Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA 11 WANASWA WAKIJIFUNZA UGAIDI

 


Osama Bin Laden enzi za uhai wake

Na Happiness Mnale
 
 
 
Hofu ya vikundi vya kigaidi vya Al-Shabaab na Al-Qaeda kuwapo nchini imeanza kujidhihirisha baada ya Jeshi la Polisi mkoani Mtwara kuwakamata vijana 11 wakichukua mafunzo ya kigaidi mlimani wakiwa na CD zinazoonesha mauaji mbalimbali ya vikundi hivyo.
Tukio hilo linakuja zikiwa ni siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete kuviagiza vyombo vyote vya dola kuchukua tahadhari ya kuimarisha ulinzi maeneo yote nchini kufuatia shambulizi la kigaidi lililotokea nchi jirani ya Kenya na kuua watu zaidi ya 67 na wengine 175 kujeruhiwa.
Magaidi ambao hadi sasa wanajitambulisha kuwa wafuasi wa kundi la Al-Shabaab la nchini Somalia, ndio wamekuwa wakijigamba kutekeleza shambulizi hilo katika jengo la biashara la Westgate jijini Nairobi kama shinikizo la kuitaka Kenya iondoe jeshi lake nchini Somalia.
Vijana hao wanaodaiwa kujihusisha na mafunzo ya ugaidi walikamatwa wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara, katika Mlima wa Mkoliongo wakiwa na vifaa mbalimbali zikiwamo CD 25 za mafunzo hayo.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zelothe Stephen, alisema kuwa vijana hao walikamatwa wakiwa na CD zilizoonesha mauaji ya Osama Bin Laden, Idd Amin Dadaa wa Uganda na mafunzo ya Al-Shabaab.
Itakumbukwa kuwa Osama ndiye muasisi na kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda linalodaiwa kutekeleza mashambulizi kadhaa duniani, likiwamo lile la balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 1998.
Kiongozi huyo alisakwa kwa udi na uvumba na Marekani hadi alipouawa mwaka juzi akiwa mafichoni nchini Pakistan, lakini vitendo vya kigaidi bado vimeshika kasi.
Kamanda Stephen alitaja CD nyingine walizokutwa nazo vijana hao kuwa ni ‘Zinduka Zanzibar’, zinazoonesha namna ya kuua, kuandaa majeshi na nyinginezo zinazohusisha mafunzo ya kigaidi ya Al- Shabaab.
Pia alitaja vitu vingine kuwa ni ‘solar power’, ‘DVD play’, visu, mapanga, betri, jiko la mkaa, baiskeli tatu, mfuko wa mbaazi, jiko la mafuta na nembo yenye nanga ya meli.
“Ni mapema mno kuwaelezea kwa undani, ila mafunzo yao yanaendana na Al-Shabaab na tutafanya uchunguzi kubaini mambo mbalimbali ikiwamo nani yuko nyuma yao,” alisema.
Stephen alieleza kuwa vijana hao wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18-39, ambapo kiongozi wa kundi lao alifahamika kwa jina la Mohamed Makai.
Alisema kuwa vijana hao wamefikishwa mahakamani na kujibu tuhuma za kukutwa na vitu hivyo na kujifunza mafunzo hayo kinyume cha sheria.
Pia alisema kuwa upelelezi wa kina unaendelea kwa kushirikiana na makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam pamoja na mikoa mingine.
Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali zinazohusisha masuala ya uvunjifu wa amani, kwani usalama ni wa Watanzania wote.
chanzo-Tanzania Daima

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com