Akizungumza na waandishi wa habari
juzi kijijini kwake Nyanhembe kata ya Kilago wilayani Kahama mkoani Shinyanga,
mwenyekiti huyo ambaye taasisi yake inashughulika na masuala ya utawala bora,
utamaduni, michezo na haki za binadamu alielezea kushangazwa kwake na kauli
hiyo na kueleza siyo kweli Sumaye anaichukia rushwa kama alivyodai kwa vile
wakati akiwa waziri mkuu ariruhusu kufanyika mambo mengi yaliyokuwa yakiashiria
mianya ya rushwa.
Alisema katika kipindi hicho,
Tanzania ndipo ilipofunga mikataba mingi mibovu katika sekta ya madini,
viwanda, mashamba na ranchi za taifa ikiwemo uuzwaji wa benki ya umma (NBC)
iliyouzwa kwa bei ya kutupa ikiwa ni mikataba iliyofungwa kutokana na rushwa
kubwa.
“Binafsi napingana na Sumaye katika
hili, siyo kweli anachukizwa na tatizo la rushwa hapa nchini kama kweli
angekuwa na sifa hiyo basi wakati wa kipindi cha uongozi wake asingeruhusu nchi
yetu kufunga mikataba mibovu, leo hii watanzania wanalia kwa mikataba mibovu
iliyofungwa wakati wake,”alisema Mgeja
“Katika kipindi chake rushwa ilikuwa
kubwa sana, hata rushwa ya ngono ilishamiri wakati huo ili mtu aweze kupata
ajira, kama anabisha mimi nitamtajia watu waliopewa ajira wake wake baada ya
kutoa rushwa ya ngono, leo hii usafi anaodai anao uko wapi,”aliongeza
“Mimi nampa ushauri wa bure ni
vizuri aache kupaparika akae chini atulie, maana kauli zake anazozitoa hivi
sasa anaonekana amekuwa ni mtu wa kulalamika kila siku, hatoi ushauri nini
kifanyike ili tufikie mafanikio, asiwakumbushe watu vidonda alivyowasababishia
wakati wa uongozi wake,” alieleza Mgeja.
Mgeja alielezea kushangazwa kwake ni
kitendo cha vyombo vya dola kuendelea kufukuzana na vidagaa huku vikiwaacha
mapapa waliosababisha nchi kuingia katika matatizo makubwa ikiwemo wizi wa fedha
za EPA, Meremeta, mikataba ya Songas na IPTL ambayo yote yalifanyika wakati wa
Sumaye.
“Tunashangaa hii nguvu ya kuwasonta
vidole wenzake anaipata wapi au ana lengo la kufunika madhambi yake
aliyoyafanya wakati akiwa waziri mkuu, lakini suala la rushwa analopigia kelele
hakuna mtanzania anayelipinga wote tunakerwa na rushwa, ni vizuri angeonesha
mfano mzuri kwa kukemea mikataba mibovu iliyofungwa katika kipindi chake,”
alisema Mgeja.
Alisema uingiaji wa mikataba mibovu
inayoiumiza nchi hivi sasa ni rushwa kubwa kushinda rushwa ndogondogo
anazozipigia kelele Sumaye na kwamba huenda kinachosababisha apige kelele na
kutapatapa ni baada ya kuangushwa kwenye uchaguzi wa mjumbe wa NEC wilayani
Hanang mkoani Manyara ambako alishindwa na Mary Nagu.
Pia Mgeja alitoa mfano wa maamuzi
mabovu yaliyofanyika kipindi cha uongozi wa Sumaye kwa kuamua kuuza nyumba za
umma zilizojengwa kwa nguvu ya watanzania wote wakiwemo wafugaji, wavuvi na
wakulima ambao hawakushirikishwa katika kufikia maamuzi ya kuuzwa kwake na
badala yake waliokumbuka ni wafanyakazi peke yao.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi
wa habari iwapo hivi sasa yupo katika harakati za kumfanyia kampeni mmoja wa
watu wanaotaka kuwania urais nchini, Mgeja alisema yeye binafsi haamini kama ni
wakati muafaka wa watanzania kuanza kulumbana juu ya mtu gani awe Rais mwaka
2015.
“Mimi nafikiri suala nani awe rais
mwaka 2015 siyo wakati wakati hivi sasa, na halipaswi kupewa nafasi ya
kusababisha watanzania tugawanyike, tujengeane uhasama, chuki na fitina na
kusababisha kupoteza umoja na mshikamano wetu tulionao, maana urais unapangwa
na mungu mwenyewe yeye ndiye anayemjua rais ajaye atakuwa nani,” alisema Mgeja.
Alisema suala la rais ajaye tayari
limo ndani ya mioyo ya watanzania, ndiyo wanaojua ni nani atakuwa rais wao
baada ya Rais Kikwete, hakuna sababu ya kulumbana na kwamba iwapo kelele
za Sumaye ni juu ya kutaka kuwania urais mwaka 2015, ni vizuri akawaachia
wananchi wenyewe ndiyo wataamua wakati utakapofika.
“Kama kelele hizi za mwenzetu ni urais
wa mwaka 2015, tunamshauri aache kupaparika, akae chini atulie, na asiwasonte
vidole vibaya wenzake, hakuna mtantania mwenye hatimiliki ya urais hapa nchini,
wote wana haki sawa, ni juu ya watanzania wenyewe kuamua rais wao awe nani,”
alisema Mgeja.
Hata hivyo alisema ni vizuri rais
ajaye awe na sifa mbili kuu moja ni kuwekeza hisa za imani kwa watanzania,
anayeaminika na sifa ya ziada iwe ni uwezo wa kutatua changamoto zilizopo
nchini.
Social Plugin