Dereva
Mwanamke wa Basi la la Shabiby, Nusra Maguluko, akizungumza wakati
alipoalikwa mbele ya viongozi kutoa ushuhuda kuhusiana na kazi yake ya
Udereva wa magari makubwa kama Mwanamke, wakati wa hafla ya uzinduzi wa
Jengo la Kampuni ya usafirishaji ya DHL, iliyofanyika siku za hivi
karibuni jijini Dar es Salaam. Nusra alialikwa katika hafla hiyo baada
ya kuwa ni mmoja kati ya wanawake waliopata tuzo za Usafirishaji kutoka
kampuni hiyo ya DHL.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bila,
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Mkurugenzi wa DHL na Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano
Zanzibar, Rashid Seif Suleiman, wakiwa katika picha ya pamoja na Nusra
Maguluko, wakati wa hafla ya uzinduzi wa jingo la DHL, hivi karibuni.
KUTANA NA NUSRA MAGULUKO (28) MWANAMKE JASIRI ANAYEENDESHA BASI LA SHABIBY, DAR-DOM
Na www.sufianimafoto.blogspot.com
NUSRA
Maguluko (28) ni msichana jasiri na anayependa kujaribu na kupata
mafanikio ya majaribio yake bila woga wala kujali ni aina gani ya kazi
anayotakiwa kufanya yeye kama mwanamke na ipi asiyostahili kufanya yeye
kama mwanamke.
Ni
ujasiri wake hasa ndiyo ulimuwezesha kumfikisha hatua aliyonayo kwa
sasa, ambaye ni miongoni mwa wanawake wachache na hasa kwa Tanzania
waliopata kuifikia na kujiamini hadi kuwa na ujasiri wa kubeba roho za
watu zisizopungua 40 kila safari moja ya kwenda Dodoma ama kotoka Dodoma
kuja Dar.
Nusra
ni mzaliwa wa Mkoa wa Manyara katika wilaya ya Kiketo, na ni mtoto wa
nne kuzaliwa kati ya 12 wa familia ya baba yake mzazi mzee, Maguluko na
Elimu yake ni Kidato cha pili tu.
Alimaliza
elimu ya Msingi mwaka 1997, katika Shule ya Msingi Matui iliyoko
Wilayani Kiteto, baada ya kuhitimu elimu ya msingi alijiunga na elimu ya
Sekondari ambayo kwa bahati mbaya hakuweza kumaliza na kuishia Kidato
cha pili baada ya kusumbuliwa na maumivu ya kichwa mara kwa mara.
Nusra,
alishauriwa na madaktari kupumzika kwa muda wa miaka mitatu bila kusoma
ama kuwa akiangalia karatasi nyeupe mara kwa mara, jambo ambalo
lilimfanya kuamua kumsumbua Baba yake mkubwa, Hamis Mang'endi aliyekuwa
ni fundi wa magari ili amfundishe ufundi na udereva wa gari.
Baada
ya kumsumbua sana baba yake mkubwa, kwa kuwa akiripoti katika gereji
yake kila asubuhi na kushinda hapo huku akimfuatilia kila analofanya
katika magari, Mzee Hamis, baada ya kuona kuwa Nusra alikuwa na moyo wa
kweli wa kujifunza ufundi, aliamua kuanza kumfundisha ufundi hatua kwa
hatua.
Baada
ya kumudu kidogo kishika Spana, Mzee Hamis, mwaka 1998, alianza
kumfundisha udereva, tena kwa kumfundishia katika gari aina ya Comb Volkswagen, ambapo baada ya miezi sita tu Nusra tayari alishamudu kuendesha gari na kutulia barabani.
Nusra
alipomudu kufanya vurugu za barabarani, alikabidhiwa na baba yake
mzazi, Canter ya Tani 3 na robo ili aweze kufanyia kazi ya kubebea
mizigo, huku akikodishwa ambapo alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka
miwili.
Hatimaye
mwaka 2001, Nusra, aliamua kuachana na kazi ya kuendesha Canter ya
kubeba mizigo na kuamua kuanza kazi ya kulima kwa Treka, ambapo alikuwa
akikodishwa na wakulima na alimudua kulima hadi Heka 10 kwa siku kwa
ujira wa Sh. 10, 000 kwa kila heka moja.
Mwaka
2003, Nusra alianza kuendesha Min Bus, huku akiwa na Leseni ya Clac C
baada ya wakati huo kudanganya umri ili aweze kupata uhalali ya kufanya
kazi anayoipenda ya udereva.
Alifanya
kazi hiyo ya kutoa huduma usafiri kwa abiria kutoka Wilaya ya Kiteto
kwenda Vijijini hadi mwaka 2006, alipokabidhiwa Basi aina ya Fuso lenye
uwezo wa kubeba abiria 40, nakutoa huduma hiyo ya usafirishaji wa abiria
kutoka Wilaya ya Kiteto hadi Dodoma, kazi aliyoifanya hadi mwaka 2011.
Baada
ya kuchoshwa na njia za Vijijini na kile alichodai kuaua kutafuta
maslahi zaidi, Nusra, aliamua kuvaa, Mbunge wa Gairo, he Shabiby, na
kumuomba kazi jambo ambalo lilimshangaza na kumuhoji kama anaweza kweli
kuendesha gari kubwa tena la abiria.
''Baada
ya kuniuliza swali hilo, mimi nilimjibu Mheshimiwa samahani wewe
nisaidie unipe kazi, halafu ndiyo utaniona nikiwa kazini kama naweza ama
siwezi, kwani najiamini na ndiyo maana nimekuja kwako''. alisimulia
Nusra
Baada
ya maongezi marefu ya maswali na majibu juu ya ujasiri wa Binti huyo,
aliyeonekana mdogo akiwa na maelezo ya mambo makubwa, Mhe. Shabiby,
aliamua kumwajiri, Nusra ambapo hadi sasa anapiga mzigo katika kampuni
hiyo ya Shabiby, akiburuza Basi linalofanya safari zake Dar-Dom.
Hivi
Sasa Binti huyo, anandoto za kufungua Chuo cha Mafunzo ya Udereva kwa
wanawake, akiwa na lengo la kuwafikisha mbali wanawake wenzake ili
waweze kuwa na ujasiri wa kuendesha magari makubwa na si gari ndogo
pekee.
Kwa
hatua hiyo sasa Nusra, ameanza kusaka wafadhili, ili aweze kutimiza
ndoto zake hizo, ambapo amewamba wadau mbalimbali pamoja na Serikali
kujitokeza kumsapoti, ili kufanikisha kufungua chuo hicho chenye lengo la kuwainua Kinamama.
Social Plugin