Wizi Mbayaaa!! WANNE WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 579 JELA KWA KUIIBIA SHULE YA MSINGI -MKOANI KATAVI,WAMO WALIMU WATATU NA MFANYA BIASHARA


Mahakama  ya wilaya ya Mpanda  Mkoa wa Katavi  imewahukumu  waalimu watatu wa Shule ya Msingi  Tukoma  iliyoko  tarafa ya Nsimbo  Wilaya ya Mlele  Mkoa wa Katavi  na mfanyabiashara wa mjini  Mpanda  kifungo cha miaka 579 jela kwa wote baada ya kupatikana na hatia ya kuiba fedha za shule  kiasi cha  shilingi milioni ishirini  na moja.

Hukumu  hiyo ilitolewa hapo jana  na Hakimu Mkazi  Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya  ya Mpanda  Chiganga Ntengwa baada ya mahakama kuwatia hatiani kwa jumla ya  makosa sitini na  nane.
Washitakiwa waliohukumiwa   ni Joel Mwakyusa (37)   Mwalimu
wa shule ya Msingi Tukoma  Mkazi wa  Kawajense  ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka  255 baada ya kupatikana na makosa arobaini ya wizi wa fedha, Lenatus Ngalo   (50)  mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Tukoma Mkazi wa Nsemlwa amehukumiwa kifungo cha miaka 148  baada ya kupatikana na hatia ya makosa 38.
Wengine waliohukumiwa ni Joachimu  Katabi  (39) Mwalimu wa shule ya Msingi Tukoma  Mkazi wa Majengo  ambae amehukumiwa kifungo cha miaka 143 na  Fredilik  Mlenje  (50) mkazi wa  Nsemulwa  Mfanyabiashara ambaye akaunti yake  ilitumika kuibia fedha hizo  shilingi milioni 21mali ya shule hiyo ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 33.
Washitakiwa hao  walidaiwa kutenda kosa hilo la wizi wa fedha za
shule ya  Msingi Tukoma   mwaka 2009  kwa kugushi  nyaraka ambazoziliwawezesha  kuiba fedha hizo kwa kupitia akaunti  ya mshitakiwa wanne  Fredilik Mlenje.
Akisoma hukumu  hiyo iliyochukua masaa mawili  kuisoma  Hakimu Mkazi Mfawidhi Chiganga Ntengwa  alisema  baada ya kusikiliza  mwenendo mzima wa  kesi  mahakama yake  imewaona  wshitakiwa  wanapatikana na makosa  kwa mujibu wa vifungu vya sheria Namba 384,335, 337,270 na 242.
Washitakiwa kabla ya kusomewa hukumu walipewa  nafasi ya kujitetea ambapo waliomba mahahama  iwasamehe kwani kuna  familia zao zinawategemea pamoja na wazazi  wao.
Baada ya maombi hayo mwendesha mashitaka Mkaguzi wa Polisi Ally Mbwijo alipinga maombi hayo na kuiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo za kuiba mali ya umma ndipo hakimu alipowasomea washitakiwa adhabu  hiyo ya kifungo jela kwa washitakiwa hao na kuwataka watakapomaliza kifungo hicho wote kwa pamoja warejeshe fedha hizo mali ya shule ya Msingi Tukoma
Na  Walter  Mguluchuma-Katavi



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post