WANAUME wanaotumia muda wa saa tatu na zaidi kwa siku kutazama
runinga wanapoteza nguvu za kiume ukilinganisha na wale wanaotazama
runinga mara chache.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya ya Umma cha Havard (HSPH) kilichopo Boston nchini Marekani, umebaini kuwa kuporomoka kwa kiwango cha mbegu za kiume kunahusiana moja kwa moja na kutofanya mazoezi na kutazama runinga kwa muda mrefu.
Imeelezwa kuwa wanaume wanaotazama runinga kwa zaidi ya saa 20 kila wiki wanapoteza asilimia 44 ya mbegu za kiume ukilinganisha na wale wasiotumia muda mrefu katika runinga.
Vilevile, wanaume wanaofanya mazoezi kwa zaidi ya saa 15 kwa wiki, wana uwezo wa kuongeza asilimia 73 ya mbegu zao ukilinganisha na wale wasiofanya mazoezi au wanaofanya mazoezi chini ya saa tano kwa wiki.
Kiongozi wa utafiti huo, Dk Audrey Gaskin alisema mtindo wa maisha unachochea zaidi upungufu wa mbegu za kiume na uzalishwaji wa mbegu za kiume.
Mtafiti huyo alifanya uchunguzi wa viwango vya mbegu za kiume za wanaume 189 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 22 kuanzia mwaka 2009 hadi 2010.
Wanaume hao walihojiwa kuhusu kiwango cha ufanyaji wao wa mazoezi, muda wanaotumia katika kutazama runinga au filamu katika kipindi cha miezi mitatu.
“Baada ya utafiti huo, nusu ya wanaume wasiofanya mazoezi na waliotumia muda mrefu katika runinga walikuwa na kiwango hafifu cha uzalishaji wa mbegu,” alisema Dk Gaskin.
Dk Gaskin alisema: “Masuala mengine ya kiafya yanayoweza kuathiri kiwango cha mbegu za kiume ni chakula, msongo wa mawazo na uvutaji wa sigara,” alisema.
Daktari huyo alisema mwanamume anapokaa kwa muda mrefu katika sofa mbegu za kiume zinapata kiwango kikubwa cha joto ambalo huathiri uzalishwaji wa mbegu.
Alisema wanaume wanaohitaji watoto wanatakiwa kuacha kuvaa nguo za ndani zinazobana ili kuimarisha kiwango cha mbegu za kiume huku madereva na waendesha baiskeli wakionywa kuwa katika hatari ya kupungukiwa kutoa mbegu nyingi.
Mhadhiri Mkuu katika Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza, Dk Allan Pacey anasema matokeo ya utafiti wake yatasaidia kuelimisha umma.
Hata hivyo, Daktari bingwa wa Uchunguzi wa Magonjwa kwenye Kitengo cha Patholojia katika Hospitali ya Muhimbili, Henry Mwakyoma aliyewahi kufanya utafiti kuhusu ugumba kwa wanaume, alisema bado utafiti wa Dk Gaskin una maswali mengi.
“Siwezi kuukubali au kuukataa utafiti wake, inawezekana ni mionzi au joto ndilo linalosababisha udhaifu wa mbegu hizo, lakini bado utafiti wake una maswali mengi,” alisema Dk Mwakyoma.
Alisema mazingira ya eneo husika na hali ya hewa na mlo vinaweza kusababisha mabadiliko ya kiafya, ikiwemo uzalishwaji wa mbegu za kiume.
Dk Mwakyoma aliwahi kufanya utafiti katika kipindi cha Oktoba 2009 hadi Septemba 2010 na kubaini kuwa kati ya wanaume 221 waliopimwa, asilimia 17.2 walikuwa hawana mbegu za kiume kabisa na asilimia 30.03 walikuwa na mbegu dhaifu na chache.
Hivyo basi, asilimia 47.05 ya wanaume waliokwenda kupima katika hospitali hiyo, waligundulika kuwa na matatizo ya ugumba.
Dk Mwakyoma alisema sababu za ugumba kwa wanaume huweza kusababishwa na kuambukizwa kwa vijidudu vya bakteria au virusi katika tezi inayozalisha mbegu za kiume au magonjwa ya zinaa.
“Baadhi wamezaliwa hivyo, miili yao haizalishi mbegu au walipata maambukizi ya vijidudu wakati wa kuzaliwa,” alidokeza Mwakyoma.
Alitaja sababu nyingine zinazosababisha ugumba kwa wanaume ni kuziba kwa mirija inayosafirisha mbegu za kiume kutoka katika korodani hadi katika uume na kwenda kwa mwanamke.
Sababu nyingine ni mionzi, hasa kwa watu wanaofanya kazi migodini, jeshini kutokana na baadhi ya kemikali zinazopatikana kwenye shughuli zao na hasa kuathiri watu wenye umri kuanzia miaka 50 hadi 59.
‘Pia, wanaume waliowahi kuugua ugonjwa wa matezi nao huathirika katika nyumba ya kuzalisha mbegu,” alisema Dk Mwakyoma.
Naye Injinia John Ben Ngatunga wa Tume ya Mionzi Tanzania, (TAEC) alisema mionzi iliyopo katika runinga nyingi za kisasa haziwezi kuleta madhara katika mwili wa binadamu.
“Pengine utafiti wake unaweza kuwa na ukweli iwapo kutazama runinga kutamwathiri mtu kisaikolojia.
Runinga nyingi ni zile zenye LCD (Liquid Crystal) ambazo hazina athari za mionzi,” aliongeza Ngatunga.
Alisema runinga nyingine zinaweza kuwa na mionzi, lakini ni pale ambapo mtu ataikaribia kwa umbali wa kati ya inchi saba hadi 12.
SOURCE:MWANANCHI
Social Plugin