Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amedaiwa kutoroka usiku Makao Vatican ili apate fursa ya kwenda kutoa misaada kwa walemavu na watu wasiojiweza.
Tetesi za Papa Francis kuwatembelea maskini hao usiku kwa kujificha zimekuja baada ya mahojiano yaliyofanywa na Askofu Mkuu, Konrad Krajewski ambaye kazi yake kubwa ni kukusanya fedha toka kwa wasamaria wema na kuwapelekea maskini.
Imeelezwa kuwa Askofu Krajewski amekuwa akiambatana na Papa Francis wakati mwingine na kwenda kuwapa misaada maskini maeneo ya vijiji, mjini Vatican.
Askofu Krajewski alisema tangu zamani alipokuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Buenos Aires, Papa Francis amekuwa akipenda kwenda mijini nyakati za usiku na kuwatembelea wenye shida mbalimbali.
“Amekuwa akionyesha dalili ya kupenda kunisindikiza kwenda kuwapa misaada maskini, pindi nikiondoka kwenda kufanya kazi hiyo,” alisema Padri Krajewski.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo Papa aliwahi kwenda naye nje ya mji kwa ajili hiyo, Askofu Krajewski, alisita kujibu swali hilo.
Wakati huohuo, gazeti la Huffington Post limeripoti kuwa walinzi wa Uswisi, wamethibitisha kuwa Papa amekuwa akizunguka maeneo mbalimbali usiku akiwa amevalia mavazi ya kawaida ya wachungaji na kuwapa misaada, wanaume na wanawake wenye shida mbalimbali.
Tangu kuteuliwa kwake, papa Francis amevipamba vichwa vya habari duniani baada ya kuonekana akijaribu kuvaa kofia za polisi wa zimamoto, kuwaruhusu vijana wadogo wa kiume kuibusu miguu yake na kuwapigia simu waumini wake na kuzungumza nao.
Hivi karibuni, aliripotiwa katika vyombo vya habari akiwabusu na kuwafariji waumini walemavu katika Kanisa la Mtakatifu Peter, huku taarifa nyingine zikionyesha kuwa ametuma fedha zake binafsi kwa wahamiaji na wanaohangaikia mafao yao.
Alipokuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Buenos Aires, Papa Francis alifahamika kwa kutoroka usiku na kuwatafuta watu, kuzungumza nao na wakati mwingine kuwanunulia chakula.
Mapapa wengine waliopita pia wametajwa kutoroka usiku, kwa mfano papa John wa X111 alikuwa na tabia ya kutoroka usiku na kwenda mitaa ya Rome kufurahia uzuri wa jiji hilo, wakati Papa Pius wa X11alivalia kama Mfaransa wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kwenda mipakani kuwasaidia Wayahudi wa Kirumi kisha kuwaweka katika sehemu salama.
Social Plugin