Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela amefariki dunia.Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma muda mchache uliopita amesema Mandela amefariki dunia nyumbani kwake mjini Johannesburg nchini humo akiwa na umri wa miaka 95,amesema taifa limepoteza baba wa taifa na bendera zitapepea nusu mlingoti kufuatia msiba huo mkubwa kwa taifa hilo.Mandela amekuwa akiugua kwa muda mrefu.
Naye rais wa Marekani Barack Obama amesema nchi ya Afrika Kusini pamoja na dunia kwa ujumla imepoteza mtu muhimu
Naye rais wa Marekani Barack Obama amesema nchi ya Afrika Kusini pamoja na dunia kwa ujumla imepoteza mtu muhimu
Historia ya Maisha yake
Nelson Rolihlahla Mandela alikuwa mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati
aliyepambana na sera za ubaguzi za makaburu wa Afrika Kusini na hatimaye kuwa
Rais wa kwanza Mwafrika nchini humo. Ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel.
Mbali na tuzo hiyo, ameshatunukiwa zaidi ya tuzo 250 katika miongo minne
iliyopita.
Alizaliwa Julai 18 mwaka 1918. Ni rais wa kwanza aliyechaguliwa
kidemokrasia nchini Afrika Kusini. Alikuwa mwanasheria na mwanachama wa Chama
cha African National Congress (ANC) aliyepinga siasa ya ubaguzi nchini Afrika
Kusini.
Mandela anatokea katika ukoo wa Thembu uliokuwa ukitawala mkoa
wa Transkei lililopo katika
jimbo la Eastern Cape .
Alizaliwa katika Kijiji cha Mvezo katika Wilaya ya Umtata na ana asili ya Kabila la Khoisan kwa
upande wa mama yake.
Babu yake wa upande wa mama aliyefariki mwaka 1832
Ngubengcuka, alikuwa mfalme wa ukoo wa Thembu na mmoja kati ya watoto
wake aliitwa Mandela. Huyo ndiyo Babu yake Nelson na chanzo cha jina hilo la ukoo.
Baba yake Mandela Gadla Henry Mphakanyiswa alikuwa chifu wa mji
wa Mvezo, hata hivyo baadaye aliondolewa na wakoloni katika cheo hicho na
kubaki kuwa mjumbe wa baraza. Mphakanyiswa alikuwa na wake wanne ambao
walimpatia watoto 13, wanaume wanne na wanawake tisa.
Mandela alizaliwa kwa mke wa tatu na kupewa jina la Rolihlahla
likiwa na maana ya kuvuta tawi la mti au kwa nahau ‘msababisha matatizo’.
Rolihlahla alikuwa mtoto wa kwanza katika familia yao kwenda shule ambako
mwalimu wake Mdingane alimpa jina la Nelson. Baba yake alifariki kwa ugonjwa wa
kifua kikuu wakati Mandela akiwa na umri wa miaka tisa, hivyo ndugu yake
aitwaye Jongintaba akawa mlezi wake.
Alisomea katika Shule ya Misheni ya Wesleyan. Alipofikisha miaka
16 alijiunga na Taasisi ya Clarkebury kwa miaka miwili ambapo alipata cheti cha
awali. Mwaka 1937 alihamia katika mji wa Healdtown katika chuo kingine cha
Wesleyan. Akiwa na miaka 19 alijihusisha na michezo ya masumbwi na riadha.
Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Fort Hare ,
ambapo alichukua shahada ya Sanaa na hapo ndipo alipokutana na Oliver Tambo
ambaye aliendelea kuwa rafiki yake kwa muda mrefu.
Baada ya mwisho wa mwaka wa kwanza, Mandela alijihusisha na
mgomo ulioandaliwa na baraza la wanafunzi wakipinga sera za chuo hicho. Matokeo
yake alifukuzwa shule hadi pale atakapokubali masharti ya chuo. Baadaye akiwa
jela, Mandela alisoma shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha London katika programu ya nje.
Baada ya kufukuzwa shule, mlezi wake Jongintaba alimtaka aoe
akiwa na ndugu yake Justice. Hata hivyo, Mandela hakutaka na hivyo akakimbilia
mjini Johannesburg
ambako alitafuta kazi ya ulinzi kwenye migodi ya madini, kazi ambayo hakuifanya
kwa muda mrefu.
Baadaye Mandela alianza kufanya kazi ya usaidizi wa ofisi katika
ofisi ya sheria mjini Johanesburg. Akiwa hapo alikamilisha masomo yake ya
Shahada ya Sanaa katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kwa njia ya posta na baada
ya hapo alianza masomo ya sheria katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand
ambako alikutana na marafiki wengine waliopambana katika vita ya ubaguzi wa
rangi ambao ni Joe Slovo, Harry Schwarz na Ruth First.
Siasa
Baada ya ushindi wa chama cha Afrikaner wa mwaka 1948
kilichokuwa kikiunga mkono ubaguzi wa rangi, Mandela alianza kujihusisha rasmi
na siasa. Alikiongoza chama cha ANC katika kampeni za uasi za mwaka 1952 na
mkutano wa mwaka 1955 ambao ulizaa mchakato wa uhuru na kuweka msingi wa kupiga
ubaguzi wa rangi.
Akiwa amevutiwa na siasa za aliyekuwa Waziri Mkuu wa India wakati
huo Mahatma Gandhi, Mandela alianza kufanya upinzani usio na vurugu.
Mwaka 1956, alikamatwa akiwa na wafuasi wake 150 na kushitakiwa
kwa uhaini. Hata hivyo baada ya kesi hiyo kwenda hadi mwaka 1961, waliachiwa
huru.
Kifungo cha maisha
Mwaka huohuo 1961 Mandela aliteuliwa kuwa kiongozi wa kikosi cha
silaha kikijulikana kama ‘Umkhoto we Sizwe’.
Aliratibu mapambano dhidi ya majeshi ya Serikali na kuweka mikakati ya vita vya
msituni, kama hujuma za kukomesha ubaguzi
zingekwama.
Agosti 5, 1962 Mandela alikamatwa na majeshi ya Serikali na
kuwekwa jela ya Johannesburg
baada ya kupotea kwa miezi 17.
Makundi mbalimbali yalihusishwa na njama za kukamatwa kwake
kikiwemo Chama cha South African Communist Party na kitengo cha Intelijensia
cha Marekani (CIA). Hata hivyo Mandela hakutilia maanani madai hayo.
Juni 12, 1964, Mandela alihukumiwa kifungo cha maisha baada ya
kujitetea mahakamani kuhusu harakati zake dhidi ya ubaguzi wa rangi. Alipelekwa
katika gereza lililopo katika Kisiwa cha Robben.
Februari 2, 1990 aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Fredrick de
Klerk aliondoa amri ya kukipiga marufuku chama cha ANC na makundi mengine
yanayopinga ubaguzi wa rangi na akatangaza kumwachia huru Mandela.
Aliachiwa rasmi Februari 11, 1990 tukio lililoonyeshwa dunia nzima.
Thabo Mbeki alichukua mamlaka kutoka kwa Mandela kama kiongozi wa chama tawala ANC na hata kushinda uchaguzi wa mwaka 1999.Mandela alimuoa Graca Machel, mjane wa aliyekuwa rais wa Msumbiji, akiwa na miaka 80. Aligunduliwa kuwa na saratani ya Tezi Kibofu na hivyo kuanza matibabu.Mnamo mwaka 2004, alitangaza kujiuzulu, akisema kuwa anataka maisha ya kimya nyumbani kwake na familia yake. Kwa mzaha aliwaambia wandishi wa habari wasimpigie simu.
Mwaka 2008 Wanamuziki, waigizaji na wanasiasa waliungana na Mandela katika sherehe kubwa uwanja wa Hyde Park mjini London kusherehekea miaka 90 ya kuzaliwa kwake. Akiongea na wale waliofika, aliwaambia, ”ni wakati kwa kizazi kipya kuchukua uongozi, kibarua kwenu sasa.”
Mandela aliweza kuonekana hadharani mara kadhaa baada ya kustaafu. Ingawa alionekana katika sherehe ya kukamilika kwa dimba la kombe la dunia mwaka 2010 nchini humo. Januari mwaka 2011, alilazwa hospitalini kwa ukaguzi maalum, huku serikali ikiwakumbusha watu kuwa aliwahi kupata matatizo ya kupumua. Alipokea matibabu ya ugonjwa wa mapafu mwaka 2012 na pia mwaka 2013 .
Nelson Mandela anefariki usiku wa kuamkia leo yaani Desemba 5 mwaka 2013 baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya mapafu.
Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu.Amina!
Social Plugin