WAKATI nchi ya Malawi ikiendelea kushikilia msimamo wake, kuwa
halali ya mpaka Mashariki mwa ziwa Nyasa kati yake na Tanzania unatenganishwa
na ardhi ya Tanzania, Wazee wilayani Kyela, wametoboa siri na kuweka hadharani
ukweli wake.
Wazee wengi waliotoa ushahidi juu ya ukweli wa mpaka kati ya
Tanzania na Malawi ndani ya ziwa nyasa, mbele ya msafara wa ziara ya siku moja
ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe ni wale
waishio kando kando ya ziwa hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mstaafu, John Mwakipesile (70), ambaye katika
maelezo yake akiwa wa kwanza, alisema anashangazwa na madai hayo mapya ya
Malawi kuwa Ziwa lote ni miliki yao.
Alisema kitendo hicho cha nchi hiyo kukurupuka kinapaswa
kuupuzwa kwa kuwa jambo hilo halina ukweli na linapingana na historia na
desturi za kweli za maisha ya kawaida ya wananchi wa mpakani wa mataifa haya
toka enzi za ukoloni.
Alisema madai ya Malawi hayajazingatia historia ya kweli ya ziwa
hilo kwani madai yao yote ni kujaribu kuficha ukweli kwa kuwa yeye kama kizazi
cha tatu hata siku moja hakuwahi kusikia kuwa ziwa lote ni mali ya nchi hiyo.
Alisema kuna ushahidi wa kutosha juu ya Tanzania kuwa miongoni
mwa wamiliki wa ziwa hilo, kwani kuna mali za watanzania ikiwemo Makaburi
yamepotelea ndani ya ziwa hilo baada ya kumezwa.
Alitolea mfano shule ya Msingi aliyesoma katika mwaka 1945 kuwa
ilishamezwa na ziwa hilo, yakiwemo majengo ya baraza (Mahakama) katika kijiji
alichozaliwa cha Mwaya katika wilayani humo.
“Mimi kwa umri wangu wa miaka 70 ni kizazi cha tatu katika
Wilaya hii nakumbuka shule niliyosoma mwaka 1945 pale Mwaya nilipozaliwa
ilishamezwa na Ziwa na ni umbali wa kilomita mbili toka pwani ya sasa kijijini
hapo” alifafanua Mwakipesile.
Naye Maini Mwakisambwe(83), Mkazi wa kata ya Katumba songwe,
alisema tangu azaliwa alikuwa akijua mpaka ni Mto Songwe ambao unaingiza maji
ndani ya ziwa hilo na ndio uliotumika kama mpaka wa kuligawa ziwa klwa mataifa
haya mawili.
Mbali na hilo, lakini pia wakiwa vijana walishuhudia viongozi wa
serikali zote mbili wakiheshimu mpaka huo ndani ya ziwa , kwa kuwa hata
waliposafiri toka upande mmoja kwenda mwingine kila wakifika eneo la Mto Songwe
bendera ya uapane mmoja ilishushwa na kupandishwa ya upande mwingine.
Philipo Mwandemele(73) kabla ya kuanza kutoa maelezo yake alitoa
kitabu kimoja kinachozungumzia maisha na desturi za wakazi wan chi hizi mbili
kama nyaraka muhimu inayoweza kutumika kueleza ukweli juu ya sakata hilo la
mpaka.
Katika kitabu hicho kilichoandikwa na mmishenari kutoka nchini
Ujerumani Teodoro Mayers , anayedaiwa kufika wilayani humo kwa lengo la kueneza
dini , katika ukurasa wake wa 31 kinathibitisha kuwa mwaka 1891 kulikuwa na
mapatano kati ya Ujeruman na Uingereza kuwa mpaka wa Tanzania na Malawi ndani
ya ziwa unaanzia pale Mto Songwe unamwaga maji ndani ya ziwa hilo.
Kutokana umuhimu wa kitabu hicho chenye jina la Wakonde, mila na
Desturi za Wanyakyusa, Waziri wa Mambo ya Nje Membe alimuomba kuiazima serikali
kwa muda ili kikarudufiwe na baadae kurejeshewa kwa lengo la kupata ushahidi
sahihi.
Waziri Membe akihitimisha ziara hiyo alisema licha ya nchi ya
Malawi kuonekana kusuasua katika vikao, kamwe Tanzania haitarudi nyuma
kushughulikia mgogoro huo na kwamba hadi kufikia mwaka 2015 suala hilo litakuwa
limepatiwa ufumbuzi.
Aliongeza kuwa maelezo na ushahidi huo uliokusanywa kwa wakazi
wa wilaya ya Kyela utatumiwa na serikali katika Mahakama ya kimataifa ya
Usuluhishi ya (ICJ), kama suluhu ya mashauriano ya pande mbili yatashindikana.
Katika mazungumzo juu ya mgogoro wa mpaka katika ziwa Nyasa
yaliyofanyika Agosti mwaka huu nchini Malawi, Waziri wa Mambo ya nje na
Ushirikiano wa kimataifa wan chi hiyo Epraim Chiume, akihitimisha maelezo yake
alisisitiza kuwa licha mgogoro huo kuhitaji busara zaidi , serikali yake
inaamini kuwa mpaka kati ya nchi hizo upande wa mashariki mwa ziwa Nyasa
unatenganishwa na ardhi ya Tanzania.
Kwahisani ya Moshi Mathias,Kyela.
|
Social Plugin