Mzee
Lukata Singu (65) anayeishi katika Kijiji cha Nyamwage wilayani Rufiji Mkoa wa
Pwani, anajivunia kuwa na familia kubwa yenye wake wengi wanaofikia 15 na
watoto zaidi ya 70.
Nimemtembelea
kijijini hapo ambapo amejenga boma analoishi na baadhi ya wake, watoto na
wajukuu.
Singu
amenikaribisha nyumbani kwake na kutaka apate picha ya ukumbusho na familia
yake japo haijakamilika. Kisha anaanza kusimulia:
“Mimi
nilizaliwa Shinyanga, sijui mwaka gani ila wakati Mwalimu Nyerere anaanza
kutawala wakati wa uhuru nilikuwa na miaka 13. Wazazi wangu walihamia Tabora na
baadaye Manyoni. Nimeishi Manyoni kwa muda mrefu hadi nikawa na familia.
Nimeishi pia Igunga na Tabora. Huko kote nimeacha wake zangu na watoto,”
anasema Singu.
Anasema
alihamia wilayani Rufiji miaka saba iliyopita akiwa na ng’ombe 600 hata hivyo
wengi walifia njiani wakati wa kuwasafirisha na magari.
“Hapa
ninaishi na wake zangu 12. Wengine hawakuja hapa kupiga picha, wamebaki kwenye
maboma wanalinda vyakula. Hawa wengine unaowaona ni watoto na wajukuu. Nina
wake wengine watatu wilayani Igunga, Tabora na Manyoni, kote huko nimeacha
familia,” anasema Singu.
Licha
ya wingi wa wake na watoto, bado Singu anasisitiza kuwa hajaacha kuzaa kwani
baadhi ya wake zake bado ni wajawazito.
“Siyo
kwamba nimemaliza kuzaa wala kuoa, tena baadhi ya wake zangu wana mimba. Kwa
nini niache kuzaa wakati bado nina nguvu?” anahoji.
Siri ya kuoa wake wengi
Singu
anaeleza siri ya kuoa wanawake wengi kuwa ni nguvu za kiume alizonazo kulingana
na umri wake mwenyewe akisema ni nguvu alizojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
“Ni
uwezo tu wa Mwenyezi Mungu, maana mimi nilizaliwa hivyohivyo, ndivyo Mungu
alivyoniumba… Situmii dawa yoyote. Kama Mungu asingeniwezesha nisingekuwepo kwa
sasa,” anasema na kuongeza:
“Sina
dini yoyote, ila ninaamini Mungu yupo na ndiye anayeniwezesha. Huwa ninamwomba
na kumshukuru. Tumezaliwa tumemkuta kwa hiyo kusali ni muhimu… naamini yupo na
kama asingeniwezesha ningeshafutika.”
Akizungumzia
elimu kwa watoto na wajukuu wake, anasema hiyo siyo kipaumbele kwake, huku
akisisitiza kuwa kuna uhaba wa shule katika kijiji hicho.
“Watoto
hawa hawasomi, tatizo huku hakuna shule, hata wenyeji wa huku hawasomi kazi ni
kukata miti tu. Hata hivyo kuna watoto wangu wako Tabora ndiyo wamesoma, lakini
sijui wamefikia darasa la ngapi,” anasema.
Ndoa za utotoni
Mbali
na mzee Singu, yupo mjukuu wake, Jiraa Lukanda Lukata anayekadiriwa kuwa na
miaka 30 anayeonekana kufuata nyayo za babu yake.
Jiraa
ameoa wake watatu na anaishi na babu yake kwenye boma hilo. Kwa mke wa kwanza,
Gindu Shija mwenye umri wa miaka 21 ana watoto wanne huku mke wa pili, Lawi
Kulwa (miaka 21) na Holo Shija (miaka 15) walioolewa miaka miwili iliyopita
bado hawajapata watoto.
Hata
hivyo, Jiraa anakanusha kufuata nyayo za babu yake:
“Siyo
kwamba nafuata nyayo za babu, mimi naishia hawa wake watatu tu wanatosha,”
anasema Jiraa.
Akieleza
taratibu za kupata wake hao, Jiraa anasema wazee hasa babu yake wamehusika
kumtafutia.
“Kwa
taratibu zetu za Kisukuma, wazee huchunguza wanawake wenye tabia nzuri kutoka
kwenye koo nyingine. Hawa wake zangu babu yangu alinioza baada ya kuridhishwa
na tabia zao,” anasema na kuongeza:
“Mke
wa kwanza nilimwolea katika kijiji cha Muhoro hapa hapa Rufiji.
Akizungumzia
ufahamu wake kuhusu sheria za ndoa anasema licha ya kutokuwa na elimu yoyote
anazifahamu sheria zinazokataza ndoa za utotoni.
“Mimi
sina elimu yoyote wala wake zangu hawana elimu, lakini naelewa baadhi ya sheria
za ndoa. Najua sijafanya kosa kosa lolote kuoa wake wenye umri huu,” anasema.
Nao
wake wadogo wa Jiraa Lawi na Holo wanasema kuwa wameridhika kuolewa naye.
Kuhusu
elimu ya wake hao, Gindu, Lawi na Holo wanasema wamemaliza darasa la saba
lakini hawajui kusoma wala kuandika.
Uhusiano na kijiji
Licha
ya kudai kuwa eneo analoishi katika kijiji hicho kuwa lake, inaelezwa kuwa
Singu hana uhusiano mzuri na wanakijiji wenzake.
Akiwa
nyumbani kwake, Singu anasema maeneo yote yanayozunguka makazi yake anayamiliki
kihalali.
Haya
yote unayoyaona hapa ni mashamba yangu, nimekuwa nikilima mihogo na mahindi.
Kwa sasa watoto wangu wanatayarisha mashamba kwa ajili ya kilimo.
Hata
hivyo Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ibrahim Mboweto anasema kuna utata katika
umiliki wa eneo hilo.
“Singu
ni kati ya wafugaji waliokuja na kuvamia maeneo ya vijiji. Baadaye waliomba
ndiyo akaruhusiwa. Lakini kwa kuwa ana mifugo mingi ilionekana lile siyo eneo
la mifugo na wananchi wanalalamika kuwa mifugo yake inaharibu mashamba yake,”
anasema na kuongeza:
“Kuna
wakati alifukua kisima cha asili akawa akitumia kunywesha mifugo yake, lakini
aliwakataza wanakijiji wasikitumie, ndiyo nao wamekasirika wanamlazimisha
ahame. Mwenyewe amegoma akisema ili ahame wanakijiji wamhamishe kwa gharama
zao. Tumemwachia mkuu wa wilaya maana hatuna uwezo tena.”
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu amekiri kuufahamu mgogoro huo na kwamba
anaushughulikia.
“Mgogoro
huo ulifika kwangu na nilifika kwenye mkutano wa kijiji, Singu akaonyesha
nyaraka zake za kumiliki hilo eneo,” anasema Babu na kuongeza:
“Yule
mzee alimilikishwa eneo na kijiji hivyo amewaambia kama wanataka ahame inabidi
wamlipe Sh90 milioni alizowekeza pale. Ndiyo nimewaambia wanakijiji wasubiri
wakati mwanasheria wangu anaangalia uwezekano mwingine, wataambulia kesi.”
Kuhusu
suala la elimu kwa wa watoto wake, Babu anasema amekuwa akihamasisha jamii za
wafugaji kupeleka watoto wao shule, ila kama hawataki ni juu yao.
“Kila
ninapokuwa kwenye mikutano nawahamasisha hasa jamii za wafugaji wapeleke watoto
shule. Tumejenga shule nyingi na walimu wapo. Kuna baadhi ya wafugaji
wamewanunulia watoto wao baiskeli wanakwenda shule. Kama yeye anaona starehe ni
kuoa wake wengi na kuzaa, basi hiyo shauri yake,” anasema Babu.
Utility
Kwa
mujibu wa sensa ya mwaka 2012, idadi ya Watanzania imefikia 44,928,923
ukilinganisha na idadi ya 12,313,469 ya mwaka 1967 wakati ambao kulikuwa na
ukuaji wa asilimia 2.9 kwa mwaka.
Watoto
walio chini ya umri kwa miaka 15 ni sawa na asilimia 44.1, huku walio kati ya
umri wa miaka 15 hadi 35 wakifikia asilimia 35.5, asilimia 52.2 ikiwakilisha
kundi la watu wenye umri kati ya 15 hadi 64 na asilimia 3.8 ni kundi la watu
wenye umri zaidi ya 64.
Idadi
yay a Watanzania inahusisha makabila zaidi ya 120 huku makabila ya Wasukuma,
Wahaya, Wanyakyusa, Wanyamwezi na Wachaga wakiwa na zaidi ya watu milioni moja.
Mkakati
wa Kukuza uchumi na kupunguza umaskini (Mkukuta) umelenga kufikisha huduma za
kudhibiti uzazi kwa asilimia 60 ya wanawake wote ifikapo mwaka 2015 na utagharimu
kiasi cha dola 88.2 milioni kati ya mwaka 2010 na 2015.
Hata
hivyo bajeti ya Taifa na utekelezaji wa mkakati huo umekuwa dhaifu licha ya
fedha za uzazi wa mpango zimeongezeka mara tatu tangu mwaka 2010 hadi 2011.
Licha
ya Serikali kuukubali mpango wa ‘Kila mwanamke Kila mtoto’ ambao ni wa kwanza
duniani na unaohamasishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
kuhusu afya ya wanawake na watoto, Mpango wa maendeleo wa miaka mitano
uliotangazwa mwaka 2012 na Rais Jakaya Kikwete una kipengele kimoja tu cha
uzazi wa mpango.
Social Plugin