Wakati Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), akisema kuwa
serikali yoyote yenye dalili za kuelekea kubaya huanza kufungia au
kudhuru vyombo vya habari halafu binadamu, Muungano wa Mabaza ya Habari
Duniani (WAPC) na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ)
wamelaani kitendo hicho.
Kauli hizo zimekuja zikiwa zimepita siku chache tangu serikali
kuyafungia magazeti ya Mwananchi kwa siku 14 na Mtanzania siku 90, kwa
kile kinachodaiwa ni kuchapisha habari za uchochezi.
Lembeli ambaye kitaaluma ni
mwandishi, alisema kuwa serikali yoyote inayotumia mabavu kama hayo,
hapo kuna madhara, na kwamba ni dalili mbaya kwamba inakoelekea siko.
Alisema kuwa amesikitishwa na hatua hiyo ya serikali kuyafungia
magazeti hayo kwa kutumia sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976,
wakati vyombo vya habari siku zote ndivyo vimekuwa watetezi wa wanyonge.
Lembeli alifafanua kuwa sababu kama hizo wakati mwingine ndizo
zinawafanya wananchi kukosa imani na serikali yao, hivyo hata wanahabari
wanapodhuriwa wanaihusisha serikali na matukio hayo.
Alisema kuwa kufungia vyombo vya habari si suluhisho la kutofichua
maovu, kwani siku hizi nchi ipo katika teknolojia ya kisasa na kwamba
ukifungia gazeti wanatumia mitandao.
“Ukifungia mitandao ya online, wanatumia kuhabarishana kwa njia za
simu. Ukianza kumuona baba anaziba midomo ya mtoto wake anayehoji na
kudadisi, basi hiyo nyumba ni lazima iwe na matatizo.
“Suluhisho hapo ni kujibu hoja na si kufungia, na kama kuna kosa, basi
baba anatakiwa kuwa wa kwanza kumkanya mtoto kwa njia sahihi badala ya
kufunga mdomo,” alisema.
Kwa mujibu wa Lembeli, sheria ya magazeti ya mwaka 1976, imepitwa na
wakati huku akishangaa sababu za serikali kushindwa kupeleka muswada
bungeni kuifanyia marekebisho.
CHANZO;TANZANIA DAIMA
Social Plugin