Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa shinyanga ACP Kihenya Kihenya |
Watu wawili akiwemo mwandishi wa habari Mazingira Fm iliyoko
Bunda mkoani Mara wamekufa baada ya kuteketea na moto wakiwa wamelala chumbani
kutokana na moto unasadikiwa kuwa unatokana na mshumaa katika mtaa wa Shunu,kata
ya Nyahanga wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa taarifa ya kaimu kamanda wa polisi mkoa wa
Shinyanga ACP Kihenya Kihenya kwa vyombo vya habari tukio hilo limetokea jana
saa tano usiku katika mtaa wa Shunu
mjini Kahama katika nyumba ya Christina Deus(38) mkazi wa mtaa huo.
Amewataja watu waliofariki dunia kuwa ni Happiness Amos (24) mkazi wa Shunu
mjini Kahama ambaye ni mwandishi wa habari wa Radio Mazingira iliyoko Bunda
Mkoani Mara na Mariam Juma (2) ambaye pia ni mkazi wa mtaa huo.
Kamanda Kihenya amesema mbali na moto huo kusababisha vifo
vya watu wawili pia watu wengine wawili walijeruhiwa ambao ni Alfred Alphonce
(15) aliyejeruhiwa mkono wa kushoto pamoja na mmiliki wa nyumba hiyo Christina
Deus (38) ambaye aliungua mikono yote miwili na mguu wake wa kushoto.
Amesema chanzo cha moto huo inasadikiwa kuwa ni mshumaa
uliowashwa na kuwekwa juu ya kochi na kusababisha kuunguza nyumba huku
akiongeza kuwa thamani ya mali iliyoteketea bado haijajulikana na kuongeza kuwa
majeruhi waliokuwa ndani ya nyumba hiyo wamelazwa
katika hospitali ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na hali zao ni mbaya.
Social Plugin