Katika dunia ya leo, watu hususan
wafanyabiashara kuwa na wavuti (website) sio jambo la anasa wala la
hiari. Kwa walio makini wavuti ni jambo la lazima.
Maendeleo ya Tehama yamefanya gharama
za kutengeneza na kumiliki wavuti kushuka, huku watengenezaji wake
wakiwa karibu na wateja.
Kila kona katika miji yetu wapo
wataalamu wanaoweza kutengeneza wavuti, achilia mbali kampuni za Tehama
kama vile Wordpress na Blogspot zinazowawezesha watumiaji wake kuwa na
wavuti bila ya kulipia gharama yoyote.
Hata hivyo, kumiliki wavuti sio
mwisho wa safari. Wamiliki wengi wana wavuti, lakini hazifanyi kazi kwa
kuwa zimelala usingizi mnono. Kwa wenye biashara wavuti ni sehemu ya
kujitangaza na pia njia mojawapo ya kuwasiliana na wateja.
Makala haya yanakusudia kuainisha
makosa kadhaa yafanywayo na wamiliki wa wavuti na namna ya kuyaepuka kwa
minajili ya kuupa mafanikio wavuti wako.
Kukosa mwelekeo.
Japo wavuti katika dunia ya sasa, ni
sehemu ya biashara, wamiliki wengi hapa nchini hawajui nini kifuate
baada ya kuwa na wavuti. Wengi huishia kwenye hatua ya kuwa na wavuti
pekee.
Hivi umejiuliza kwa nini uliamua kuwa na wavuti? Haingii akilini kama jibu lako litakuwa ulifanya hivyo ili tu nawe uonekane.
Ili uweze kuona matunda ya wavuti,
lazima ujue lengo na mwelekeo wako. Kwa wenye biashara, mwelekeo huo
lazima uende sambamba na biashara husika. Kwa mtazamo wangu sioni tija
ya kuwa na wavuti kama mtu hatojali maslahi hasa yale ya kibiashara.
Kutokutumia takwimu
Takwimu ni mojawapo ya vitu muhimu
kwenye wavuti wowote. Hata hivyo, wengi hawajui umuhimu wake achilia
mbali namna ya kuzitumia.
Swali muhimu, kama hujui idadi ya
watembeleaji wa wavuti wako, wanafanya nini wakiwa huko au wanapendelea
kurasa zipi za wavuti; utawezaje kupima uwezo wa wavuti uliouanzisha?
Kimsingi, takwimu hutoa picha halisi
ya matumizi ya watembeleaji wa wavuti wako. Aidha takwimu zitakujulisha
tabia za wateja wako, kurasa wanazopendelea, mahala walipo na hata muda
wanaopenda kufungua wavuti wako.
Angalia mfano huu. Unamiliki wavuti
kuhusu mgahawa uliopo Arusha, lakini kwa kutumia takwimu unabaini
asilimia kubwa ya watembeleaji wanapatikana mkoani Dar es Salaam. Kwa
mfanyabishara makini hii ni taarifa ya kuifanyia kazi kwa maendeleo ya
mgahawa.
Ili kutatua tatizo hili, unashauriwa
kutumia programu za takwimu, huku ukitafuta wataalamu wanaoweza
kukutafsiria maana ya takwimu hizo kwenye lugha ya kibiashara zaidi.
Katika wavuti nyingi hivi
leo,wahusika wameweka takwimu kuhusu watembeleaji pekee. Idadi pekee
haitoshi kwani kuna mengi yanayopaswa kujulikana ili hatimaye yaweze
kufungamanishwa na bishara na hata uwekezaji kwenye Tehama.
Kukosekana sehemu ya kutafuta taarifa
Kwa wavuti kubwa zilizo na vitu vingi
au kufanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara, sehemu ya kutafuta taarifa
(search button) ni lazima.
Sehemu hii sio tu itasaidia kuokoa
muda wa watembeleaji wa wavuti ambao hawana muda wa kuanza kujaribu
kurasa moja hadi nyingine, lakini pia utasaidia kuongeza muingiliano
kati ya wavuti na watembeleaji.
Cha muhimu hakikisha unakuwa na
sehemu ya kutafuta taarifa kwenye wavuti wako. Pia hakikisha unaunganisa
kitafuto hiki na mitambo ya takwimu, ili kukupa picha halisi ya vitu
gani ambavyo watu wanavitafuta kwa kiasi kikubwa kwenye wavuti.
Zingatia mfano ufuatao; Una wavuti
kuhusu saluni ya kinamama, ukiwa na sehemu ya kutafuta taarifa na kisha
takwimu zikaonyesha watu wengi wanatafuta bidhaa X, taarifa hiyo
itakuwezesha kuboresha mpango wa biashara yako.
Kurasa zisizoweza kutambazika
Kimsingi watu wengi wanapotafuta
taarifa kwenye wavuti, hawasomi bali wanatambaza (scan) na huondoka mara
wanapokosa taarifa husika. Hapa kuna kosa linalofanywa na wamiliki wa
wavuti hasa Tanzania.
Wamiliki wengi wanashindwa kutoa
picha ya website yao kwa jicho la kwanza. Wavuti na blogu nyingi za
Tanzania zimejaa vitu vingi kiasi msomaji anashindwa aanzie wapi.
Ilivyo hutakiwi kuandika maneno
milioni moja ili kumfanya mtu atumie wavuti wako. Watembeleaji hawana
muda wa kuanza kudokoa kitu kimoja kimoja. Wengi wanadhani, kuwa na
makala nyingi ndio kufanikiwa. Andaa taarifa inayojitosheleza katika
njia nyepesi na rafiki zaidi.
Kukipa kisogo Kiswahili
Inasikitisha kuona wamiliki wengi
wakitumia lugha ya Kiingereza kwenye wavuti zao ambazo kimsingi wateja
wao wakubwa ni watumiaji wa lugha adhimu ya Kiswahili.
Inawezekana matumizi ya Kiingereza
yakawa mujarabu zaidi ikiwa biashara husika ni ya kimataifa, lakini kama
biashara ama taarifa inahusu zaidi Watanzania ambao wengi wanatumia
Kiswahili, hakuna haja ya kutumia lugha ngeni.
Matumizi ya lugha ipi inafaa kwenye
wavuti yategemee vitu kama vile lengo na mwelekeo wa wavuti na nani
unawalenga. Ukijiuliza haya utakuwa na nafasi nzuri ya kuchagua lugha ya
kutumia katika wavuti wako.
Wapo wanaotumia lugha zaidi ya moja kufikisha taarifa kwenye wavuti zao. Ni jambo la kupongeza na la kuigwa.
Mkata Nyoni ni mtaalamu wa Menejimenti ya Teknolojia ya Habari na Mshauri wa Biashara.Anapatikana kupitia barua pepe: mnyoni@dudumizi.com
CHANZO-DJ'ARUNGU
Social Plugin