Na Hillary Shoo, Singida
Majambazi wanne waliohusika katika utekaji wa gari la Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) na kuwapora fedha waombolezaji kisha kuvunja jeneza na kumpekua marehemu, wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida, Flora Ndale, mwendesha mashitaka, Sajenti wa Polisi, Godwel Laurence, alidai kuwa Desemba 8 mwaka jana, washitakiwa kwa pamoja huko katika eneo la Kindai barabara ya Singida-Dodoma, waliteka gari la SUA lenye namba za usajili SU 3712 aina ya Land Cruiser hard-top lililokuwa limebeba mwili wa marehemu, mwanafunzi wa chuo hicho kuelekea Tarime kwa maziko na kuwapora waombolezaji fedha na mali nyingine.
Laurence alivitaja vitu vilivyoporwa kuwa ni pamoja na fedha taslimu, kompyuta mpakato (lap top), simu ya mkononi aina ya Samsung na moderm moja, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh 8,739,000.
Aliongeza kuwa siku ya tukio, saa 7:30 usiku wa manane, washitakiwa waliweka mawe makubwa barabarani hali iliyomlazimu dereva wa gari hilo kusimama, na ndipo walivamiwa na kuanza kuwapiga watu marungu na fimbo sehemu mbalimbali za miili yao na kisha kuwapora.
Alidai kuwa mkuu wa msafara huo, Makaranga Nona, pamoja na waathirika wengine wa tukio hilo, waliweza kuwatambua washitakiwa baada ya polisi kuendesha gwaride maalumu la utambuzi Desemba 10 mwaka jana.
Hakimu Ndale alisema upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka yoyote, kwamba washitakiwa wana hatia kama walivyoshitakiwa.
Alisema upande wa mashitaka umejiridhisha na mashahidi wa kesi hiyo baada ya kuwatambua washitakiwa kwa kutumia taa za gari wakati wakiwafanyia upekuzi huo siku ya tukio.
Pia alisema kutokana na washitakiwa kutojifunika nyuso kwa vitambaa maalumu vinavyotumiwa na majambazi wengi kwenye uporaji, hivyo waliweza kutambuliwa kirahisi na upande wa mashitaka.
Katika utetezi wao, washitakiwa waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu, kwa kuwa wengi ni vijana na wengine wana watoto wanaosoma shule, na hivyo kuwategemea wao.
Hata hivyo, akisoma hukumu hiyo, Hakimu Ndale alisema licha ya utetezi huo maneno yao hayana miguu ya kusimamia, na kwamba sio lazima vitu vilivyoibwa vikutwe majumbani mwao.
“Kitendo mlichofanya ni cha kinyama na sio cha kibinadamu mbele ya jamii, kwa hiyo mikono yangu imefungwa juu yenu, pia mmefanya makosa ambayo adhabu yake imebainishwa wazi sio ya kupunguza bali ikiwezekana kuongezwa.
“Mahakama hii inawahukumu kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja ili iwe fundisho kwenu na watu wengine wenye tabia ya kufanya vitendo vya kinyama kama hivyo mbele ya jamii, haki ya kukata rufaa mnayo ndani ya siku 30,” alisema.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin