa,akaahaidi kuwa  hatua za kisheria zitachukuliwa kwa askari aliyehusika.

Kwa upande wa viongozi kwa maana ya Mbunge na Diwani wamewaahidi wananchi kuwa watashughulikia suala hilo na wamelitaka jeshi la polisi lichukue hatua za kisheria kwa askari huyo.
Msafara wa Mbunge, wa Bukombe, Profesa Kulikoyela Kahigi Pamoja na Diwani na baadhi ya askari na wananchi wakiwa wanaongozana kwenda katika hospitali ya Wilaya ya Bukombe kwa ajili ya kuangalia mwili wa marehemu Rashid Juma aliyepigwa risasi na polisi na kufa hapo hapo. (Picha na Danson Kaijage.)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com