Mwendesha bodaboda mkazi wa mtaa wa mkoani wilayani Geita amenusurika kufa leo asubuhi mara baada abiria wake aliyekuwa amembeba kumpiga nondo kichwani kisha kuanguka na kupoteza fahamu huku abiria huyo akitoweka na pikipiki hiyo kusikojulikana.
Akisimulia tukio hilo mwendesha bodaboda huyo Robert Adamu(28) aliyelazwa katika hospitali ya wilaya ya Geita wodi namba 8 amesema jana muda wa saa 12 jioni alipata mteja akimwomba ampeleke Kasamwa ili afuatilie gari aina ya Cruser iliyokuwa na mzigo wake wa laptop aliyokuwa ameisahau humo.
Ameeleza kuwa baada ya kukubalina wakaenda na walipofika Kasamwa hawakuipata gari hiyo wakaamua kurudi mjini Geita na mteja huyo kumlipa sh 16,000/= ……
“ Baada ya kunilipa pesa zangu akaniuliza wapi naweza kupata Guest kwa ajili ya kulala kwa madai kwamba yeye ni mgeni nikampeleka guest ya mtaa wa shilabela iitwayo FM na akalala chumba namba 8…..”,alieleza Robert Adam
“Baada ya kumwonesha Guest hiyo akaniomba nimwachie namba zangu za simu kwa madai kwamba kesho asubuhi atanipigia nimpeleke Katoro…………”
“Leo ilipofika saa 11 alfajiri akanipigia simu nikamfuata na kuanza safari lakini tupofika eneo la samina nje kidogo na mji wa Geita ghafla abiria huyo aliyekuwa na kibox kilichokuwa na nondo na vyuma vingine akanipiga na nondo kichwani hadi kuzimia huku akikimbia kusikojulikana”,alieleza mwendesha bodaboda huyo.
Mkuu wa usalama barabarani mkoani Geita John Mfinanga amesema amesikitishwa na tukio hilo na kuwataka waendesha bodaboda wanapopata abiria muda wa usiku wasindikizane ili linapotokea tatizo kama hili waweze kusaidiana lakini pia pindi wanapoona abiria wanamtilia mashaka wajulishe jeshi la polisi mara moja.
Kamanda wa polisi mkoani Geita Leonard Paul amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa upelelezi unaendelea kuhusu tukio hilo na kwamba linaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo.
Na Valence Robert Geita
Social Plugin