Jeshi la Polisi kwa kutumia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Morogoro, wamelazimika kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa na silaha za jadi wa Kijiji cha Msowelo Wilaya ya Kilosa waliozuia mwili wa mkulima aliyeuawa na mfugaji wa jamii ya Kimasai baada ya ng’ombe watatu wa mfugaji huyo kufa katika shamba la mkulima huyo baada ya kula sumu.
Tukio hilo lilitokea jana baada ya ng’ombe watatu wa mfugaji wa jamii ya Kimasai ambaye hakufahamika jina kuingia katika shamba la mkulima huyo na kufa kwa madai ya kula sumu.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Morogoro, John Laswai alisema kuwa kundi la ng’ombe wa mfugaji huyo liliingia katika shamba la marehemu na kuanza kula majani ya nyanya chungu ambazo zilipigwa dawa kwa lengo la kuua wadudu waharibifu wa zao hilo na muda mfupi watatu walidondoka na kufa wakiwa katika shamba hilo.
Kamanda huyo alisema kuwa mara baada ya kufa, mfugaji huyo alimfuata mkulima mwenye shamba hilo ambaye ni marehemu na kumpiga rungu la kifuani na kumkata na sime sehemu za kiunoni na kusababisha kifo.
Alisema kuwa kutokana na kifo cha mkulima huyo wananchi wakiwemo vijana walianza kupigana na wafugaji wa jamii ya Kimasai kwa kutumia mawe, mishare na silaha nyingine za jadi.
Hata hivyo alisema kuwa vurugu hizo ziliendelea kushamiri na wananchi wa kijiji hicho walifunga barabara kwa kuweka mawe na magogo ya miti na kuwarushia mawe askari polisi waliofika kuuchukua mwili wa mkulima huyo. Laswai alisema kuwa polisi walifanikiwa kuondoka na mwili huo na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
CHANZO-Mwananchi
Social Plugin