Katika hali isiyokuwa ya kawaida kaburi ambalo alizikwa
mtoto Shabani Maulidi (15), ambaye anadaiwa kufariki dunia miaka mitatu
iliyopita na kuonekana akiwa hai hivi karibuni, jana lilifukuliwa na viungo vya
mwili wake kukutwa ndani.
Kazi hiyo iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi
pamoja na Mtafiti wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Lucas
Ndungulu, ilizua taharuki kwa umati wa watu waliokuwa eneo hilo, baada ya
nyumba ya jirani lilipo kaburi hilo, Masanja Marwa, kubomoka ghafla wakati
ufukuaji huo ukiendelea, huku mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara
moja naye akianguka na kuzirai.
Kwa sasa mtoto huyo ambaye alionekana hai, amelazwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uangalizi wa kitaalamu.
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Ndungulu
alisema kuwa wameamua kufukua kaburi hilo
ili kupata sehemu ya viungo vya mwili kwa ajili ya vipimo.
“Lengo la kufukua kaburi hili ni kutaka tupate kiungo
chochote cha mwili wa marehemu ili tufanye utafiti wa kitaalamu ili tujue kama ni kweli huyu anayedaiwa kuwa ni mtoto wao ndiye,”
alisema.
Alisema kuwa ufukuaji huo umemalizika na kwamba wamepata
baadhi ya viungo vya mwili wa marehemu na kuchukua baadhi ya mifupa ya mapaja
yote mawili ambayo itapelekwa katika hospitali ya rufaa kwa ajili ya uchunguzi
zaidi.
Kwa mujibu wa Ndugulu, majibu ya vipimo hivyo yatatolewa
baada ya wiki mbili kama hakutakuwa na tatizo
lolote la kukatika kwa umeme.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita,
Adamu Sijaona, alisema kuwa pamoja na kuchukua viungo hivyo, pia watachukua
damu ya wazazi na mtoto mwenyewe.
“Tumechukua pia damu ya mama na baba wa Maulidi mwenyewe ili
tukapime vinasaba (DNA) na kama alivyosema
mtafiti, majibu yatatoka baada ya wiki mbili,” alisema.
Akizungumza baada ya kazi ya ufukuaji kumalizika, baba mzazi
wa mtoto huyo, Maulidi Shabani, alisema kuwa endapo majibu yatakuja tofauti au
vile wanavyokusudia, wapo tayari kuyapokea na kwamba ikigundulika huyo
aliyeonekana ni Maulidi, pia watampokea na kuendelea kumtunza.
“Lakini nina imani kuwa huyu aliyeonekana ni mwanangu
Maulidi kabisa, kwa sababu anazo alama zote,” alisema mzazi huyo.
Mtoto Maulidi aliyefariki dunia miaka mitatu iliyopita na
kufanyiwa matanga, alionekana akiwa hai baada ya kukutana na mama yake ana kwa
ana mapema wiki hii asubuhi wakati akienda kwenye shughuli zake za biashara.
Ilidaiwa na wazazi wake kuwa Maulidi alitoweka ghafla na
kushindwa kurudi nyumbani kwao Januari mosi 2011, wakati alipokuwa amewapeleka
mbuzi malishoni na mwili wake kuonekana baada ya siku tatu akiwa amefia kwenye
kisima cha maji.
Kwa mujibu wa baba yake, Maulidi hakurudi nyumbani siku
hiyo, ambapo waliendelea kumtafuta bila mafanikio na ndipo baada ya siku tatu
walimkuta akiwa amefia ndani ya kisima cha maji kilicho maeneo ya Kijiji cha
Nyankumbu, Kitongoji cha Mwembeni.
Tukio hili ni la tatu kutokea mkoani hapa ambapo wilayani
Kasamwa, mwanamke aliyefariki dunia miaka mitano iliyopita alionekana hai na
kutambuliwa na ndugu yake. Tukio la pili lilitokea Wilaya ya Chato, wakati
kijana aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita alionekana akiwa hai.
Chanzo:Tanzania
Daima
|
Social Plugin