Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Padri ashambuliwa kwa risasi Zanzibar


PADRI Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki, Mjini Zanzibar amepigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake juzi saa 1:45 jioni wakati akitokea kanisani.
Hili ni tukio la kwanza katika historia ya Zanzibar kwa kiongozi wa kanisa kushambuliwa wakati wa Krismasi, lakini ni tukio la pili kwa kiongozi wa dini kushambuliwa mwaka huu.
Hivi karibuni, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga alimwagiwa tindikali iliyomjeruhi vibaya usoni na kifuani na watu wasiojulikana. Shambulio hilo lilimlazimu kiongozi huyo kwenda kutibiwa India ambako ameambiwa anapaswa kuripoti hospitalini kila baada ya miezi sita.

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Mkenda ambaye ni Paroko wa Parokia ya Mpendae, alipigwa risasi begani na shingoni na afya yake si nzuri.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed alisema jana kuwa majeraha hayo yamemsababishia kutokwa na damu nyingi.

Alisema baada ya shambulio hilo, Padri Mkenda alipelekwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Zanzibar. Hata hivyo, padri huyo alisafirishwa kwa ndege jana hadi Dar es Salaam ambako amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kamanda Aziz alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, lakini akabainisha kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa alipigwa risasi baada ya watu hao kumshuku kuwa alikuwa na fedha za sadaka.

“Father Mkenda kitaaluma ni mhasibu na amekuwa akishika makusanyo ya fedha pale kanisani. Sasa huenda wahalifu hao waliona amechukua fedha na ndipo walipomfuata na kumpiga. Lakini hata hivyo, huo bado ni uchunguzi wa awali tu,” alisema Kamanda Aziz na kuongeza:

“Waliofanya tukio hili wamelifanya kwa madhumuni gani, ni swali gumu kujua sasa. Inawezekana kuna mambo mengine zaidi ya watu hao kutafuta fedha. Uchunguzi ukimalizika tutajua cha kufanya.”

Kamanda Aziz alisema walipata taarifa za tukio hilo saa 2:00 usiku na polisi walikwenda katika eneo hilo la Francis Maria anakoishi Padri Mkenda.

“Tulipofika tukakuta maganda mawili ya risasi za bastola na upande wa kulia wa kioo cha gari yake (padri) kuna damu katika viti vyake,” alisema Kamanda Aziz.

Alisema baadaye padri huyo alipelekwa hospitalini kwa ajili matibabu ambako madaktari walifanikiwa kumtoa mabaki ya risasi mwilini kabla ya jana kupelekwa Muhimbili.

“Tumempokea padri huyo saa 4:20 asubuhi leo (jana). Tulianza kumchunguza afya yake, baadaye kumfanyia uchunguzi kisha kumchukua kipimo cha CT Scan ili kubaini ilipo risasi hiyo,” alisema, mkurugenzi wa zamu katika hospitali hiyo, Agnes Mtawa.

 Akizungumzia tukio hilo, Askofu Mkuu Msaidizi, Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa alisema kanisa linasikitishwa na kilichotokea kwani ni kitu ambacho jamii haikukitarajia na wanaviachia vyombo vya usalama vifanye kazi yake... “Sisi kama kanisa tunajitahidi kuhakikisha anapata matibabu yaliyo bora ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida.”

Askofu huyo alisema viongozi wa dini wanachukua tahadhari kujilinda ingawa wanafahamu kuwa wahalifu hao nao wanajipanga kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Kwa upande wake, Askofu Michael Hafidh wa Kanisa la Anglikana la Mkunazini, Zanzibar alisema: “Tukio hililimenisikitisha sana.” Alisema amepokea taarifa hizo kwa mshtuko mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa tukio hilo ni mwendelezo wa mengine kadhaa ya kuwahujumu viongozi wa dini, Zanzibar.
Alisema tukio hilo ni miongoni mwa matukio ya kushtusha na yanayoashiria hali mbaya ya kiusalama katika Mji wa Zanzibar na kuwaomba viongozi wa Serikali kuchukua hatua za tahadhari haraka kunusuru hali hiyo.

“Ni busara Serikali ikachukua hatua sasa kwani hili siyo tukio la kwanza kuwahujumu viongozi wa dini. Katibu wa Mufti Zanzibar Sheikh Soraga aliwahi kukumbwa na mkasa wa aina hiyo pia,” alisema na kuongeza:

“Hii ni hali ya hatari katika nchi yetu na haipendezi kabisa kwa sababu inaashiria na kutishia usalama wa nchi. Sisi hatujawahi kushuhudia kitu kama hiki. Tumezoea Wazanzibari kusherehekea sikukuu kwa pamoja miaka yote. Krismasi tunasherehekea na wenzetu Waislamu na Idd El Haj tunasherehekea kwa pamoja bila ya tofauti za kidini sasa hili linatokea wapi sasa!”

Askofu Hafidh alisema kibaya zaidi ni tukio la Padri Mkenda kutokea katika kipindi ambacho kumekuwa na vipeperushi vilivyosambazwa na watu vikiwatisha watu wenye imani ya Kikristo.

“Tumeona hivi vipeperushi na kwa kweli tulikuwa na hofu, lakini ndiyo tunasema tunaelekea wapi katika maisha haya Zanzibar?” alihoji Askofu Hafidh.
Akizungumzia vipeperushi hivyo, Kamanda Azizi alisema jeshi lake halijaviona wala kuona mtu akivilalamikia na siku zote limekuwa likiimarisha ulinzi katika makanisa na misikiti siku za sherehe za kidini.

“Hakuna hata kanisa moja ambalo hatujaliwekea ulinzi wa kutosha. Tumejitahidi sana na pia kuna askari wetu wanaozunguka kuimarisha ulinzi kwa miguu na wengine wanazunguka kwa pikipiki katika maeneo yote. Sasa tunawaomba wananchi wasaidie kutoa taarifa wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani kwa sababu polisi hawawezi kumlinda mtu mmoja mmoja,” alisema.

Kuhusu uchochezi wa kidini, Kamanda Aziz alisema Jeshi la Polisi haliamini kwamba kuna uchochezi wa kidini... “Sisi hatuamini kwamba kuna kisasi kwa viongozi wa dini, tunachukulia hilo ni tukio la kihalifu.”

Msemaji wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shaaban Simba alisema ingawa hajapata habari hizo kwa undani kwa kuwa yupo safarini, wanalilaani tukio hilo na kusema kuwa vyombo vya dola vitachukua hatua stahiki.


source:mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com