Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, amesema kuwa vijana waliomfanyia fujo katika mkutano wake Wilayani Kasulu, wamefikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
Hayo aliyasema juzi mjini hapa alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara, uliofanyika katika viwanja vya Mwanga Center Kigoma mjini, uliohudhuriwa na mamia ya wapenzi wa chama hicho.
Alisema kuwa, wakati anafanya mkutano wake kasulu, ambapo ulikuwa ni mkutano wa halali ghafla walivamiwa na kikundi cha wahuni wachache waliotumwa na Chama Cha mapinduzi CCM, kuja kufanya fujo katika mkutano wake.
“Jamani hizo propaganda za siasa zitawapeleka pabaya jamani, CCM walijipanga Kasulu na kutuma vijana kuja kunifanyia fujo kwenye mkutano wangu, sasa wameshakamatwa jumla ya vijana 24 na wamefikishwa mahakamani.
“Na kwa kuwa makosa yao yanadhaminika, wamepewa dhamana na walio wadhamini ni viongozi wa CCM wa Kasulu, hamuoni kama hiyo ni hujuma,” alihoji Dk. Slaa.
Alisema kuwa vijana wanaoingia na mabango katika mikutano yake, wanakuwa wametumwa na wanaowatuma wameshawajua.
“Huwezi kuingia kucheza ngoma ya CHADEMA, wakati wewe si mwana CHADEMA na huwezi kuicheza ngoma ya CCM kama wewe si mwana CCM.
“Nilifika Kakonko walikuja vijana na bango kwa lengo la kuharibu mkutano wangu, kumbe walikuwa wametumwa tena mmoja wa vijana hao ni mtoto wa kiongozi wa CCM Wilaya ya Kakonko, jamani hakuna siasa za hivi,” alisema.
chanzo-chadema blog
Social Plugin