HAYA HAPA MASHTAKA 11 DHIDI YA ZITTO KABWE YALIYOWEKWA HADHARANI




Mashtaka 11 dhidi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, yamebainisha kuwa kosa kubwa la kiongozi huyo kijana, ni nia yake ya kutaka kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.

Chanzo chetu cha habari kilichoona mashitaka hayo kabla ya kutumwa kwa washitakiwa, kimebainisha kuwa makosa saba kati ya makosa 11, yanahusu kugombea uenyekiti Taifa, au kumkashifu Mwenyekiti wa Taifa.

“Ukiona hayo mashitaka yenyewe ndugu yangu, yanajirudia rudia na kuzunguka katika kosa moja la nia ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa… angalia kosa la kwanza, kosa la tatu, tano, sita nane na tisa, ni kama vile kuwania uenyekiti ndio kosa kubwa.


“Hata hivyo kwa jinsi mgawanyiko ulivyo ndani ya chama sasa, nakuhakikishia hawa jamaa (Zitto, Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba), watarudishwa katika nyadhifa zao na hakuna atakayeadhibiwa,” alisema mtoa taarifa wetu.

Alinukuu kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu aliyehoji kama makosa wanayotuhumiwa akina Zitto ni makubwa kiasi cha kuyeyusha mema aliyoyafanya katika chama. “Si umesikia akina Baregu wakizungumza? Kwa mashitaka yale nakuhakikishia kitakachofanyika ni kufunika kombe mwanaharamu apite,” alisema mtoa habari wetu.

Kosa la kwanza kwa Zitto, Dk Mkumbo na Mwigamba, wanadaiwa kuvunja Kanuni ya Chama inayokataza kukashifu chama, kiongozi au mwanachama yeyote. Katika maelezo ya kosa hilo, akina Zitto wanadaiwa kumkashifu Mwenyekiti wa Taifa, Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema.

Moja ya madai katika mashitaka hayo, ni kilichoandikwa katika Mkakati wa Mabadiliko 2013, kuwa Mbowe amekuwa akinunua vifaa vyote vya chama nje ya nchi kwa bei anayoijua mwenyewe na ambayo haihojiwi popote. Wanadaiwa pia wamemkashifu Dk Slaa kwa kudai ni mdhaifu kwa kumruhusu Mbowe kuingilia shughuli za kiutendaji.

Zitto na wenzake wanadaiwa katika kosa la pili, kutokuwa wawazi na wa kweli wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na udanganyifu kinyume na Kanuni za Uendeshaji kipengele cha 10.1 (VIII. Katika kosa la tatu, wanadaiwa kutoa tuhuma juu ya viongozi wenzao bila kupitia vikao halali na utaratibu wa ngazi zilizowekwa, kinyume na kanuni ya 10.1 (X).

Katika kosa la nne, akina Zitto wanadaiwa kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya chama, miongoni mwa jamii, kisiasa au kijamii. Katika kosa hilo wanadaiwa kwenda kinyume na kipengele cha 10.1 (IV), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.

Akina Zitto katika kosa la tano, wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya kuchonganisha na kuzua migogoro kwa viongozi wa chama au wanachama, kinyume na kifungu cha 10.1 (IX), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.

Katika kosa la sita ambayo mtoa habari wetu alisema ndio kubwa, Zitto na wenzake wanadaiwa kutekeleza mpango wa kusudio la kugombea uenyekiti wa Chama Taifa, bila kutangaza kusudio la kutangaza nafasi hiyo.

Hatua hiyo inadaiwa kuwa ni kinyume na kifungu 2.C cha Muongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi ya Uongozi wa Chama, Mabaraza na Serikali wa 2012.

Zitto na wenzake katika kosa la saba, wanadaiwa kutengeneza mitandao ya kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya kujihakikishia ushindi kinyume na kanuni ya 2 (D), ya Muongozo wa Kuwania Uongozi. Katika kosa la nane, Zitto na wenzake wanadaiwa kuwachafua viongozi na wanachama wengine wenye kusudio/nia ya kutaka kugombea nafasi ya uenyekiti kinyume na kifungu 2 (E) cha Muongozo wa Kuwania Uongozi.

Katika kosa hilo, kumewekwa maelezo ya ziada kuwa kosa hilo linaunganishwa na kosa la kwanza ambalo washitakiwa wanadiwa kuwakashifu Mbowe, Dk Slaa na Lema.

Kosa la tisa, akina Zitto wanadaiwa kujihusisha na upinzani dhidi ya chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa chama, kinyume na kifungu cha 10.3 (IV), cha Kanuni za Uendeshaji.

Kosa la kumi linamhusu Zitto peke yake, ambapo anaidaiwa kukashifu chama na kiongozi wa chama nje ya Bunge kinyume na kifungu 2 C (B), kikisomwa pamoja na kifungu 3 B cha Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya Wabunge.

Katika hilo Zitto kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa chama yaani Dk Mkumbo na Mwigamba na mtu mwingine ambaye hajajulikana, wanadaiwa kusambaza waraka uitwao Mkakati wa Mabadiliko 2013.

Mkakati huo, unadaiwa kukashifu chama na/ au viongozi wake wakuu kama ilivyoelezwa katika kosa la kwanza, tatu, nne na nane. Mwisho katika kosa la 11, Zitto na wenzake wanadaiwa kuchochea mgawanyiko ndani ya chama kinyume na kanuni ya 3 F ya Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya Bunge.

Katika hali inayoonesha muendelezo wa kupukutika kwa chama hicho, jana mkoani Mwanza kulianzishwa kinachoitwa Muunganiko wa Wawakilishi wa Matawi 189 ya Chadema katika mkoa huo.

Taarifa ya kiongozi wa Muungano huo, Robert Gwanchele, kwa vyombo vya habari, ilibainisha kuwa unawajumuisha wajumbe kutoka majimbo yote ya mkoa wa Mwanza na lengo ni kupinga hatua za Kamati Kuu dhidi ya Zitto na wenzake.

Kuibuka kwa muungano huo katika mkoa muhimu kisiasa kwa Chadema, kunaonesha kuwa chama hicho kinaelekea kupata pigo kwa wanachama kuanza kugawana makundi mawili yaliyoibuka katika chama hicho yanayoongozwa na wagombea uenyekiti; kundi la Mbowe na Zitto.

“Katika kikao chetu tulichoketi Novemba 30, 2013 kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa tisa kasorobo, pamoja na mambo mengine tumeazimia kuanzisha umoja huu wa wanachama.

“Hii ni kutokana na ukweli kwamba viongozi wetu wanaotuwakilisha kwenye vikao vya uamuzi kama vile wilaya, mkoa na taifa, wamekuwa waoga na wameshindwa kuwakilisha mawazo yetu tuliyowatuma badala yake wengi wao wamekubali kuwa vibaraka wa kile kinachoitwa Chadema Kaskazini,” ilieleza taarifa ya kundi hilo linalomuunga mkono Zitto.

Kundi hilo dhidi ya upande wa Mbowe Mwanza, limeeleza kuwa sababu zilizotolewa na Kamati Kuu kwa ajili ya kumuadhibu Zitto na wenzake, hazikubaliki na kutoa walizoziona kuwa ndio sababu za kuandamwa kwa kiongozi wao.

Kwa nini Zitto? “Uamuzi wa Kamati Kuu wa Novemba 20-21 mwaka huu wa kuwavua uongozi Zitto Kabwe, Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, umeonesha dhahiri si woga tu wa demokrasia, bali ni unafiki wa hali ya juu kwa viongozi wetu kukwepa demokrasia kwa kisingizio cha usaliti na uhaini ndani ya chama,” taarifa hiyo ilieleza. Taarifa hiyo iliyotolewa na Gwanchele, ilieleza sababu za kuandamwa kwa akina Zitto kuwa ni kutaka kujua mapato na matumizi ya fedha za chama zinazotokana na ruzuku ya fedha za serikali.

Nyingine ni michango ya wanachama na wapenzi kwenye mikutano ya wazi, harambee za Operesheni ya M4C Mwanza, Arusha na Dar es Saalam na kutaka kujua taratibu za ununuzi wa rasilimali za chama na namna wazabuni wa kusambaza bendera, kadi za chama, magari na pikipiki walivyopatikana. Nyingine ni kutaka kuona usawa wa kimadaraka kwa viongozi wote bila ubaguzi wa aina yoyote, kuanzia ngazi ya chini mpaka Taifa kinyume na ilivyo sasa hasa makao makuu ya chama ambapo ilidaiwa ukanda na ubaguzi wa hali ya juu umetawala.

“Mwenyekiti na Katibu Mkuu, wameshindwa kutatua migogoro ya viongozi na wanachama kutoka mikoani kwa njia sahihi za vikao na kwa wakati, hivyo kutoa mwanya kwa viongozi na wanachama kutumia njia ya mitandao ya kijamii tukiongozwa na Katibu Mkuu mwenyewe, kujitokeza mara kwa mara kwenye mitandao hiyo hiyo kwa madai ya kutolea ufafanuzi wa mambo mbalimbali yahusuyo masuala ya chama, ilihali akijua kufanya hivyo ni usaliti mkubwa kwa chama chake,” ilidai taarifa hiyo.

Gwanchele alidai katika taarifa hiyo kuwa njia hiyo ya Dk Slaa kutoa ufafanuzi wa mambo ya chama katika mitandao, ndiyo iliyosababisha migogoro mikubwa hususan katika mkoa wa Mwanza, iliyochangia kupoteza Halmashauri ya Jiji la Mwanza, baada ya kufukuzwa kwa baadhi ya madiwani.
“Tunataka kujua hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kumkashifu kiongozi wa chama Zitto Kabwe kuwa ni mnafiki na mzandiki kwenye mitandao ya kijamii,” ilieleza taarifa hiyo ya Gwanchele ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Matawi ya Chadema Mkoa wa Mwanza, Mwenyekiti wa Vijana Kanda ya Chama Ziwa Magharibi na Mjumbe Kamati Tendaji Wilaya Ilemela.

“Tunataka kujua hatua gani zilizochukuliwa na chama dhidi ya Henry Kilewo (Mkurugenzi Chadema) kwa kuweka waraka unaoitwa ripoti ya siri inayomhusu Zitto ambao chama makao makuu kupitia kwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi kimeukana mbele ya vyombo vya habari,” ilieleza taarifa hiyo.

Kilewo, ambaye pia ni kiongozi wa chama ngazi ya mkoa wa Kinondoni kichama, anadaiwa aliweka waraka huo kwenye Blog yake wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume na kanuni za viongozi wa chama kuhusu maadili ya viongozi kanuni ya 10.

“Tunataka kuona nguvu iliyotumika kuwaadhibu Zitto na wenzake kwa kuandaa waraka ujulikanao kama mkakati wa mabadiliko 2013, nguvu hiyo hiyo itumike kwa hawa waliotumia njia chafu ya kuandaa waraka wa kumchafua Zitto ambao chama kinawajua na baadhi yao tumewaweka humu kwenye tamko letu.

“Kingine tunataka kwa mara nyingine viongozi wa chama makao makuu wauambie umma wa Watanzania ni kwanini waraka huo huo unaoitwa waraka wa siri kuhusu Zitto, leo unagawiwa kwa viongozi na wanachama mikoani kwa agizo la makao makuu… kama si ubaguzi ni nini?” Taarifa hiyo ilidai.

Katika hitimisho lao, wanaumoja hao wametaka Mwenyekiti na Katibu Mkuu wajiuzulu mara moja, ili kupisha uchunguzi wa mapato na matumizi ya fedha za chama ambazo zinatokana na kodi za wavuja jasho. Pia wamependekeza uamuzi wa Kamati Kuu ubatilishwe na mchakato wa kuwavua uongozi akina Zitto ufuate taratibu na kanuni kwa mujibu wa Katiba.


Katika utaratibu ule ule wa kauli za wafuasi wa Zitto kujibiwa na wafuasi wa Mbowe, Katibu wa Vijana wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Florian Rwela, alikanusha madai hayo. Rwela alisema Gwanchele kwa sasa ni mwanachama wa kawaida anayetoka Kata ya Nyamanoro na kwamba zamani aliwahi kuwa kiongozi lakini alivuliwa madaraka kwa mujibu wa taratibu za chama.

Alisema hata kikao hicho cha wawakilishi wa matawi 189 si cha kweli kwa kuwa hakiwezi kufanyika bila yeye kupata taarifa na mwenye mamlaka ya kuratibu kikao cha namna hiyo, lazima atoke makao makuu.

Aliongeza kuwa Gwanchele anaweza kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kama mwanachama, lakini si kwa utaratibu wa kuratibu kikao cha namna hiyo.

chanzo-Bongonews

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post