Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limesema matukio ya kujichukulia
sheria mkononi katika maeneo mbalimbali mkoani hapa yanasababishwa na baadhi ya viongozi wa
serikali za vijiji na makamanda wa sungusungu kuhusika katika kusimamia mauaji
hayo kwa matendo na kauli zao.
Hayo yamesemwa na kamanda wa polisi mkoani hapa ACP Evarist
Mangala mwishoni mwa wiki hii katika kongamano
la vikundi vya ulinzi shirikishi sungusungu”
mkoa wa shinyanga lililofanyika katika ukumbi wa VETA mjini hapa ambalo
lilikutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo viongozi wa dini.
“Viongozi hawa wamehusika kusimamia mauaji hayo kwa matendo
na kauli zao badala ya kuwaelimisha wananchi kutojichukulia sheria mkononi,na
pindi jeshi la polisi linapofika eneo la tukio hukuta mtuhumiwa kauawa na
linapouliza nani kahusika katika mauaji huambiwa kauawa na yowe maarufu kama
mwano, sasa unajiuliza yowe ni nani,lakini jibu ni binadamu hao hao”, Mangala
alisema.
Akizungumzia kuhusu mauaji yanayotokana na imani za
kishirikina,ingawa kwa miaka ya hivi karibuni yanaonekana kupungua,alisema
uchunguzi unaonesha kuwa waganga wa jadi wanaojihusisha na upigaji wa ramli
chonganishi wamehusika zaidi kuendeleza uwepo wa mauaji dhidi ya vikongwe na
walemavu wa ngozi, Albino.
Hata hivyo alisema bado kuna changamoto katika mauaji hayo
kutokana na sababu kuwa yapo ndani ya jamii au familia zaidi ,ambapo ndugu wa aliyeuawa
wamekuwa wahusika au wanajua wauaji wa ndugu yao, lakini hawasemi na wanalifanya suala
hili kuwa la siri.
“Wanajamii wa eneo husika mkiwemo makamanda wa sungusungu na
wenyeviti wa serikali za vijiji nyie mmekuwa sehemu ya kuficha siri hizo,
nawasisitiza kusema ukweli popote na kwa jambo
lolote la kisheria”,Kamanda Mangala alisisitiza.
Kwa upande wake mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa
Shinyanga ACP Hussein Kashindye alivitaka vikundi vya ulinzi shirikishi yaani
sungusungu vilivyoanzishwa na kufundishwa kutii sheria za nchi,kutambua wajibu
na miiko ya kazi yao
ili kupunguza au kuzuia matukio ya uhalifu katika jamii.
“Wajibu na miiko ya sungusungu na ile ya askari polisi
haitofautiani ,kwani wote tunakatazwa kuulinda uhalifu na wahalifu waliopo
katika maeneo yetu, na badala yake tunawajibika kuwataja hadharani ili sheria
ichukue mkondo wake”,Kamanda Kashindye alisema.
Katika hatua nyingine aliwatahadharisha na kuwakumbusha kuwa
mhalifu naye ana haki yake,na haki hiyo inapatikana mahakamani tu na si
vinginevyo,hivyo mhalifu anapokamamtwa apelekwe polisi na polisi nao hawawezi
kumhukumu bali watampeleka mahakamani.
Aidha aliwaagiza wakuu wa upelelezi wa wilaya zote mkoani
hapa kufanya zoezi la kuwapiga picha makamanda wa sungusungu na viongozi wa vijiji vyote ikiwa ni pamoja na kuchukua
alama zao za vidole ili jeshi la polisi litambue viongozi wahalifu wanaojificha
katika vikundi hivyo vya ulinzi shirikishi.
Social Plugin