Watu
watatu wanaodaiwa kuwa ni mafundi cherehani wakazi wa kijiji cha Kizungu kata
ya Lyamidati tarafa ya Nindo wilaya ya Shinyanga wameuawa kwa kupigwa marungu
na wananchi wa kijiji hicho baada ya kubainika kuwa wamemdanganya kamanda wa
jeshi la jadi sungusungu kwamba wameibiwa vitambaa vya kushona pamoja na nguo.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka jeshi la polisi mkoa wa shinyanga tukio hilo limetokea
juzi majira ya saa nne usiku,ambapo mafundi cherehani hao watatu waliuawa kwa
kupigwa marungu sehemu mbalimbali za miili yao na kisha kuchomwa moto na
wananchi waliojichukulia sheria mkononi.
Kamanda
wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kamishina msaidizi wa polisi Evarist
Mangalla aliwaja watu waliouawa kuwa ni Juma Silivester(27),Ruben
Silivester(30) na Juma Marco(26) wote ni mafundi cherehani wakazi wa kijiji
hicho cha Kizungu.
Kamanda
Mangalla alieleza chanzo cha mauaji kinatokana na wananchi kujichukulia sheria
mkononi baada ya mafundi cherehani hao
kubainika kuwa walitoa taarifa za uongo kwa kamanda wa sungusungu kwamba
wameibiwa vitambaa mbalimbali vya kushona pamoja na nguo kwenye kibanda chao
cha kushonea ambapo baada ya ufuatiliaji wa taarifa hizo walibaini kuwa vitu
hivyo vilikuwa katika nyumba za wahusika.
Aliongeza
kuwa kitendo hicho kiliwakera wananchi
na kuanza kuwapiga marungu na kisha kuwachoma moto watu hao.
Kamanda
Mangalla alisema juhudi zakuwasaka na
kuwakamata watu waliohusika na mauaji hayo bado zinaendelea huku akiwataka
wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika hao kwani kitendo
hicho ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Social Plugin