Ukisoma mabango haya niliyokuwekea kwenye ukurasa huu leo, hutapata
shida kutambua kuwa matatizo mengi ya Watanzania, si tu kwamba
yanasababishwa na wanasiasa.
Ndiyo maana nimejiepusha kujadili Mkutano Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na uteuzi wa viongozi wapya wa Sekretarieti ya chama
hicho. Kwa ufupi ni kwamba matatizo ya Tanzania na Watanzania ni zaidi
ya siasa na wanasiasa.
Ukisoma ujumbe ulio kwenye mabango haya unauona upumbavu
unavyotamalaki katika jamii yetu. Bahati nzuri kwa wanaosambaza
upumbavu huo ni kwamba wapo wanaouamini, na kwa sabahu hiyo wamewafanya
matapeli hawa waendelee kuwapo na wengine wazidi kuibuka kila uchao.
Kwanza, nisema kwamba tatizo la imani za kishirikina na ujinga wa
kuamini ndumba vimeenea sehemu nyingi duniani. Masuala hayo yapo pia
Ulaya, Marekani na Asia. Tofauti iliyopo ni viwango na aina za uongo;
pamoja na idadi ya watu walio wafuasi wa mambo hayo.
Hapa kwetu hali ni mbaya. Mauaji ya albino ni aina ya ujinga huo.
Dunia ya leo bado kuna watu wanaamini kuwa kiungo cha albino kinaweza
kuwatajirisha.
Pamoja na ukweli kwamba Katiba yetu imewapa wananchi uhuru wa
kuabudu (kuamini?), kuna mambo tunayopaswa kuyahoji. Upuuzi huu
unafanywa mbele ya Serikali ilhali ikitambua kuwa wanaoendesha mambo
haya ni waongo, matapeli, majizi na watu waliodhamiria kuviza akili na
maendeleo ya Watanzania.
Wapuuzi hawa walianza kujitangaza kwa majina na mahali wanakoishi.
Maendeleo ya teknolojia yamewawezesha kumiliki simu. Matangazo yao
yanapambwa kwenye kila kona hapa nchini. Haitashangaza kuyaona kwenye
ukuta wa Ikulu!
Walianza kudanganya kuwa wanatibu Ukimwi. Serikali haikuchukua hatua
madhubuti kukanusha upuuzi huo. Wananchi wenyewe hawakuamini kuwa huo
ni uongo. Hatua hiyo haijawakatisha tamaa, maana wateja wapo japo ni
wachache.
Sasa wameibuka na mambo mengine hatari. Wapo wanaojitangaza kwamba
wana uwezo wa dawa wa kumfanya mwanafunzi afaulu mitihani! Wamelenga
kuwapata wanafunzi wa shule za msingi, vyuo na sekondari.
Kwa maneno mengine ni kwamba mwanafunzi asisome kwa bidii. Atulie
tu, siku ya mtihani atashinda kwa sababu dawa ya kumwezesha kushinda
imeshapatikana! Ujinga huu unapatikana Tanzania, na pengine Afrika
pekee!
Wameibuka wengine wanaeneza ujinga kwamba wana uwezo wa kumfanya mtu
apandishwe cheo kazini! Huu ni upumbavu wa hali ya juu. Kama kweli dawa
hizo zipo, basi jeshini wote wangekuwa majenerali! Kusingekuwapo koplo
wala sajini!
Kama kweli kuna dawa ya vyeo, basi nchi hii kila mtu angekuwa
mkurugenzi, au waziri, au katibu mkuu, au rais! Badala ya watu kufanya
kazi kwa weledi na juhudi, wanaaminishwa kwamba dawa zitawawezesha
kupata vyeo vya juu! Ujinga mtupu.
Wapo wanaojitanabaisha kuwa na dawa za kurejesha mali zilizoibwa. Huu
nao ni uongo tu. Kama hivyo ndivyo, kwanini hawajajitokeza kumsaidia
Zitto Kabwe ili mabilioni yaliyofichwa ughaibuni yarejeshwe? Kwanini
Serikali itumie gharama kubwa kuendesha kesi za ufisadi ilhali kuna
“wataalamu” inaoweza kuwatumia kurejesha fedha hizo?
Wapuuzi hawa wanajigamba kutibu kisukari, wakati wanatambua kuwa
hakuna dawa ya kutibu maradhi hayo. Kama ipo, wanasubiri nini kuisambaza
duniani ambako matajiri wengi wanasumbuliwa na maradhi hayo?
Wengine wanasema wana dawa za mapenzi kiasi kwamba kama mwanamme
akimtaka mwanamke, atampata! Au mwanamke akimtaka mwanamme, atampata!
Huu ni uongo mwingine. Kuna binti gani wa Kitanzania asiyependa kuolewa
katika ukoo wa kifalme?
Mbona hatujasikia kina Prince Charles kutoka ughaibuni wakifika hapa
nchini kwa mvuto wa dawa hizo kuleta posa kwa mabinti zetu? Mbona
hatujasikia kijana mvulana wa Kitanzania kaenda kuoa katika ukoo wa
mfalme Hirohito au Akihito huko Japan?
Tunahangaika na dawa za kuongeza nguvu za kiume, dawa za kufauli
mitihani, dawa za mvuto wa biashara na ujinga mwingi; huku tukiwaacha
wazungu, wahindi na waarabu wakijitwalia malefu ya ekari za ardhi yetu.
Tufanye nini? Upuuzi huu lazima tuhakikishe unakomeshwa katika jamii
yetu. Kazi ya kuukomesha imerahisishwa na matapeli hao wenyewe kwa
kuweka namba za simu kwenye mabango yao. Serikali za Mitaa hazipaswi
kufumbia macho ujinga huu.
Matangazo haya yanaifanya jamii ya Watanzania ikose weledi wa
kupambana na maisha kwa njia za kisayansi. Yanawafanya wananchi wengi
waamini kuwa unaweza kusafishwa nyota kisha ukaamka ukiwa tajiri! Hizi
ni athari za kupenda njia za mkato. Watanzania tunapenda sana mkato.
Matangazo haya ni wizi wa fedha kutoka kwa watu wenye uelewa mdogo,
na hasa kutokana na uhaba wa elimu na umasikini. Matangazo haya
yanakifanya kizazi chetu kiwe cha mbumbumbu wanaoamini katika
mitishamba, miujiza, ngekewa; na si katika kujisomea au kufanya kazi
kwa juhudi na maarifa.
Imani hizi zinatufanya tusiwe na utashi wa kujenga mabweni, maabara
wala nyumba za walimu au hata kuweka madawati katika shule zetu!
Hatufanyi kazi hizo kwa sababu tumeaminishwa na wapuuzi hawa kwamba
hata bila maabara, vitabu, vyumba bora vya madarasa, nyumba za walimu
na walimu waliohitimu vizuri, bado tutashinda mitihani na mwisho
tutayashinda maisha!
Matapeli hawa wanawaumiza wananchi kiuchumi. Serikali nayo imebariki
wananchi wake waumizwe. Fedha ambazo wananchi wanahangaika kuzipata,
wanazipeleka kwa watu hawa kwa matarajio ya kufanikiwa zaidi. Huu ni
wizi. Matapeli hawa wanapaswa kushitakiwa kwa makosa ya wizi na
ulaghai.
Haya niliyoyasema kwa matapeli hawa wa mitaani, nayasema pia kwa
matapeli wa makanisani. Huko nako tunaaminishwa kuwa kusali pekee
kunaweza kubadili maisha yetu. Tunadanganywa. Kumeanzishwa redio eti za
kuendesha maombi kwa sadaka zinazopelekwa kwa njia ya Tigo-Pesa,
M-Pesa, na kadhalika. Wizi tu.
Jamii iungane kutokomeza imani hizi za kipuuzi. Tufanye hivyo kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu.
source;rizikimgaya blog
Social Plugin