WAKATI fukuto la kufukuzwa uanachama kwenye Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) likiwa bado bichi, chama kipya cha siasa kimeanzishwa na watu wanaodaiwa kuwa ni muungano wa wanachama waliofukuzwa kutoka vyama vya upinzani nchini.
Taarifa zilizothibitishwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, zinakitaja chama hicho kuwa ni African Alliance for Change and Transparence (AACT) na kwamba mipango ya usajili wa muda wa chama hicho inadaiwa kuanza kuratibiwa kwa takribani mwezi mmoja sasa.
Tayari chama hicho kimekamilisha baadhi ya taratibu na kinatarajiwa kupewa usajili wa muda na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa siku ya Jumanne, wiki ijayo.
Imedokezwa kuwa iwapo chama hicho kitapata usajili huo, upo uwezekano wa wanachama waliofukuzwa uanachama kutoka Chadema hivi karibuni kujiunga na chama hicho.
Wanasiasa wengine wanaotajwa ama kuwa nyuma ya kuanzishwa kwa chama hicho au wanatarajia kujiunga, ni wale waliofukuzwa kutoka CUF, nia ikiwa ni kuendeleza harakati zao za kisiasa.
Mmoja wa watu wanaounda chama hicho alisema endapo chama hicho kitapata usajili baada ya hapo, taratibu na harakati za kuanza kukitangaza zitafanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema pia wamepanga kuendesha siasa zenye upinzani, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 iwapo kitakuwa tayari kimejiimarisha.
MTANZANIA Jumapili limedokezwa kuwa mchakato wa kuanzisha chama kwa wanachama waliofukuzwa upinzani, ulianza kitambo, ukilenga nia yao ya kuhakikisha wanashiriki katika chaguzi hizo.
Hivi karibuni Kamati Kuu Chadema, iliwavua uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, akikimbilia Mahakamani kuomba zuio la kutojadiliwa uanachama wake na kikao hicho.
Zitto, Dk. Kitila na Mwigamba walituhumiwa na uongozi wa juu wa Chadema kuandaa waraka wa siri wenye lengo la kufanya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, hali iliyoibua mgogoro mzito hadi kufikia uamuzi wa kuwavua uanachama baadhi yao.
Aidha taarifa nyingine ambazo MTANZANIA Jumapili limezipata zinaeleza kuwa mbali na AACT, chama kingine kilichopata usajili wa muda hivi karibuni ni Chama cha Wananchi na Demokrasia (CHAWAD).
Gazeti hili lilimtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kujua iwapo kuna chama kilichoanzishwa na wanachama waliofukuzwa upinzani, alisema hana taarifa hizo, ingawa kuna chama ambacho kimepata usajili wa muda na kingine kipo kwenye mchakato huo.
MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Mwigamba ili kujua kama anafahamu kuhusu uanzishwaji wa chama hicho, ambapo alisema hivi sasa bado hawajakaa pamoja na wenzake kujadili suala la kuanzisha chama, kutokana na kila mmoja kuwa mbali.
“Tangu maamuzi ya Kamati Kuu hatujakutana, hii ni kwa kuwa tuko mbalimbali, mimi niko Arusha na nashauriana kwanza na familia yangu nijue nini cha kufanya,” alisema Mwigamba.
Alisema hivi sasa anachokifahamu ni kwamba Dk. Mkumbo anarudi kwanza kwenye kazi yake ya awali na Zitto anasubiri uamuzi utakaotolewa dhidi ya uanachama wake.
Alipoulizwa Dk. Kitila kama ameshiriki na wenzake kuanzisha chama cha siasa, alishindwa kukataa wala kukubali, kwa kusema kuwa ukweli ama uongo wa habari hiyo utajulikana.
Alipotajiwa chama hicho na kwamba kinatarajia kupata usajili wa muda, alisema hafahamu hilo na hawezi kuzungumzia.
“Sina cha kuzungumza juu ya swali lako, kuwapo kwa chama kipya au la, nadhani ukweli utajiweka wazi nanyi mtabaini tu, hata hilo jina la chama kipya kuitwa AACT sijui,” alisema Dk. Kitila.
Mpaka sasa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu nchini ni 23, ambavyo ni CCM, CUF, Chadema, UMD, NCCR-Mageuzi, NLD, UPDP, NRA, Tadea.
Vingine ni TLP, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP, APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, Sau na AFP, UMD, FORD, CCK, ADC na Chaumma.
CHANZO-MTANZANIA
CHANZO-MTANZANIA
Social Plugin