Rais Kikwete
Hayati Nelson Mandela enzi za uhai wake |
Rais wa
Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania ,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma
wa Afrika ya Kusini na kupitia kwake, kwa mkewe Bi. Graca Machel,
wanafamilia wote na wananchi wote wa Afrika ya Kusini kufuatia kifo cha Mzee
Nelson Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba, 2013 baada ya kuugua kwa
muda mrefu.
Rais ameuelezea msiba huu kuwa ni msiba mkubwa kwetu
sote.
"Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla
imepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa Karne ya 20 na 21.Tunaelewa
machungu waliyonayo wananchi wa Afrika ya Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu,
jasiri, mwana mapinduzi , mvumilivu na mstahimilivu". Ameongeza
Rais Kikwete.
Rais amemuelezea Mzee Mandela kuwa ni
kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na
upendo uliomuwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini
kuwa taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa
rangi.
"Mandela ni mfano bora kwa wanadamu
wa jinsi binadamu muungwana anavyopaswa kuwa . Ni wajibu wa wana
Afrika Kusini, Afrika na dunia kwa jumla kuiga mfano wake hasa moyo wake wa
uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake" .Rais
ameongeza kusema, "Tuzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho
ya Marehemu Mzee Mandela mahali pema peponi".
Kufuatia kifo
hicho Rais ametangaza siku 3 za maombolezo kuanzia leo tarehe 6 hadi 8 Disemba,
2013.
Aidha,
Mheshimiwa Rais ameagiza kuwa katika siku hizo 3 bendera zote
zipepee nusu mlingoti.
Mwisho.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa
Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu,
DAR AS
SALAAM.
06 Desemba,2013
Social Plugin