Nhende Ng’wanandilima akipata matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar.
“Ule msemo wa wahenga, hujafa Hujaumbika ulikuwa sahihi kabisa. Wahenga waliona mbali,
wanatakiwa kuheshimiwa kwani misemo yao inaishi mpaka leo. Ni kweli binadamu kamili ni yule anayezikwa, kabla ya hapo hujakamilika.
“Unaweza kuishi na viungo vyako vyote miaka hamsini, lakini siku ya mwisho ukapata ajali, ukakatika mikono na kufa, pale ndiyo umeumbika sasa,” ndivyo anavyoanza kusimulia Nhende Ng’wanandilima (35), mkazi wa Kwimba, Mwanza ambaye amelazwa Jengo la Sewa Haji,Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar baada ya sehemu ya uso wake kuliwa na fisi aliyedai ni mtu aliyejibadili.
Akisimulia kwa majonzi tena akiwa hawezi kuzungumza sawasawa, kijana huyo alisema tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Kibetelwa, Nh’ungumalwa, Kwimba usiku wa Mei 10, 2012.
MKASA KAMILI
Akisimulia mkanda mzima wa tukio hilo, Nhende anasema: “Siku hiyo nilitoka kilabuni kunywa pombe kidogo. Nikiwa njiani narudi nyumbani sasa, nilipita kwenye pori la kijiji kile, ndipo ghafla nilianguka na kukumbana na sura ya fisi akiwa mkali sana.
“Yule fisi bila kujali mimi ni binadamu, alianza kunitafuna sura bila huruma. Alinitafuna sehemu za kuzunguka kinywa kama unavyoniona. Lilikuwa jambo la ajabu sana kwangu.
“Wakati nikipigania maisha, fisi aliendelea kunila. Nikapiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa wanakijiji ambapo walifika na kunikuta nikiendelea kupambana na yule fisi huku nikiwa nimelowa damu.
“Alikuwa fisi mwenye nguvu za ajabu na hata ule woga tunaosema fisi anao sikuuona. We fikiria, watu wamefika lakini fisi aliendelea kunitafuna bila kuogopa.
“Ilibidi wanakijiji wafanye kazi ya ziada kunitoa katika miguu na fisi ambapo sasa alikaribia kabisa kunila sehemu za siri kwani alishafika huko. Nilikuwa hoi sana. Ndipo wanakijiji wakanichukua na kunikimbiza Hospitali ya Rufaa Bugando (Mwanza) kwa matibabu zaidi,” alisema kijana huyo.
IMANI YA FISI MTU
Hata hivyo, Nhende alisema kuwa anaamini fisi aliyemfanyia kitendo kile ni binadamu aliyejigeuza kuwa mnyama huyo.
Anasema kuwa, si rahisi kwa fisi kumla binadamu, tena mtu mzima.
Alisema vitendo vya watu kuliwa na fisi katika maeneo hayo vinasababishwa na mambo ya kishirikina ambayo hayajapatiwa ufumbuzi kutokana na wahusika kutojulikana.
Alioongeza kuwa, wapo binadamu ambao kama ana chuki au kisasi na mtu anajigeuza fisi usiku na kumrarua kama alivyofanyiwa yeye na si ajabu mtu huyo huyo akatokea hospitali kumjulia hali.
KWA MUJIBU WA MADAKTARI
“Nilipofikishwa Bugando, madaktari mashuhuri wa masuala ya koo na mfumo wote wa ‘ogani’ za fahamu walijitahidi kunitibu lakini bila mafanikio. Nikaletwa hapa Muhimbili ambapo pia imeshindikana, sasa natakiwa kupelekwa India kwa matibabu zaidi.
“Wameniambia nikifika kule nitasukwa upya (plastic surgery) sehemu zote nilizoliwa na fisi. Ninachoweza kusema ni kwamba, yule fisi ameniharibia sana maisha, nina mke na watoto watano sijui nitawalisha nini, nimekuwa kilema mimi. Nimekuwa nikipata maumivu makali, sikuwahi kujua kama fisi anaweza kumla binadamu hivi
KUHUSU KWENDA INDIA
“Kuhusu safari ya India, nimeahidiwa kusafirishwa, lakini awali ya yote mimi mwenyewe natakiwa niwe na pesa zangu zisizopungua shilingi milioni moja ili kukamilisha mipango ya hati za kusafiria.
KAMA SI POMBE ANGEMSHINDA FISI
Nhende hakusita kuweka wazi kwamba, ushauri wake kwa vijana ni kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi, kwani anaamini kama asingekuwa amekunywa pombe angeweza kumshinda yule fisi.
MSAADA ANAOUOMBA KWA WATANZANIA
Nhende ameomba walioguswa na tukio lake wamsaidie kwa hali na mali ili aweze kukamilisha taratibu za usafiri wa kwenda India. Walio tayari wamchangie kupitia namba za simu +255 763 176454.
Credit: GPL
Social Plugin