Jamaa na ndugu wakiendelea na mazishi katika makaburi ya Nakonde nchini Zambia ambako mtoto Kalebu alizikwa |
Katika hali isiyo ya kawaida mmoja wa watoto wa Diwani wa Kata ya Nkangamo Weston Simwelu(55) ambaye watoto wake waliuawa kwa kuchinjwa na kunyongwa,Enock Simwelu(23) amekiri kufanya mauaji hayo kwa madai kuwa yametokana na baba yao kumrithisha mali zote marehemu mdogo wao.
Mauaji hayo yalitokea Disemba 19 eneo la TAZARA katika mji mdogo wa Tunduma ambapo wauaji walivamia nyumbani kwa Diwani huyo na kufanya mauaji ambapo walimchinja kwa kisu mtoto Kalebu Simwelu(6) na mfanyakazi wa ndani Sista Nyirenge(17) na miili yao kuficha sebuleni nyuma ya kochi.
Imeelezwa kuwa Enock pamoja na nduguye wa mama mmoja Gabriel walishirikiana kwa pamoja kufanya mauaji hayo kwa madai ya baba yao kufanya upendeleo kwa mdogo wao Kalebu(6) ambaye ni mtoto wa mke mdogo wa baba yao.
‘’Chanzo cha mauaji hayo kimebainika, mtoto wa mke mkubwa wa Diwani, Enock amekiri kuhusika na mauaji hayo ameshirikiana na nduguye Gabriel Simwelu, madai yao, baba yao amemwandikisha mali zote marehemu Kalebu, mtoto wa mke mdogo wa Diwani,’’amesema Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Barakael Masaki katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi kwa Vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda Masaki ni kwamba mmoja wa watuhumiwa walioshikiliwa kwa ajili ya mahojiano ambaye ni kaka wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Enock Simwelu(23) amedai kukiri kufanya mauaji hayo akishirikiana na mdogo wake aliyemtambulisha kwa jina la Gabriel Simwelu(19).
Kulingana na taarifa hiyo ni kwamba mtuhumiwa huyo alidai kuwa yeye amehusika moja kwa moja na mauaji hayo kutokana na tatizo la baba yake kuandikisha mali zote kwa mdogo wao ambaye ni mtoto wa mke mdogo Kalebu Simwelu.
Kamanda Masaki alisema kuwa mauaji hayo pia yalifanywa kwa kushirikiana na jirani na rafiki yao aliyefahamika kwa jina la Patrick Msigwa(18) mkazi wa eneo la Majengo katika mji mdogo wa Tunduma.
Mara baada ya kutokea kwa mauaji hayo Jeshi la Polisi liliwanasa watu watano wakiwemo watoto wa mke mkubwa wa Diwani Simwelu ambapo kulingana na madai ya awali ni kwamba chanzo kilitokana na mgogoro wa kifamilia.
Wakati tukio hilo la mauaji linatokea Baba wa marehemu Simwelu alikuwa shambani katika kijiji cha Kipaka ilhali mama mzazi wa mtoto Tumaini Yohana(29) alikuwa kazini katika Ofisi ya Halmashauri ya mji wa Tunduma.
Aidha mazishi ya mtoto Kalebu yalifanyika Disemba 21 kwenye makaburi ya Nakonde katika mji mdogo uliopo nchini Zambia na kuhudhuria na umati wa wakazi wa mpakani mwa Tanzania na Zambia ambapo mwili wa mfanyakazi wa ndani Sista Nyirenge yalifanyika katika kijiji cha Isansa wilayani Mbozi.
Social Plugin