KONDOMU zinazodaiwa kuwa ni bandia ambazo zilipigwa marufuku nchini
Uingereza kutokana na kubainika kuwa hazina ubora unaotakiwa,
zimetapakaa katika maduka mbalimbali ya dawa nchini.
Kondomu hizo ni Durex na Trojan ambazo zina vipele na imebainika kuwa zinauzwa katika maduka
mbalimbali ya dawa kwa bei ya Sh5,000.
Mwishoni mwa mwaka jana, Serikali ya Uingereza ilifanya msako mkali kwa
lengo la kukamata mamilioni ya kondomu hizo, wakati ambao ilikuwa
imepita takriban miezi 18 tangu zilipokuwa zimeingizwa nchini humo.
Mdhibiti wa Dawa na Bidhaa za Afya wa Uingereza alinukuliwa akisema kuwa
mamilioni ya kondomu hizo feki ziliingizwa kutokea Mashariki ya Mbali
na kwamba tayari zilikuwa zimetumiwa na idadi kubwa ya watu.
Kondomu hizo zinadaiwa kutokuwa na ubora hali inayoweza kuongeza hatari
kwa watumiaji kwa kusambaza kwa kasi magonjwa ya zinaa, virusi vya
Ukimwi au kusababisha mimba zisizohitajika, hivyo kuharibu mikakati ya
uzazi wa mpango.
Ofisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia
Simwanza akizungumza na gazeti hili jana, alithibitisha kuwapo kwa
taarifa za kondomu hizo za Durex na Trojan na kuongeza kuwa mamlaka hiyo
imewaagiza wakaguzi wake kuzichunguza ili kubaini kama zina ubora ama
la. “Wakaguzi walichukua sampuli ya kondomu hizo kwa lengo la
kuzichunguza, nipe muda kidogo ili nizungumze na mkurugenzi ili kujua
uchunguzi ule umefikia wapi,” alisema Simwanza.
Alipotafutwa baadaye alibainisha kwamba uchunguzi wa sampuli hiyo bado
upo maabara na kwamba majibu yake hayajatoka. Hata hivyo hakusema ni
lini yatatolewa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania
(TBS), Leandri Kinabo aliomba apewe muda ili afuatilie kujua ni kondomu
za aina gani zilizowahi kukamatwa na kupigwa marufuku zisitumike.
“Nipe muda kidogo nifuatilie ili kujua zilizopigwa marufuku na ambazo
tulizizuia kuingizwa nchini, nitafute mchana,” alisema Kinabo ambaye
alipotafutwa baadaye alisema yuko kwenye kikao na kwamba alikuwa
hajaweza kuwasiliana na watu wa maabara.
Hii siyo mara ya kwanza kuibuliwa kwa taarifa za kuwapo kwa kondomu feki
nchini, kwani Desemba 20, mwaka jana kontena lililosheheni kondomu za
kiume aina ya Melt Me kutoka nchini India lilikamatwa na kuzuiwa katika
Bandari ya Dar es Salaam, baada ya kubainika kuwa hazifai kwa matumizi.
Maofisa wa TBS walilazimika kufanya msako katika baadhi ya maduka ya
dawa jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua ya kuziondoa kondomu hizo
katika soko.
Source: Mwananchi
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin