Waziri wa Fedha, Dk. William Augustao Mgimwa (63) amefariki dunia.
Taarifa za hivi punde zinasema Waziri huyo wa fedha katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete amefariki dunia hii leo baada ya kuugua na kulazwa nchini Afrika Kusini.
Mgimwa aliyezaliwa January 20, 1950 na kuwa mbunge wa jimbo la Kalenga mkoani Iringa kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Binafsi ya Milpark ya nchini humo.
Dk. Mgimwa alikuwa mkufunzi katika Chuo cha Benki mkoani Mwanza, kabla ya kufanikiwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mkoa wa Iringa, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Hospitali hiyo ya Milpark ndiyo imekuwa ikitumiwa na Serikali ya Tanzania kupeleka watu wanaoumwa na mtu wa karibuni zaidi kuhudumiwa katika hospitali hiyo ni marehemu Dk. Sengondo Mvungi.
HIKI NDICHO ALICHOANDIKA MBUNGE WA KIGOMA KASKAZINI ZITTO KABWE KWENYE UKURASA WAKE WA FACEBOOK MUDA MCHACHE ULIOPITA
Tanzia Waziri wa Fedha William Mgimwa, Mb
Nimepokea kwa
masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Waziri wetu wa Fedha ndg. William
Mgimwa.
Kwa kipindi kifupi
nilichofanya naye kazi kwa karibu, kwanza kwenye Kamati ya Fedha (nikiwa
mkaribishwa kama Waziri wa Fedha kivuli), kisha kwenye kamati ndogo niliyounda
kuhusu miradi ya Umeme ya Mchuchuma na Liganga na Ngaka, na baadaye akiwa
Waziri wa Fedha, jambo la msingi
nilioona kwake ni unyenyekevu na heshima kubwa aliyonayo kwa watu wengine.
Hakusita kuomba ushauri licha ya kuwa na tofauti za
kivyama na kwa kweli ni Waziri wa Fedha niliyeelewana naye zaidi kuliko wengine
wote waliopita nikiwa ama Waziri Kivuli au Mwenyekiti wa Kamati za Mahesabu.
Uzalendo wake hauna mashaka
na kujituma kwake katika kazi ni tabia ya kupigiwa mfano.
Mungu ameamua kumchukua mja wake na sisi wanadamu
hatuna uwezo wa kupinga.
Nawapa pole sana
familia yake kwa kumpoteza baba yao
mpendwa. Naomba mola awape moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu.
Nawapa pole wananchi wa Jimbo la Kalenga na
Halmashauri ya Wilaya Iringa kwa kupoteza kiongozi wao.
Mola ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi.
Amina
Social Plugin