Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHILINGI BILIONI 86 ZAIBWA WIZARA YA NISHATI



Gazeti la The East African la Novemba 24 – 30, 2012 limetoa taarifa kwamba jumla ya dola za kimarekani milioni 54 zimegundulika kuibwa na watumishi waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la TANESCO kupitia manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mtambo wa Umeme wa IPTL.

Gazeti hili limenukuu taarifa ya ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Tanzania (Controller and Auditor General). Taarifa hiyo inasema kuna kikundi (racket) ambacho kazi yake kubwa ni kujifaidisha binafsi na mpango wa umeme wa dharura kupitia manunuzi ya Mafuta mazito ya IPTL.

Itakumbukwa kwamba toka mwaka 2011 kumekuwa na shinikizo lililotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba zabuni za ununuzi wa mafuta ya kuendesha mpango wa umeme wa dharura na mchakato mzima wa manunuzi ya mafuta haya ufanyiwe uchunguzi wa kina (forensic audit).

Katika mkutano wa 3 wa Bunge la Kumi (April 2011) niliuliza swali Bungeni kuhusu kashfa hii ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mtambo wa IPTL na baadaye tarehe 16 Aprili 2011 nilimwomba Spika airuhusu Kamati ya Nishati na Madini kufanya uchunguzi kuhusu kashfa hii. 

Kamati ya Nishati na Madini chini ya aliyekuwa Mwenyekiti ndugu January Makamba ililitaka Bunge kuazimia kufanyika kwa uchunguzi kuhusu suala hili kwenye Taarifa yake ya mwaka 2011 iliyowasilishwa Bungeni mwezi Aprili mwaka 2012. 

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ndugu John Mnyika katika Hotuba yake ya Bajeti ya Wizara hiyo mwaka 2011 alipendekeza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu kashfa hii pia. Juhudi zote hizo hazikuzaa matunda.


Kipindi hicho kiwango kilichokuwa kinahojiwa kuibwa ni shilingi bilioni 15 tu. Taarifa ya The East African kama walivyonukuu kutoka kwenye taarifa ya CAG inaonyesha fedha zilizoibwa ni shilingi bilioni 86.

Zabuni za kununua mafuta ya kuendesha umeme wa dharura zimekuwa zikitolewa bila kufuata utaratibu wa zabuni kwa mujibu wa Sheria ya manunuzi. Hivi sasa kila mwezi Tanzania inatumia dola milioni 70 kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme. 

Fedha hizi zinatoka Hazina na sehemu ndogo kutoka TANESCO. Wakati fedha hizi bilioni 112 zinachomwa kila mwezi kununua mafuta mazito na dizeli ya kuendesha mitambo ya umeme, Taarifa za kitaalamu zinaonyesha kwamba Bwawa la Mtera hivi lina kina cha maji chini ya kiwango kinachotakiwa na uzalishaji wa umeme ni asilimia 20 tu ya uwezo (installed capacity).

Iwapo TANESCO wataendelea kutumia zaidi maji yaliyopo Mtera, Mitambo itashindwa kazi na Gridi nzima itasimama maana Mtera ndio nguzo kuu ya Gridi ya Taifa. Hali hii ni hatari sana kwa uchumi na ulinzi na usalama wa Taifa. Kimsingi Gridi ya Taifa ipo hatarini kutokana na kiwango cha Maji kilichopo Mtera hivi sasa na kuendelea kupungua kwa kina hicho cha maji.

Wananchi wanapaswa kuelezwa kinaga ubaga nini kinaendelea katika sekta ndogo ya umeme hapa nchini;

1.      Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuhusu zabuni za manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa dharura iwekwe wazi na ‘racket’ inayosemekana kuiba jumla ya shilingi bilioni 86 ionyeshwe na hatua za kisheria zichukuliwe mara moja na bila kuchelewa.

2.      Waziri wa Nishati na Maadini auleze umma hali yalisi ya sekta ya umeme nchini, uzalishaji wa umeme upoje, hali ya maji katika bwawa mkakati la Mtera na nini hatma ya mitambo ya IPTL, kesi zake na utekelezaji wa mapendekezo ya Bunge kuwa kesi za kampuni hii zimalizwe nje ya mahakama. Pia Taifa lielezwe Mpango wa Dharura wa umeme unakwisha lini maana muda uliotolewa na Bunge mwezi Agosti mwaka 2011 tayari umekamilika. Waziri aeleze hatua agni amechukua baada ya kukabidhiwa taarifa na CAG kuhusu maafisa waandamizi wa Wizara waliohusika na wizi wa shilingi bilioni 86 za kununua mafuta ya IPTL.

3.      Waziri wa Fedha na Uchumi aueleze umma ni kiwango gani cha fedha Hazina imetoa kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa dharura kati ya Mwezi Novemba mwaka 2011 na Oktoba mwaka 2012 na kama taratibu zote za zabuni zilifuatwa na pale ambapo hazikufuatwa ni hatua gani PPRA wamechukua dhidi ya waliokiuka sheria ya manunuzi na kuleta hasara ya mabilioni ya fedha kwa Serikali.

Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha
Dar es Salaam. Novemba 25, 2012

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com