WATUMISHI WA ZAHANATI WATUHUMIWA KUFANYA MAPENZI NA WAGONJWA-NZEGA TABORA

                                    

 WATUMISHI wawili katika zahanati ya Mwanhala wilayani Nzega, wamekumbwa na kashfa ya kufanya mapenzi na wagonjwa hospitalini.

Kutokana na kashfa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Bitun Msangi, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa watumishi hao.
 
Agizo la mkuu huyo limetolewa hivi karibuni, baada ya Diwani wa kata ya Utwigu, Sawaka Shita kuwalalamikia watumishi hao mbele ya Baraza la Madiwani, kwa kukithiri kufanya mapenzi na wagonjwa nyakati za kazi, licha ya kuonywa kwa mara kadhaa.
 
Diwani huyo aliliambia baraza hilo kuwa vitendo hivyo vina hatarisha maisha ya watumishi hao na ya wananchi, hususani waliotembea nao na kutishia kuvunja ndoa za wananchi.
 
Alidai kuwa taarifa hizo za malalamiko, zilishafika katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, tayari kwa utekelezaji, lakini wananchi wa kata hiyo walitaka kuifunga zahanati hiyo, baada ya kukithiri vitendo hivyo vya kufanya mapenzi katika wodi zilizopo.
 
Aliomba baraza liwahamishe na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watumishi hao, ambapo majina yao yamehifadhiwa kwa usalama wao, huku jitihada za kuwachukulia hatua zikifanyika.
 
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Patric Mbozu alisema suala hilo ni la hatari na linapaswa kufuatiliwa kwa umakini ili lipatiwe ufumbuzi na wananchi waendelee kupatiwa huduma za tiba.
 
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Abraham Mdeme alikiri kupokea malalamiko hayo na kuahidi kuwa suala hilo, litafuatiliwa mapema ikiwemo kuwahamisha kwa kufuata taratibu zilizopo.
 
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Msangi alisema watumishi hao, wamevunja maadili ya afya, hususani kufanya ngono katika wodi za zahanati kwa nyakati za kazi.

PERUZIBONGO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post