Kiwango cha ufaulu katika matokeo ya darasa la saba mwaka huu
kimeongezeka, ambapo wanafunzi 427,606, sawa na ongezeko la asilimia
19.89 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za
sekondari za serikali.
Hata hivyo licha ya ufaulu kuongezeka, matokeo hayo yanaonyesha kuwa
wanafunzi wengi wamefeli somo la Hisabati na wamefanya vizuri zaidi
katika somo la Kiswahili.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu
Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Dk. Charles Msonde, alisema somo la
Kiswahili liliongoza kwa asilimia 69.06 huku Hisabati likiambulia
asilimia 28.62.
Alisema kwa upande wa somo la Kiingereza, lilifanya vizuri kwa
asilimia 35.52, Maarifa ya Jamii asilimia 53.00 na Sayansi asilimia
47.49.
Katika hatua nyingine, wavulana wameng’ara kwa kuongoza kwa asilimia 55.1 na kuwapita wasichana waliopata asilimia 46.68.
Alisema wanafunzi 427,606 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali.
Alisema kati ya wanafunzi hao, wasichana ni 208,227 na wavulana ni
219,379, hivyo kufanya idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kuongezeka kwa
asilimia 19.89 tofauti na mwaka jana ambapo kiwango kilikuwa asilimia
8.8 .
Dk. Msonde alisema kuwa mtihani huo ulifanyika Septemba 11 na 12
ambapo watahiniwa walitumia karatasi maalumu za ‘optical mark reader’
na kusahihishwa kwa mfumo wa kompyuta.
“Matokeo haya yanaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 9,126 walipata daraja A, wakati wanafunzi 82,293 walipata daraja B.
“Jumla ya wanafunzi 336,187 walipata daraja C, 389,948 daraja D na
waliobaki, yaani 27,367 walipata daraja E,” alisema Msonde.
Hata hivyo, Msonde, hakuweza kutaja mikoa iliyofanya vema na ile
iliyoshika nafasi ya mwisho, zikiwamo shule zilizoongoza na kueleza
kuwa baraza limewasilisha matokeo hayo kwenye mamlaka husika.
“Tumewasilisha matokeo kwa mamlaka husika ili zifanye uchaguzi wa
watahiniwa wa kujiunga na elimu ya sekondari na matokeo hayo
yatatangazwa na mamlaka husika mara baada ya kazi ya uchaguzi
itakapokamilika,” alisema.
Akizungumzia udanganyifu katika mtihani, alisema takwimu zinaonyesha
kuwa idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo kutokana na kujihusisha na
vitendo vya udanganyifu katika mtihani huo imepungua.
Alisema waliofutiwa matokeo mwaka huu ni watahiniwa 13,
ikilinganishwa na watahiniwa 293 waliofutiwa matokeo kwa undanganyifu
mwaka jana.
Kuhusu tatizo la baadhi ya wanafunzi kutojua kusoma na kuandika,
Msonde alisema ni mapema mno kulijua hilo, kwani linahitaji muda.
Wanafunzi 844,983 wa shule za msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo
wa kumaliza darasa la saba, wengine 23,045 sawa na asilimia 2.66
hawakufanya kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya utoro, vifo,
ugonjwa na wasichana kupata mimba.
chanzo-Tanzania daima
|
Social Plugin