Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BABA AMZIKA MWANAE BAADA YA UGOMVI NA MKEWE



MTU mmoja Mkazi wa Kitongoji cha Iponjola Kijiji cha Isange Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya  anashikiliwa na Jeshi la Polisi akituhumiwa kumzika mwanaye wa kumzaa kwa siri ndani ya nyumba yake.
  
Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema lilitokea juzi majira ya saa Saba  mchana baada ya kugundua kuwa  mtoto Debora Riziki (3) kyusa, mkazi wa Iponjola, aligundulika akiwa amefariki baada ya kufukiwa kwenye shimo ndani ya nyumba ya baba yake mzazi.
  
Amemtaja mtuhumiwa kuwa ni Riziki Saidi Mwangoka (27),kyusa,mkulima ,mkazi wa Iponjola na kuongeza kuwa tukio hilo lilifanywa na mzazi huyo Novemba 29, Mwaka 2012.
  

Amesema  chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa kindoa kati ya mtuhumiwa na aliyekuwa mke wake Esther  Msafiri Mwambenja (23),kyusa,mkulima ,mkazi wa Kibumbwe-Kiwira.
  
Kamanda Diwani amesema mgogoro wao ulipelekea wagombee nani aishi na mtoto huyo baada ya wanandoa hao kutengana hivyo Novemba 28, Mwaka 2012 majira ya saa 11 Jioni  mtuhumiwa alimchukua kwa nguvu marehemu kutoka kwa mama yake na kwenda nae kwake kisha kumuua na kumfukia sebuleni ndani ya  nyumba yake.


Amesema  mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari kisha kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya kuzikwa ambapo mtuhumiwa amekamatwa na taratibu zinafanywa ili afikishwe mahakamani.

Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya  anatoa wito  kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi ili kuepusha matatizo yanayoweza kuepukika.
  
Pia  anatoa rai kwa wanandoa kutatua matatizo na migogoro yao kwa njia ya  kukaa meza ya mazungumzo badala ya kutanguliza hasira na matumizi ya nguvu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com