Mwanaharakati
wa haki za Binadamu, Yasin Yuta, alisema majirani waligundua baada ya
kusikia kelele za mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Erasto Emmanuel
(11) aliyekuwa amefungiwa ndani na kukaa kwa siku tano.
Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto
vimeendelea kushika kasi katika baadhi ya maeneo hususani vijijini, licha ya
Serikali na asasi mbali mbali kulipigia kelele ambapo hivi karibuni Baba mmoja
aliamua kuuza nyumba ikiwa na watoto ndani na kutokomea kusikojulikana na
kuwaacha wasijue la kufanya.
Mkasa huo wa ajabu ulitokea katika
kijiji cha Hatwelo, Kata ya Ijombe Mbeya Vijijini ambapo Mkazi huyo
aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Yuta alipouza nyumba yake na kutokomea yeye
na mkewe na kuwaacha watoto wawili wenye umri kati ya miaka 9 na 11 wakikosa
mahala pa kuishi.
Akizungumzia sakata hilo kijijini hapo,
Mwanaharakati wa haki za Binadamu, Yasin Yuta, alisema majirani waligundua
baada ya kusikia kelele za mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Erasto
Emmanuel (11) aliyekuwa amefungiwa ndani na kukaa kwa siku tano.
Alisema baada ya kumfungulia mtoto huyo
ndipo ilipobainika kuwa nyumba hiyo ilikuwa imeshauzwa huku mtoto akiwa ndani
na ndipo mnunuzi alipofunga na kufuli bila kujua kama kuna mtoto ndani huku
watoto wengine wakiwa kwa ndugu zao ambao pia hawakuelezwa kama nyumba imeuzwa.
Nyumba hiyo iliuzwa kwa Dati Nsagaje kwa
gharama ya shilingi 750,000/= ikiwa ni nyumba mbili pamoja na kiwanja ambapo
mnunuzi huyo alilipa kianzio cha shilingi laki nne biashara iliyofanyika tangu
April 26 mwaka huu na kiasi kilichobaki wakiwa wameahidiana kulipana
Mwezi Mei 15, Mwaka huu.
Wahanga wa tukio hilo ambao ni watoto
walisema hawakuwa na taarifa zozote za kuuzwa kwa nyumba wanayokaa ambapo
walisikia kuwa baba yao ameenda Sumbawanga kumfuata mke wake ambaye
inasemekana aliolewa na mwanaume mwingine.
“ Nilikuwa nimelala ndani ambapo
nilipoamka asubuhi nilikuta mlango umefungwa kwa nje hata hivyo nilivumilia
hadi njaa ilipoanza kuniuma baada ya siku tano nikaanza kupiga kelele
ndipomajirani walipokuja kunifungulia na kuniambia nyumba imeuzwa” alisema
mtoto Erasto Emmanuel.
Mtoto mwingine aliyetelekezwa ambaye
siku ya tukio alikuwa ameenda kulala kwa bibi yake Groli Emmanuel (9) ambaye ni
mwanafunzi wa shule ya msingi Hatwelo alisema siku akiwa anaondoka aliagwa na
baba yake ambaye alimwachia shilingi 3000 lakini hakumwambia kama nyumba
imeuzwa.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya
kawaida na kuonesha kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi wa Serikali ya
Kijiji ambao walishiriki moja kwa moja zoezi hilo huku wakiwa wamesaini kama
mashahidi na kugonga mhuri wa Serikali ya Kijiji walipoulizwa kuhusiana na
sakata hilo hawakuwa na majibu ya kuridhisha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Hatwelo,
Ibrahimu Mponzi, alisema kitendo alichokifanya muuzaji ni cha kawaida kwa
sababu ameuza mali yake mwenyewe na kwamba wao kama majirani na serikali ya
kijiji hawawezi kuhoji atakako waacha watoto kwa sababu ni mipangilio ya maisha
ya kila mtu.
Mbali na mwenyekiti wa Kijiji kuwa
shahidi wa upande wa mnunuaji akiwa sambamba na watu wengine wanne akiwepo
Mkewe ambaye pia ni Balozi wa nyumba kumi pia waliosaini wengine ni ndugu wa
mnunuaji ili hali muuzaji akiwa hana shahidi hata mmoja.
Chanzo-Mbeya yetu
|
Social Plugin