Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Walalamikia kukosa kondomu

Na Godfrey Kahango, Mbeya 

BAADHI ya Madiwani wa Halmashuri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, mkoani hapa wameilalamikia kamati ya  kudhibiti Ukimwi ya halmashuri hiyo kwa madai kuwa imeshindwa kukidhi huduma ya ugawaji kondomu kwa watumishi wa halmashauri.
Imeelezwa kwamba katika suala la utoaji wa huduma hiyo ya kondomu kwa watumishi, kamati hiyo ikishirikiana na mratibu wa Ukimwi wa halmashauri hiyo, ilijiwekea utaratibu wa kuweka mipira  hiyo katika vyoo vya halmashauri hiyo na kwamba kila choo huwekwa boksi moja au mbili za Salama, lakini hiyo imeonekana kutofanyika kwa muda sasa, jambo lililowafanya madiwani hao kuhoji kwa nini imekuwa hivyo.
Madiwani hao walitoa hoja hiyo juzi katika uchangiaji wa taarifa ya Kamati ya Ukimwi, kwenye kikao cha baraza la madiwani cha halmashauri hiyo,kilichofanyika kwenye  ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Diwani wa Kata ya Nsalala, Mashauri Mbembela, aliitolea uvivu kamati hiyo akisema kuwa, kumekuwa na uzembe fulani wa kutoweka boksi hizo  za Salama kwenye vyoo vya halmashauri, ambapo utaratibu huo ulibainika wazi kwamba ulikuwa ukiwasaidia ipasavyo watumishi wake.
Hata hivyo kauli ya diwani huyo uliwasababisha umati mzima uliokuwemo katika kikao hicho kuangua kicheko, kwani  ilikuwa ni muda mfupi tu  baada ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mwalimgo Kisemba, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Ukimwi kuwasilisha taarifa ya utekelezaji  wa kamati hiyo ya Ukimwi.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Anderson Kabenga, akijibia hoja hiyo aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuonana na watumishi wa kitengo cha kuratibu Ukimwi katika halmashauri hiyo ili waweze kurudisha huduma hiyo ili kunusuru afya za watumishi.
Lakini pia katika majadiliano ya hoja hiyo, madiwani hao walihoji sababu za halmashauri hiyo kushindwa kutoa huduma ya elimu ya Ukimwi kwa ufanisi, badala yake katika mwaka uliomalizika ni kata 10 tu ndiyo zilipata huduma hiyo.

CHANZO:MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com