Tabia ya kutumia vitu vyenye kemikali bila ya ushauri wa kitaalamu imeendelea kujijenga miongoni mwa Watanzania, ambapo sasa dawa ya malaria aina ya Metakelfin inatumika kutengeneza kipodozi cha kurembesha nywele.
Matumizi hayo hatari ya Metakelfin yamegundulika huku kukiwa na taarifa za maji ya betri za magari, kutumika kama malighafi ya kutengeneza mkorogo unaotumiwa na baadhi ya wanawake kuchubua ngozi zao.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na shirika lisilo la kiserikali la Envirocare linalojihusisha na mpango wa kupunguza madhara yatokanayo na bidhaa za vipodozi kwa binadamu na mazingira, umebaini dawa ya malaria aina ya Metakelfin ni mojawapo ya kemikali inayotumika kienyeji katika kutengeneza kipodozi cha kurembesha nywele.
Kwa mujibu wa mtafiti Issai Sen’genge, Metakelfin ni miongoni mwa kemikali inayotumika kutengeneza mchanganyiko wa kulainisha na kurefusha nywele.
Alisema idadi kubwa ya waliohojiwa, waliitaja dawa hiyo ya malaria kuchanganywa ndani ya dawa nyingine za nywele ili kupata mchanganyiko ambao husaidia kurembesha nywele.
“Swali lilikuwa kama kuna vitu vinavyotumika katika kutengeneza mchanganyiko wa kupaka kwenye ngozi au nywele, waliohojiwa walikiri kuchanganya, Metakelfin, Jik, maji ya betri na kemikali nyingine,” anasema Seng’enge.
Kwa upande wake, Maria Kimiro ambaye ni mmiliki wa saluni ya wanawake iliyopo Makongo jijini Dar es Salaam, alikiri kusikia matumizi ya vidonge katika vipodozi lakini hana uhakika wa aina ya dawa hizo.
“Nakumbuka kuna mtu nimeshawahi kumsikia anazungumzia vidonge katika masuala ya vipodozi, lakini sina uhakika kama ndiyo hiyo Metakelfin au vidonge vingine,”anasema Kimiro.
Asha Rashidi mkazi wa Tabata jijini Dar es salaam, alikiri kuwa katika kutafuta urembo wanawake wanatumia vitu mbalimbali hata vinavyohatarisha maisha ili mradi kutimiza azma yao .
Anasema kuwa hali hiyo mara kwa mara imekuwa ikisababishwa na kuiga au kusikia kutoka kwa wengine bila kufikiria madhara ya ambacho anatarajia kukifanya.
“Binafsi sijawahi kutumia hiyo Metakelfin kwa kuwa nafahamu ni dawa ya malaria lakini naamini kuna watu ambao wanaweza kuichakachua kwa namna wanavyoweza wakidhani kwamba inaweza kuwa na matokeo mazuri kwenye ngozi au nywele,” alisema.
Wataalamu wa afya wanazungumziaje
Mtaalamu wa masuala ya Afya, Samwel Shita alisema mchanganyiko huo wa dawa unaweza kuwa na madhara makubwa katika ngozi ya mtumiaji kutokana na kemikali zinazotengenezwa.
Anafafanua kuwa Metakelfin imetengenezwa kwa ajili ya matumizi ya ndani ya mwili na endapo itatumika nje ya mwili, ina uwezekano mkubwa wa kusababisha ngozi kubabuka au ugonjwa wa saratani.
“Metakelfin ina sulphur na dawa za nywele pia zina sulphur ndani yake, endapo mchanganyiko wake utawekwa kwenye ngozi kuna hatari ya kubabuka au kusababisha saratani, hilo linatokana na kemikali hizo kuwaua bakteria wanaolinda ngozi,”alisema Shita.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza alisema licha ya kutofahamu kuhusiana na mchanganyiko huo lakini lazima utakuwa na madhara makubwa kwa mtumiaji.
“Sijawahi kusikia kuhusu hiki kitu lakini naamini huo mchanganyiko utakuwa na matokeo ambayo yanaweza kumdhuru mtumiaji, hii ina maana unajitengenezea bomu likulipue mwenyewe,” alisema.
Kuhusiana na utengenezaji wa vipodozi kienyeji alisema kuwa udhibiti wake unatokana na utashi wa mtu binafsi.
“TFDA inasimamia na kudhibiti vipodozi vilivyopo dukani hilo la watu kujichanganyia na dawa nyingine wakiwa majumbani mwao linatuwia vigumu mno ingawa tunajitahidi kutoa elimu na kuelezea madhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na michanganyiko hiyo na vipodozi kwa ujumla,” alisema.
Mara kwa mara TFDA imekuwa ikifanya jitihada za kuviweka wazi vipodozi vyenye kemikali ambazo zina madhara kwenye mwili wa binadamu.
Vipodozi hivyo ni vile vyenye sumu ambavyo ni pamoja na Carolight, inayotajwa kuwa na sumu kali zaidi pamoja na vile vyenye madini ya zebaki au mercury, ikiwamo sabuni ya Jaribu na Mekako.
Vingine ni vile vilivyochanganywa na viambata sumu kama Clobetasol na Betamethasone ambapo inatajwa pia krimu ya Amira, Betasolna Skin Success.
Matumizi yaliyokithiri ya vipodozi vyenye kemikali kwa wanawake husababishia kundi hilo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata maradhi ya saratani, figo, ini, fangasi, mzio na hata kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo au kupoteza maisha.
Aidha, utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 55 ya Watanzania hawana uelewa kuhusiana na vipodozi vilivyokatazwa kutumika kutokana na kuwa na madhara kwa mwili wa binadamu.
Utafiti huo unaonyesha kuwa licha ya jitihada kubwa ambazo zimefanyika katika kuviweka wazi na kupiga marufuku ya vipodozi vyenye kemikali idadi kubwa ya Watanzania hawana taarifa za kutosha kuhusiana na vipodozi hivyo.
Kutokana na hali hiyo watu wengi wanajikuta wakitumia vipodozi bila kufahamu kuwa vina kemikali ambazo zinaweza kuwa na madhara makubwa katika miili yao .
Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali, Sabanitho Mtega anakiri kuwa kuendelea kutumika kwa vipodozi vyenye kemikali kunatokana na baadhi ya watumiaji kutoelewa lugha iliyotumika nje ya makopo hayo na wengine kutoelewa ni kemikali gani zina madhara katika mwili wa binadamu.
Na Elizabeth Edward, Mwananchi
Social Plugin